Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf (wa nne kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wa MCL, Noor Shija, Samson Mfalila, Costantine Sebastian na Lucas Liganga. Picha na Emmanuel Herman.
Wiki iliyopita tuliona namna Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf alivyoelezea kuhusu ziara yake hapa nchini na uzoefu wa uhuru wa vyombo vya habari nchini mwake, alipokuwa kwenye mahojiano maalumu na waandishi waandamizi wa magazeti ya Mwananchi na The Citizen.
Leo anaendelea kuelezea mambo mbalimbali ikiwemo mishahara ya viongozi, umuhimu wa viongozi kulipa kodi na mabilioni yaliyofichwa kwenye benki za Uswisi. Mwandishi Wetu Noor Shija alikuwa miongozi mwa waandishi waliomuhoji Maya Graf.Endelea...
Likaulizwa swali la nyongeza kwamba anafikiri utaratibu huo utasaidia kwa Tanzania?
Balozi Chave aliendelea kujibu; sioni sababu utaratibu huu ushindwe kufanyakazi, najua umuhimu wa haki ya kupata habari na haki ya kutoa maoni. Kama kuna mtu ana matatizo apeleke malalamiko yake mahakamani.
Rais Graf aliongeza kuwa; kwenye Katiba yetu haki ya uhuru wa kutoa maoni imo kwenye kifungu cha 17 kwamba uhuru wa magazeti, redio na televisheni na aina yoyote ya njia ya upashanaji habari unalindwa kwa mujibu wa Katiba na pia mtoa habari analindwa kwa mujibu wa Katiba.
Suala la kulalamikia vyombo vya habari hata kwetu lipo na wakati mwingine linatokana na habari yenyewe kutokuwa kwenye viwango vya kiuandishi, lakini malalamiko yote hayo hupelekwa mahakamani.
Swali: Kwa kuangalia uzoefu wa kisiasa wa Uswisi, Tanzania inaweza kujifunza nini hasa katika mfumo wa uchaguzi wa vyama vingi.
Jibu: Mfumo wa kisiasa wa masuala ya uchaguzi yako katika ngazi mbalimbali ikiwemo ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya shirikisho. Kwa mfano miaka mingi iliyopita, mimi nilianza kwa kuchaguliwa katika uongozi wa ngazi ya manispaa, baadaye nikachaguliwa kwenye bunge dogo, nikachaguliwa kwenye jimbo (Uswisi ni muunganiko wa majimbo 24) na hadi sasa nimechaguliwa katika ngazi ya kitaifa.
Swali: Uswisi ina utaratibu gani katika kuhamasisha wananchi washiriki masuala yenye masilahi ya kitaifa? Kwa upande wa Tanzania, nchi ipo kwenye mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini kwa kiwango kikubwa mjadala huo umetawaliwa na wanasiasa na ushiriki wa wananchi uko kwa kiwango kidogo. Madhara yake ni yapi?
Jibu: Wananchi wamekuwa wakihusika kwa kiwango kikubwa katika masuala ya kisiasa, ambapo wananchi 50,000 katika jimbo wanaweza kuhoji sheria iliyopitishwa na bunge, wanapoona haina maslahi kwa taifa na hufanya hivyo kwa kukusanya saini zao.
Kwa wale ambao watakuwa na mapendekezo wanayotaka yajadiliwe ndani ya bunge, wanatakiwa kukusanya saini za watu kuanzia 100,000 ili mapendekezo yao yaweze kujadiliwa, lakini Bunge ndiyo lenye uamuzi wa mwisho, hakuna Bunge la Katiba kama ilivyo huku.
Alipoulizwa swali la nyongeza kwamba sheria za Uswisi hazina mwelekeo kwa kuwa zinaweza kubadilishwa wakati wowote, mradi kundi fulani limeamua kufanya hivyo. Alijibu kuwa utaratibu wa kubadili sheria mchakato wake ni mrefu ambao unaweza kuchukua mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili. Hapo Balozi Chave aliingilia kati kwa mujibu ya nyongeza kuwa mapendekezo ya wananchi baada ya kukusanya saini zao hupelekwa kwenye bunge la chini kuona kama yanafaa na baadaye hupelekwa kwenye bunge ambao nao watatoa uamuzi.
Swali: Kwa nini benki za Uswisi zinakuwa kimbilio la watu wa nje kuweka fedha zao huko, tofauti na nchi zingine za Ulaya?
Jibu: Nitazungumza wazi zaidi hapa. Watu wengi wanaweka fedha zao kwenye nchi zingine zaidi ya Uswisi na ninazijua lakini siwezi kuzitaja hapa. Lakini ni rahisi kuishambulia Uswisi kwa sababu ni nchi ndogo, na tuna mafanikio mengi na baadhi ya taasisi za fedha za kigeni zinaona uchungu kwa mafanikio yetu. Hata hivyo tumebadili mfumo wetu na kuwekwa mwingine ambao unakwamisha wale wote wenye fedha za wizi kuwekwa kwenye benki za Uswisi, kwa sababu zikibainika zinarejeshwa zilikotoka.
