Mashabiki wa Simba walisababisha uvunjifu wa amani na kung'oa viti vya Uwanja wa Taifa mwishoni mwa mchezo wa ligi kuu ya Bara uliomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.
Katika taarifa ya klabu hiyo kwa vyombo vya habari jana, Rage alisema fujo za juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam zilimshtua kwa vile si desturi ya klabu hiyo kufanya vurugu viwanjani.
"Kilichotokea jana (juzi) ni jambo la aina yake na linatakiwa kufanyiwa tafakari jadidi kubaini nini haswa kilikuwa chanzo na muktadha wa yaliyotokea," alisema Rage katika taarifa hiyo.
"Wapenzi wa Simba kwa tabia hawapendi vurugu na wamekuwa na utaratibu wa kawaida wa kuwapigia makofi wachezaji hata pale timu inapofungwa."
Rage ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa mjini Dodoma anakoendelea na vikao vya Bunge, alisema hakuna maelezo yanayoweza kutolewa kutetea uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani.
Aidha, Mbunge huyo wa Tabora Mjini (CCM) alitoa wito kwa mashabiki wa Simba kujiepusha kufanya vitendo kama hivyo katika siku zijazo.
Bodi ya Ligi imeshakemea tukio hilo na kuahidi kutoa adhabu kali ili iwe fundisho.
Rage alisema uongozi wa Simba upo tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika kwa lengo la kuhakikisha fujo katika viwanja vya soka zinakomeshwa; ili watu wazidi kwenda viwanjani badala ya kubaki majumbani wakihofia vurugu.
Baadhi ya mashabiki wa Simba waling'oa viti baada ya beki Salum Kanoni kuisawazishia Kagera Sugar kwa penalti katika dakika za majeruhi baada ya muamuzi Mohamed Theofilo kuona beki wa kati Joseph Owino alimuangusha mshambulaji Daudi Jumanne ndani ya boksi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment