ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 22, 2013

UNYUMBA NI MARIDHIANO YA PANDE ZOTE SASA KWANINI UTAKE KUMTOA ROHO MWENZIO NA POMBE ZAKO

Sada Majaliwa mkazi wa Temeke Mikoroshini jijini Dar.

Stori: IMELDA MTEMA
MWANAMKE mmoja Sada Majaliwa mkazi wa Temeke Mikoroshini jijini Dar, amedai kunusurika kutolewa roho na mumewe Mohamed Rashid hivi karibuni kwa kosa la kunyimwa unyumba.
Akizungumza na mwandishi wetu, Sada alisema siku ya tukio, mumewe alirudi nyumbani usiku akiwa amelewa na kudai unyumba kwa nguvu, jambo ambalo hakukubaliana nalo na kusababisha kutokea kasheshe kati yao.

“Siku zote nimekuwa nikimpa unyumba kama kawaida, lakini siku hiyo mwenzangu alirudi akiwa amelewa chakari, sikupendezwa na hali yake ndiyo maana sikutaka kushirikiana naye,” alifafanua Sada.

Mke huyo alisema baada ya kukataa kushiriki tendo hilo, mumewe alianza kumkaba shingoni kwa kutumia mikono yake, lakini alipoona haitoshi akachukua khanga na kuendelea kumkaba nayo.

Sada alidai kwamba hali ilikuwa mbaya na alishindwa kujiokoa kirahisi na kulazimika kumng’ata mumewe mkononi ndipo alipojiokoa huku shingo yake ikiwa imechubuka.

“Baada ya kunikaba na khanga shingoni sikuwa na jinsi ilinibidi nimng’ate ndipo aliponiachia na kupata upenyo wa kutoka nje,” alisema.

Sada alidai baada ya tukio hilo yeye na watoto wake walikimbilia kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Rehema Bakari kuomba hifadhi wakati akisubiri mwafaka na mumewe.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo mume wa Sada amekamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
“Mume wake amekatwa leo (Jumatano iliyopita) lakini nitaendelea kumhifadhi mwanamke huyu hadi pale suala lake litakapopata mwafaka,” alisema mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa.

No comments: