MKANDARASI anayejenga barabara ya Nzega hadi Puge mkoani Tabora amejikuta matatani baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya mradi huo.
Mkandarasi huyo, China Communications Construction Company Ltd (CCCC) kutoka China alitakiwa kukamilisha mradi huo Mei mwaka huu lakini hadi Waziri Dk. Magufuli anatembelea eneo la mradi ni asilimia 30 pekee ilikuwa imekamilika.
Kwa mujibu wa Meneja wa Barabara Mkoa wa Tabora, Injinia Damian Ndabalinze, mradi huo ulisainiwa Julai, 2010 ukitakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 27.
Naye Meneja wa Kampuni ya CCCC, Injinia Zhou Ming Tao, akijitetea kuhusu ucheleweshwaji huo alizitaja baadhi ya sababu zilizokwamisha mradi huo kuwa ni upatikanaji wa maji kwa ajili ya ujenzi na kusubiri kwa muda mrefu malipo kutoka Tanroads.
Wakati akihutubia wananchi katika viwanja vya stendi mjini Nzega, Dk. Magufuli alizikataa hoja hizo na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha kilomita 59 za mradi huo kwa kiwango cha lami ndani ya miezi saba kuanzia sasa.
“Nimefanya ziara ya kushtukiza na nimeona mkandarasi amekwisha kujenga makalvati na madaraja madogo 65 kati ya 68 hivyo kazi iliyobaki inaweza kukamilika ndani ya miezi saba endapo mkandarasi ataongeza kasi ya kazi.
“Sipo tayari kupokea visingizio vyovyote vitakavyosababisha ongezeko jingine la muda,” alisisitiza Waziri Magufuli huku akimtahadharisha msimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa viwango vya ubora vinazingatiwa.
Awali waziri huyo aliwahakikishia wananchi hao kwamba ingawa barabara hiyo itapita nje kidogo ya mji wa Nzega, kutakuwepo na barabara ya kiwango cha lami itakayounganisha barabara hiyo mpya na mji wa Nzega kwa kufuata barabara inayotumika sasa.
Ujenzi wa barabara ya Nzega hadi Tabora umegawanywa katika sehemu mbili, ya kwanza inaanzia Nzega hadi Puge na ya pili inatoka Puge kuelekea Tabora, zote zina urefu wa kilometa 114.5.
No comments:
Post a Comment