Swali: Mishahara ya viongozi, hasa viongozi wa juu nchini Uswisi ni siri au inaweza kuwekwa hadharani na wananchi wakaweza kuona?
Jibu: Mshahara wa viongozi wa juu wa serikali unaweza ku-google, (kwa maana unapatikana katika mtandao), mtu yeyote anaweza ku-google na akaona mshahara wa viongozi wake na pia namna unavyokatwa kodi.
Swali: Mishahara ya viongozi inakatwa kodi?
Jibu: Viongozi ni watu wa kawaida na wana wajibu kama raia wengine. kuwa kwangu spika hakunifanyi niwe tofauti na raia wengine. Inanifanya niwe raia wa kwanza wa Uswisi lakini siyo wa juu. Katika nchi yetu, viongozi wanatakiwa kuwa mfano mzuri kwa kila jambo ikiwemo kulipa kodi.
Swali: Bunge la Tanzania limekuwa na kitu kinachoonekana ni utamaduni wa kuwafukuza ndani ya ukumbi wa Bunge hasa wabunge wa upinzani kwa kinachodaiwa utovu wa nidhamu. Hali ikoje kwenye Bunge la Uswisi ni mbinu gani anazotumia Spika kuhakikisha naweka uwiano sawa kwa wabunge wote?
Jibu: Baada ya wabunge kuchaguliwa hakuna masuala ya vyama. Ambapo Balozi Chave aliongeza kuwa; Serikali ya Uswisi inaundwa na watendaji saba, ambao ndiyo mawaziri au baraza la mawaziri, hawana waziri mkuu wala hawana rais. Ndani ya baraza hilo linalochaguliwa na Bunge kwa vyama saba vikubwa kupeleka wawakilishi wao na ambalo hudumu madarakani kwa miaka minne, huteua mmoja wao kuwa rais wa nchi na uongoza kwa mzunguko wa mwaka mmoja.
Hapo liliulizwa swali lingine la nyongeza iwapo wabunge wa Bunge la Uswisi wamewahi kutwangana masumbwi. Rais Graf alijibu kuwa wabunge ndani ya Bunge lake wamekuwa wakipigana kwa hoja na siyo makonde.
Swali: Unafahamu kuwa tayari kuna hoja binafsi ndani ya Bunge letu iliyowasilishwa mwaka jana na Mbunge wa Upinzani, kuhusiana na mabilioni ya shilingi yaliyofichwa kwenye benki za Uswisi. Bunge lako tayari limewasilishiwa hoja hii?
Jibu: Hili siyo suala la Bunge ni suala kati ya Serikali yetu na Serikali ya Tanzania. (likaulizwa swali tena, lakini umesikia suala hili linashughulikiwa na Serikali yako?). Serikali yetu ni Serikali yenye kuwajibika. Nina hakika kama Serikali itakuwa imeelezwa itafanya kazi yake.
Alipobanwa zaidi kuhusu Serikali yake kushindwa kutoa taarifa kwa Serikali ya Tanzania, alijibu; hivi karibuni Serikali ya Uswisi ilisaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa kuhusu masuala ya fedha, ambao unajulikana kwa kwa jina la ‘Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters’. Tanzaniza ikisaini mkataba huo itasaidiwa na Serikali ya Uswisi kupata taarifa ya fedha zilizofichwa na Watanzania.
Mimi siyo mwanasheria, lakini Serikali ya Tanzania kuweka mkakati wa kisheria utakaotengeneza mazingira ya kubadilishana taarifa za fedha na mataifa mengine. Kwa jambo hili hata Serikali ya Uswisi inaweza kusaidia katika kupatikana kwa fedha zilizofichwa. Kwa sasa itakuwa vigumu kwa Tanzania kupata fedha hizo kwani haijasaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa za fedha na mataifa mengine.
Katika miaka ya karibuni Serikali ya Uswisi imeandaa muswada wa sheria wa kubana fedha zilizopatikana kwa njia haramu na kufichwa katika benki za Uswisi.
Sheria hiyo ikipita utaruhusu Serikali yetu kutaifisha fedha ambazo zimepatikana kwa njia ya haramu na kufichwa katika benki hizo. Muswada huo ‘Freezing and Restitution of Assets of Politically Exposed Persons obtained by Unlawful Means Bill’ ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Mei, mwaka huu.
Siyo fedha zote zilizowekwa kwenye benki ya Uswisi ni haramu kuna zingine zilipatikana kihalali, lakini zinatakiwa kutozwa kodi ambapo fedha hizo zitakazotokana na kodi zinaweza kuisaidia nchi katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Akizungumzia alichojifunza katika ziara yake nchini Tanzania, Graf alisema ni mara yake ya kwanza katika maisha yake kuona wanyama wakiwa katika maisha yao halisi ya porini, kwani aliweza kuona wanyama wengi kama vile tembo, twiga na simba wakiwa katika maisha yao ya asili.
Alisema Tanzania ina rasilimali nzuri za kuweza kuifanya kuendelea, ikiwamo mli ma Kilimanjaro, ambapo alisema si kuilinda tu pia inatakiwa kuendelezwa katika kufanikisha kukuza uchumi wa nchi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment