Dodoma, Rukwa, Kigoma. Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, itafanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake Kivuli wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma.
Panga pangua hiyo ambayo imesukumwa na kuvuliwa nyadhifa zote kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe itawalenga pia mawaziri vivuli walioshindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema Zitto ni mlengwa mkuu wa mabadiliko hayo ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu (CC) ya chama chake.
Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe iliagiza kuvuliwa nyadhifa zote, Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo kwa kile kilichodaiwa ni kukisaliti chama.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika Mkutano wa 14 wa Bunge unaoanza leo, kambi rasmi ya upinzani imepanga kumvua rasmi Zitto nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha.
Jana, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alithibitisha kuwapo kwa mpango wa mabadiliko hayo na kwamba yanatarajiwa kufanyika kati ya mwishoni mwa wiki hii na mwanzoni mwa wiki ijayo.
“Tutakaa mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo kwa sababu Kiongozi wa Kambi (Freeman Mbowe), atafika bungeni Desemba 6, mwaka huu na ndiye Mwenyekiti wa Baraza Kivuli,” alisema Lissu na kuongeza:
“Mbali ya Zitto kuna Said Arfi (Mbunge wa Mpanda Mjini) ambaye amejiuzulu nafasi zake zote ikiwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Uchukuzi na tutaangalia ufanisi wa mawaziri wengine kivuli”.
Baraza kivuli linaundwa na mawaziri 18 wakiongozwa na Mbowe na Zitto aliyekuwa Naibu wake na Manaibu saba.
Kujitoa kwa wanachama
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki, alisema angeogopa kama kungekuwa na wimbi la wanachama zaidi ya 1,000 kuondoka katika chama kupinga misingi ya chama.
“Lakini kama walimfuata Zitto ndani ya chama ni ruksa sisi hatuna shida lakini kama ni chama hapo kuna la kuangalia… Sisi tunaamini wanachama wetu hawafuati mtu, bali misingi,” alisema
Kuhusu suala la Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi, Ally Omary Chitanda, aliyejiondoa Chadema, Lissu alisema kiongozi huyo aliondoka katika chama hicho baada ya kuona anapoteza masilahi yake.
“Huyu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Lindi, wakati huohuo alikuwa ni ofisa anayetumikia makao makuu jambo ambalo lilileta mgogoro kwa wanachama,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Yeye alitakiwa kuachia nafasi ya ofisa wa chama Makao Makuu kwa sababu wanachama walikuwa wakilalamika kwamba anakaa Dar es Salaam wakati yeye ni Mwenyekiti Lindi”.
Dk Slaa kutua jimbo la Zitto
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amesema atafanya ziara ya kukijenga chama mkoani Kigoma licha ya kuwapo taarifa inayomzuia kwa madai kwamba hali ya usalama kwa viongozi wa kitaifa kwenda huko kwa sasa si nzuri.
Hatua ya Dk Slaa imekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba wafuasi wa Chadema mkoani humo wamekasirishwa na kuvuliwa madaraka kwa Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafar Kasisiko alisema uchunguzi wao unaonyesha kuwa watu wengi mkoani humo wamejenga uhasama na uongozi wa juu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutoridhika na uamuzi wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto.
Hata hivyo, Dk Slaa alisema jana kwamba hana wasiwasi na atatua keshokutwa katika mkoa huo kuanza ziara wiki moja kuanzia Desemba 5 hadi 13 kwa lengo la kuimarisha chama.
“Mimi sijapewa taarifa hizo… wanachama wengi wananipigia wanasema wananisubiri kwa hamu na hakuna taarifa zozote mbaya,” alisema Dk Slaa akiashiria kwamba chama hicho mkoani humo kiko bega kwa bega na uongozi wa juu.
Juu Kusini waunga mkono
Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeunga mkono hatua ya Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua nyadhifa zote za uongozi Zitto, Dk Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Mratibu wa Chadema Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema uongozi na wanachama cha Chadema Nyanda za Juu Kusini wanaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na wana imani kubwa na viongozi wa juu wa Chadema.
Taarifa za nyongeza na Anthony Kayanda, Kigoma na Mussa Mwangoka, Sumbawanga.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake