ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 22, 2013

WASANII KIBAO KUSINDIKIZA TAMASHA LA GURUMO TCC CLUB


Mwimbaji mkongwe nchini, Muhidin Maalim Gurumo.

BENDI za Twanga Pepeta, Msondo Ngoma na wanamuziki kibao kutoka Sikinde ni sehemu ya wasanii watakaosindikiza tamasha kubwa la Gurumo 53 litakalofanyika mwezi huu.
Tamasha hilo ambalo ni mahsusi kwa ajili ya kumuaga mwimbaji mkongwe Muhidin Maalim Gurumo litafanyika Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe Jumamosi ya Desemba 14 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kamati ya watu sita inayoratibu tamasha hilo, Gurumo anaagwa baada ya kutangaza rasmi kuachana na muziki wa jukwaani baada ya kudumu kwenye kazi hiyo kwa miaka 53.

Mratibu wa kamati hiyo Juma Mbizo amesema kutakuwa pia na wasanii wa bongo fleva, vichekesho na sarakasi.
Aidha Mbizo amesema tamasha litatanguliwa na bonanza la soka la maveterani.

Hadi kustaafu kwake Gurumo aliyezitumikia pia bendi za Kilimanjaro Chacha, Rufiji Jazz, Kilwa Jazz, Sikinde na OSS – Ndekule, alikuwa ni kiongozi na mmoja wa wamiliki wa Msondo Ngoma ambayo hapo awali ilijulikana kwa majina ya NUTTA, Juwata na OTTU. Gurumo ameitumika Msondo katika majina yote ya nyuma.

Wasanii waliowahi kuitumikia Sikinde ambao watakuwepo kumsindikiza Gurumo ni pamoja na Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Benno Villa Anton, Tshimanga Kalala Assossa na Ibrahim Mwinchande.

Baadhi ya wasanii wengine watakaotumbuiza ni Komandoo Hamza Kalala, Kassim Mapili, Hafsa Kazinja na Waziri Ali.
Kamati ya Gurumo iko chini ya uenyekiti wa Asha Baraka, makamu ni Waziri Ali na katibu ni Said Mdoe huku mratibu akiwa Juma Mbizo, wajumbe ni Said Kibiriti na Richardson Sakala. Credit GPL

No comments: