ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 22, 2013

KUJIUZULU MAWAZIRI: Wengi wapongeza lakini

Wahoji Pinda kuendelea kukalia kiti
 Wataka Makatibu wakuu, Wakurugenzi wawajibishwe
  Kagasheki apongezwa
Wanasiasa, wasomi, wanaharakati na wananchi wamesifu hatua ya kuondolewa madarakani mawaziri wanne kwa kashfa ya “Operesheni tokomeza majangili”.

Hata hivyo, wamesema uamuzi huo umechelewa kutolewa na kuhoji Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kushindwa kuchukua hatua licha ya kuona tatizo.

Juzi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo, waliondolewa kwenye nyadhifa zao baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, iliyofichua maovu yaliyofanywa kwenye Operesheni hiyo.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na NIPASHE mjini Dodoma, walisema kuwajibika kwao kumesaidia kulinda heshima ya CCM na taifa.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema ni uamuzi wa busara kwa sababu ni suala la kuwajibika kwa mambo ambayo hawakuyafanya wao bali watendaji walio chini yao.

“Kama mawaziri wasingefanya maamuzi haya ya kujiuzulu, mliona hali ya hewa ya humu ndani (Bunge) iliyokuwepo kwa sababu ni mambo ya kinyama ambayo hayajawahi kufanyika.

Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi), alimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kaghasheki, kwa kuamua kujiuzulu baada ya malalamiko ya wabunge.

“Lazima tukubali kuwa kuna matatizo ya kimfumo ambayo yamewafanya baadhi ya watendaji kuwa miungu watu,” alisema.

Alisema kuna makatibu wakuu na wakurugenzi ambao mawaziri anashindwa kuwawajibisha baada ya kujiwekea mfumo.

Mbatia alisema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye uwezo wa kufumua mfumo huo kwa kutumia tume ya uchunguzi wa kimahakama.

Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), alisema mawaziri wameonyesha uwajibikaji kwa sababu matatizo yametokea katika wizara zao wanazoziongoza.

“Tatizo limetokea kwenye wizara yako hata kama hukushiriki kwa sababu limetokea lazima uonyeshe kukomaa kwako kwa hiyo nawapongeza kwa kweli,” alisema Dk. Kafumu.

Spika wa Bunge Anne Makinda, aliwashauri mawaziri kuhakikisha kuwa wanafanya kazi katika wizara zao badala ya kuwategemea watendaji peke yao kwa sababu wanaokuja kuadhibiwa na Bunge ni wao.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema kuwa suala la mawaziri hao kujiuzulu ni hatua nzuri lakini la muhimu haki za wananchi zionekane.

Alisema pendekezo lililotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kuundwa kwa tume ya kuchunguza suala hilo, itasaidia kupatikana kwa suluhu na haki kutendeka.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba alisema kuwa wanashukuru kwa hatua hiyo licha ya kwamba imechelewa kutekelezwa kwa wakati.

Alisema kuwa awali operesheni sarangara ilipokuwa ikifanyika, Kituo cha Haki za Binadamu kilibaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuitaka serikali kuchukua hatua lakini haikufanya hivyo.

Alisema waliohusika wachukuliwe hatua ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya dola na walioumizwa walipwe fidia zao.

Simba alisema anashangazwa na kauli kuwa yote yaliyokea yanasababishwa na mfumo mbaya na kueleza kuwa kama suala hilo linajulikana lilitakiwa kurekebishwa mapema.

Hata hivyo, alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hakutakiwa kuendelea kukikalia kiti hicho kwa kuwa tangu mwanzo alijua suala hilo lakini hakuchukua hatua.

Alisema Pinda alitakiwa kuchukua hatua kabla ya wabunge kuchachamaa kwa kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka hayo. “Ninashangaa ni kwa nini hajihudhulu”.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alisema kuwa kwa bahati mbaya mawaziri huwa hawawaeliwi wanapokuwa wanawakosoa, wakati mwingine wanadhani wanafuatwa kwa sababu ya vyeo vyao.

Aliongeza kuwa mawaziri wanapokuwa hawafanyi vizuri ni wajibu wao kuwakosoa ili waende kwenye mstari lengo ni kuijenga serikali.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walisema hatua ya mawaziri wanne kutowajibika hadi kulazimishwa na Bunge kujiuzulu ni ya kuchelewa kwani maamuzi hayo yamefanywa baada ya uovu dhidi ya raia kukithiri.

Walisema taifa limekuwa na ukiukaji wa haki za binadamu mfano mauaji ya vikongwe, albino, mauaji na mashambulizi ya Mapadri Zanzibar, kuuliwa kwa bomu mwanahabari Daudi Mwangosi, kuteswa kinyama Dk. Stephen Ulimboka na watu kumwagiwa tindikali, ambayo hayajapata majibu hadi sasa.

Cecilia Ngaiza, mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akichambua suala hilo, alisema watendaji na viongozi hasa Wizara ya Mambo ya Ndani walistahili kuwajibishwa siku nyingi.

Ngaiza alisema viongozi wanajiuzulu lakini uovu unaendelea, mfano kwenye umeme mawaziri na manaibu wengi waliwajibishwa lakini mgawo upo na shida ya umeme inazidi kuongezeka.

Mwanasheria huyo alisema viongozi wengi wanapuuza sheria ama wanatumia mwanya wa kukosekana sheria na kuvunja haki za binadamu kwa kufanya wanavyotaka.

Kujiuzulu ni taswira ya kutotimiza wajibu

Mwanafunzi wa Shahada ya Ualimu, Exavery Jaston, akizungumzia hatua hiyo alisema kinachoonekana katika kazia hiyo ni mwenendo mzima wa serikali kutokuwajibika na uzembe uliojikita kwenye wizara zake.

“Kutokuwajibika huku kunatokana na mazoea ya kutokuchukua hatua kila mara makosa yanapotokea kutokana na uzembe wa dola na vyombo vyake,” alisema na kuongeza kuwa ndiyo maana udhalimu umeendelea kwani wahusika hawachukuliwi hatua.

Alisema kuvunja haki za binadamu na uongozi duni unatokana na rushwa kuota mizizi. “Hali hii itadhibitiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwajibika kwa Bunge.”

Alitaka katiba mpya iwezesha Takukuru na CHRAGG kuwajibika kwa Bunge ili kufuatilia utendaji na uwajibikaji wa vyombo hivyo.

Wabunge kuwajibishwa
Alisema wabunge wanatuhumiwa kula rushwa, kubweteka majimboni nakuisimamia serikali na kwamba hali hiyo idhibitiwe kwa katiba kuwapa wapiga kura uwezo wa kutaja wala rushwa za uchaguzi na kulibana Bunge likizembea kuisimamia serikali.

Profesa Mwesiga Beregu, ameipongeza Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Utalii, kuwawezesha Watanzania kuelewa ukatili waliofanyiwa raia kwenye operesheni tokomeza.

Alisema matendo kama hayo yamefanywa pia na operesheni kimbunga na kwenye vurumai za gesi Mtwara, hata hivyo havikubainika kutokana na kutokuwepo na chombo cha kufuatilia.

Alisema hayo yalitarajiwa kutokana na serikali kutumia jeshi kwenye zoezi ambalo lingewahusha polisi.

Akizungumzia hatua ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kutangaza kujiuzulu mbele ya Bunge, alisema ni uungwana na imemjengea heshima.

Alipinga kitendo cha Dk. David cha kujitetea akieleza kuwa kimempa doa na kuonekana sio mtu wa kukubali kuwajibika pale inapotokea tatizo katika eneo analoliongoza.

"Hakuna suala la kusema alionewa, kilichotakiwa kufanyika ni kujiuzulu kwa sababu matukio yote yamefanyika wakati anaongoza wizara hiyo," aliongeza Profesa Baregu.

Hata hivyo, alisema serikali inatakiwa kueleza chimbuko la ujangili nchini na iachane na tabia ya kuhangaika na raia ambao hawana hatia.

Naye Mwanasheria maarufu, Profesa Peter Maina, pamoja na kuwapongeza mawaziri kuamua kujiuzulu, alikemea utaratibu uliotumika katika operesheni hiyo isiyofuata sheria na kusababisha mauaji na ukatili.

Alisema kujiuzulu kwa mawaziri hao, ni dalili njema ya kuanza utaratibu wa uwajibikaji kisiasa uliokuwa ukitumika wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Akitoa mfano kuwa Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi, aliyekuwa Wazira wa Mambo ya Ndani na Peter Siyovelwa ambaye alikuwa Waziri anayeshughulikia Usalama wa Taifa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Peter Kisumo na Marco Mabawa wa Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa viongozi waliojiuzulu.

"Tulichoshuhudia miaka ya karibuni, utaratibu huo ulikufa kabisa nashukuru Mungu unarudi kwa viongozi kutambua wajibu wao na kufanya hivyo, badala ya kulazimishwa," alisema Profesa Maina.

NAPE
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi ( CCM), Nape Nnauye amesema amepokea kwa faraja kubwa, hatua ya mawaziri wanne kuenguliwa nyadhifa zao kwa ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete.

"Najisikia vizuri, maana kwa kitendo cha mawaziri hao wanne kuchukuliwa hatua, ninaamini kitasaidia wale wengine waliolala nao waamke. Bila shaka sasa hakuna atakayelala na akilala anajua itakula kwake."

DK. SLAA
Chadema, kimemng'ang'ania Waziri Mkuu, Pinda, kwa kumtaka achukue uamuzi wa kujiuzulu.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbroad Slaa, alisema baada ya mawaziri wanne kuwajibishwa kinachotakiwa iwe ni zamu ya Waziri Mkuu, Pinda kuachia ngazi na kwamba iwapo hatajiuzulu wabunge wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.

Alisema Waziri Mkuu anatakiwa kuachia ngazi kwasababu mambo mabaya na unyama waliofanyiwa wananchi na mifugo wakati operesheni hiyo ni matokeo ya kauli yake aliyowahi kuitoa Bungeni kwamba sasa serikali imechoka ni kupiga tu.

LIPUMBA
Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuenguliwa na kujiuzulu kwa mawaziri hao kunaonyesha wazi kuwa ndani ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kuna matatizo.

Alisema tayari baraza la mawazairi limekuwa likilalamikiwa na viongozi wa CCM na wabunge wake kuwa mawaziri wengi ni mizigo.

Pia alisema wabunge wa chama tawala wamekuwa wakiwalalamikia, mawaziri ambao ni waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza na naibu wake Adamu Malima, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shukuru Kawambwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Kuhusu wanajeshi kushiriki kwenye operesheni tokomeza na kudaiwa kufanya vitendo vya kikatili, Lipumba alisema jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ), jukumu lake ni kulinda mipaka ya nchi na sio kuingilia shughuli zisizo wahusu.
 
*Taarifa hii imeandaliwa na Jacqueline Massano, Gaudensia Mngumi, Moshi Lusonzo, Romana Mallya, Beatrice Shayo na Thobias Mwanakatwe
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: