ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 18, 2013

MZEE SMALL AELEZEA ALIVYOMSHIKIA PANGA MGANGA NA KUMFUKUZA NYUMBANI KWAKE-3

JUZI Jumatatu, Mzee Small alikuwa akielezea kuhusiana na namna ambavyo ndugu zake walielekeza lawama kwa mkewe, Mama Said kwamba ni mtu mbaya, yeye akapinga na kutaka waachane na mawazo potofu kwa kuwa amekuwa akijitolea sana hasa katika kipindi hiki kigumu kwake.
Lakini pamoja na hivyo, Mzee Small anaeleza kwamba katika matibabu yake amepita kila sehemu. Wakati fulani aliwahi kumchukua mganga kutoka Kigoma na alipofika Dar es Salaam akamtimua.
Sababu za kumtimua ni zipi, maana itakuwa kitu cha ajabu wakati mwigizaji huyo mkongwe anataka kupona kutokana na kukabiliwa na ugonjwa wa kupooza upande mmoja wa mwili wake ? Endelea.
SUALA la kuumwa linaonyesha kurudisha nyuma mambo mengi sana ya Mzee Small hasa kuhusiana na maisha yake ya kila siku.


Katika kipindi hiki, Mzee Small amekuwa hana uwezo tena wa kufanya kazi zake za sanaa na muda mwingi anautumia kupambana na kujiuguza ili arudi katika maisha yake ya zamani.


Mzee Small ni maarufu katika eneo analoishi la Tabata na jirani zake wengi wanaonyesha mapenzi makubwa kwake kwa kuwa ameishi nao vizuri.


Kabla ya kuanza kuugua, kazi kubwa aliyokuwa akifanya ni sanaa lakini pamoja na hivyo amekuwa na mradi wake wa visima vya maji.


Wakazi wa eneo hilo kwa asilimia kubwa wamekuwa wakichota maji kwenye visima vinavyomilikiwa na Mzee Small na kipindi hiki anashindwa kufanya kazi hiyo kwa ufasaha.


Akirudi kuelezea kuhusiana na ugonjwa wake namna ambavyo umekuwa ukimweka katika wakati mgumu, Mzee Small anasema aliwahi kumuita mganga wa kienyeji kutoka mkoani Kigoma.


“Kabla ya mganga huyo kuja hapa Dar es Salaam, alitaka nimuandalie sehemu ya kulala. Basi nilifanya hivyo kwa kuwa nilikuwa nahitaji tiba,” anasema Mzee Small.


“Kweli mganga alikuja na akakuta nimemuandalia chumba, akanieleza alikuwa na uwezo wa kunitibu hadi nipone na akasema alikuwa anataka kulipwa shilingi laki tatu kwa huduma yote.


“Fedha hizo ni nyingi sana, lakini sikuwa na ujanja nikakubali na kumueleza nitamlipa, aanze tu kazi maana nilikuwa natamani sana kupona ili nirudi katika maisha yangu ya kawaida.


“Yule mganga akaanza tiba, kweli alikuwa akinichua lakini ajabu wakati anafanya kazi ya kunichua maumivu yalikuwa makali sana upande ambao ni mzima.


“Maumivu hayo ya upande uliokuwa mzima yalikuwa makali sana kuliko hata upande uliokuwa na matatizo, nikajaribu kumkumbusha mganga kwamba upande uliokuwa na matatizo ulikuwa si ule aliokuwa akiutibu.


“Lakini hakuwa anaelewa, aliendelea tu kunichua upande ambao haukuwa na matatizo huku akisisitiza kwamba upande huo ndiyo ulikuwa wenye matatizo.


“Kweli nilikuwa nataka kupona, lakini nilishindwa kuvumilia. Nilimueleza Mama Said (mkewe) kwamba nimeshindwa, maana maumivu yalikuwa makai utafikiri ananikata visu, nilishindwa.


“Siku moja akiwa ananichua, kawaida nilikuwa nalala hapa (anaonyesha kibarazani kwake), nikamuambia nimechoka na tiba hiyo maana naona ilikuwa inazidi kunipatia maumivu tu.


“Nikaamua kumfukuzia mbali, wakati ananichua nikamuambia Mama Said aingie ndani na kuleta fedha yake aliyokuwa ananidai, nikamlipa.


“Alionekana kama alikuwa hajanielewa, lakini nilimsisitiza kwamba hayo ndiyo yalikuwa malipo yake kama tulivyokubaliana. Hata kama nilikuwa sijapona, basi mara moja aondoke zake.


“Ilionekana kama haamini vile, alianza kuhoji sababu za kumfukuza wakati alikuwa akinitibu. Nikaona haelewi vizuri, nikaomba panga langu na kumtaka aondoke mara moja.”


MZEE SMALL amecharuka, amebeba panga lake na kumtaka mganga wa kienyeji kutoka Kigoma aondoke mara moja katika eneo lake la nyumbani. Lakini inaonekana kama mganga bado haelewi kinachoendelea. Je, nini kitafuatia?FUATILIA ZAIDI KESHOKUTWA IJUMAA.


SOURCE: CHAMPIONI

No comments: