ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 3, 2013

Kagasheki anasa Wachina na meno ya tembo Dar

  Ni zaidi ya 200 yenye jumla ya kilo 1,834
  Ashangaa wabunge wanaotaka ajiuzulu
  Tukianza kutajana baadhi ya wabunge hawatapona
Wakati serikali ikiwa imetangaza kusitisha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ juzi bungeni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, jana amewakamata raia watatu wa China wakiwa na meno zaidi ya 200 ya tembo na pesa taslimu Sh. milioni 30.2.

Zoezi hilo liliendeshwa na Balozi Kagasheki na kikosi maalum cha polisi, ambalo liliwanasa Wachina hao waliokuwa wakiishi katika mtaa wa Faru, Mikocheni jirani na nyumba za mawaziri jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa waliokamatwa na meno hayo yenye kilo 1,834, ni Huang Qin (50), Chen Jinzhan (31) na Xu Fujie (22), wote wakiwa wazaliwa wa mji wa Guangdong, China.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Balozi Kagasheki alisema licha ya kushambuliwa bungeni na baadhi ya wabunge kuhusu operesheni hiyo, lakini hawezi kuacha ‘kuwatetea’ tembo ambao wanazidi kuangamia.

“Serikali pamoja na kusimamisha operesheni hiyo, lakini bado inalichukulia kwa uzito maangamizo ya tembo…wabunge wanaongea tu bila kujali rasilimali za nchi, siwezi kuacha kabisa kutekeleza wajibu wangu,” alisema Kagasheki.

Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa wizara yake, Tarishi Maimuna, na Mkurugenzi wa Wanyamapori, alisema pamoja na malalamiko ya wabunge, anakiri baadhi ya wananchi na mifugo wamedhurika, lakini hataacha kulinda wanyamapori.

Alisema tukio la kukamatwa kwa Wachina hao, kunaonyesha ni jinsi gani tembo wengi wanavyouawa na meno yake kusafirishwa nje ya nchi kwa kuuzwa.

“Tumesimamisha operesheni, nani atawasemea tembo…kweli ipo mifugo imeuawa katika operesheni tokomeza ujangili, lakini hatuwezi kuwaacha watu kama hawa. Tukianza kutajana baadhi ya wabunge hawatapona,” alisema.

Hata hivyo, Kagasheki alisema wabunge wasijidanganye kwamba watamng’oa madarakani, bali mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye alimuamini na kumpa wizara hiyo.

Aidha, waziri aliwashukuru wote waliofanikisha kukamatwa kwa meno hayo ya tembo, na kuamini hata kontena lililokamatwa Hong kong likiwa na shehena ya meno ya tembo, lilisafirishwa na Wachina hao.

Akizungumza baada ya kukamatwa, mtuhumiwa Qin alisema amekuwa akiletewa na rafiki tofauti tofauti ‘mzigo’ huo.

“Ipo rafiki moja moja leta hapa,” alisema Qin kwa Kiswahili kisichonyooka vizuri.

Hata hivyo, mtuhumiwa mwingine Jinzhan alijitetea kwa kusema ni mgeni hapa nchini akiwa ameingia Septemba 25, mwaka huu akitokea Uganda, na kutoelewa chochote kuhusu meno hayo.

Awali, ilielezwa Wachina hao walikuwa wakitumia gari aina ya Noah lenye namba za usajili T317 BXG kubebea mzigo huo ambao walikuwa wakiuficha katika shimo moja kiufundi ndani ya gari hilo.

Ilielezwa gari hilo wakati mwingine lilibadilishwa namba na kuwa T713 BXG, na linapofika jirani na nyumba hiyo, huzunguka zaidi ya mara tatu na kisha kuingia ndani.

Shuhuda mmoja Mtanzania anayeishi ndani ya nyumba hiyo, alisema Wachina walipata taarifa ya kuvamiwa na polisi tangu asubuhi na kuonekana kuzunguka zunguka wasijue la kufanya.

Licha ya meno hayo ya tembo, pia walikuwa ‘wakijificha’ kufanya biashara ya vitunguu swaumu, pilipili na makombe ya konokono.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: