Madai yetu yako wazi, hayana kificho na siyo mageni, tunaisubiri kwa hamu rasimu ya Jaji Warioba, kama ni supu isiyolika, hatutaila tutamrudishia mwenyewe na kuendeleza madai
yetu,” Seif.
Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Wazanzibar wanaisubiri kwa hamu Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuona kama imezingatia masilahi na matakwa yao katika kupata mamlaka kamili ya Zanzibar.
Msimamo huo ameutoa kwenye mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Kinyasini, Mkoa wa Kalazini Unguja na kuhudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Aidha, katika mkutano huo, kwa mara ya kwanza Waziri wa zamani wa SMZ na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mansoor Yussuf Himid alihutubia tangu avuliwe uanachama wa CCM kutokana na madai ya kwenda kinyume na sera, maadili na nidhamu ya chama hicho.
Katika maelezo yake, Maalim Seif alisema wanachodai Wazanzibar ni mamlaka kamili ni kuifanya Zanzibar ijitegemee kiuchumi, kujipangia na kujiamulia mambo yake ya ndani na nje bila ya kutegemea upande wowote.
Alisema Zanzibar ilikuwa taifa huru lililoungana na Tanganyika kwa ridhaa na siyo mateka wa Tanganyika, hivyo wanayo sababu ya kujitegemea.
“Madai yetu yako wazi, hayana kificho na siyo mageni, tunaisubiri kwa hamu rasimu ya Jaji Warioba, kama ni supu isiyolika, hatutaila tutamrudishia mwenyewe na kuendeleza madai yetu,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alisema Zanzibar itasimama wenyewe na kujiendeleza kwa kufuata misingi iliyowekwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar hayati Mzee Abeid Amani Karume.
“Madai yetu ni kama meli iliyobeba watu wengi, ikizama tunazama wote, lengo letu ni kufika salama katika bandari ya matumaini na kila mmoja aweze kunufaika na matunda ya nchi yake,” alisema Maalim Seif.
Alisema ikiwa Wazanzibari watapata Serikali, anaamini mengine yatakuja yenyewe na kuinufaisha Zanzibar kiuchumi na kusisitiza kuwa muundo wa Serikali mbili umepitwa na wakati.
Mwananchi
1 comment:
Maalim Seif hatoridhika na chochote pasipo yeye kuwa rais wa Zanzibar.Atafanya lolote lile awe rais wa Zanzibar,na hiyo ndiyo nia yake siyo ya wazanzibari kama anavyotaka kuuuaminisha umma.
Yeye angesema hadharani nataka mnipe urais wa Zanzibar ,au naomba niwe rais wenu badala ya kuwa na hoja zake binafsi na kuzifanya za wazanzibari.Mammlaka kamili ni hoja yake,inasikika vizuri masikioni mwa wengi huko zanzibar,lakini je watafaidikaje na haya mamlaka kamili? eti vingine vitakuja vyenywe, kivipi na ni vipi hivyo? hizo ndo siasa za chuki za uzanzibari na Ubara anazozianzisha,katiba inakataza kubaguana kwa namna yoyote ile na huu ni mwanzo ashughulikiwe kikatiba,aseme ni mamlaka gani anataka? kuvunja muungano ni mwiko,sasa mamlaka gani hayo ndani ya muungano?sioni hoja humo zaidi ya kuuvunja muungano.
Rasimu inataka serikali tatu,je binge la katiba litakubali ? na likikataa maalim seif atasema bara ndiyo wamekataa au baraza la katiba?hiyo supu anataka iwe na pilipili au chumvi ili anywe je ni kiasi gani cha cumvi au pilipili ili asije sema hainyweki,tumpe kwa kiasi chake.huyu mtu ajenda yake inanitisha mimi.Sitetei muungano kama hauna tija basi,uvunjwe kwa taratibu siyo kwa chuki.eti tutaangali kama hiyo supu inanywe au la!!! mtu asiye taka kitu hata ungempa chake atakikataa kudai siyo hicho,bila kujua ndo chake alichotaka.siasa za CUF ni za upande mmoja wa nchi na si nzuri hata kidogo.Wahusika msipoziba ufa mtajenga ukuta,lakini sijui kwa ghrama za nani.
Post a Comment