ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2013

Malinzi amng’oa Osiah TFF

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Leodegar Tenga, Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametangaza kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Malinzi aliyetwaa madaraka hayo baada ya kumshinda Athuman Nyamlani katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika wiki moja iliyopita, pia amemteua Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo kwa sasa.
Katika taarifa yake iliyosambazwa jana kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Malinzi alisema Osiah atakwenda likizo hadi mkataba wake utakapomalizika.
Alisema uteuzi huo wa Wambura ulianza rasmi Novemba 2 mwaka huu, ambapo ameziomba klabu, vyama vya wilaya, vyama vya mikoa, vyama shiriki na wadau wa soka kumpa ushirikiano Wambura ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Naye Osiah akizungumza na gazeti hili kuhusiana na uamuzi huo wa Rais mpya wa TFF alisema,”Nimepata taarifa hizo, lakini sina cha kuzungumza kwa sasa, nitatoa tamko kesho (leo) au keshokutwa(Jumanne).
Uamuzi wa kuondolewa Osiah ulifikiwa na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana juzi Jumamosi ambayo imeridhia kumpa likizo ya malipo  hadi hapo mkataba wake utakapomalizika.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi ilizipata zinasema kuwa mkutano huo wa kamati ya utendaji ulifanyika muda mfupi baada ya rais aliyemaliza muda wake Leodegar Tenga kukabidhi ofisi rasmi kwa rais mpya Jamal Malinzi.
Mbali ya ajenda nyingine ikiwamo ya kufahamiana, Malinzi aliingiza ajenda yake binafsi na kuomba ridhaa ya wajumbe ya kutokuwa na imani na Katibu Mkuu wa TFF, Osiah.
“Baada ya Malinzi kusema hana imani na katibu, ikabidi Osiah aambiwe atoke nje ili ajadiliwe na baada ya majadiliano ya muda mrefu ndio ikaamuliwa apewe likizo ya malipo kwa muda wa miezi miwili hadi hapo mkataba wake utakapomalizika,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Mwananchi ilimtafuta Rais Malinzi kuzungumzia suala hilo, ambapo alikiri kumpumzisha Osiah na kwamba nafasi yake itakaimiwa na Boniface Wambura.
“Ni kweli Osiah tumempa likizo ya malipo mpaka mkataba wake uliosalia utakapomaliza, nafasi yake kwa sasa atakaimu Wambura mpaka mchakato wa kumpata Katibu Mkuu mpya utakapokamilika,”alisema Malinzi.
Osiah amebakiza mkataba wa miezi miwili wa kulitumikia shirikisho hilo baada ya ule wa awali kumalizika na kuongezewa miezi sita ambayo itamalizika Desemba 31 mwaka huu.
Kufuatia hali hiyo, TFF ipo kwenye mchakato wa kumlipa mshahara wake wa miezi miwili iliyosalia ikiwa ni pamoja na marupurupu mengine.
Hata hivyo Malinzi aliiambia Mwananchi kuwa mchakato wa kumpata katibu mwingine mpya unaanza mara moja kuanzia sasa, kwa nafasi hiyo kutangazwa wazi na watu kutuma maombi yao.

No comments: