Tuesday, January 14, 2014

Asasi 40 zakosa sifa Bunge la Katiba

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe

Watu 40 kutoka makundi tofauti ya kijamii wamethibitika moja kwa moja kupoteza sifa ya uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambalo vikao vyake vinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao.

Watu hao wamepoteza sifa, kutokana na kukiuka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, katika kupendekeza majina yao Ikulu ili yazingatiwe na Rais Kikwete kwenye uteuzi wake wa wajumbe wa Bunge hilo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, aliliambia NIPASHE juzi kuwa watu hao ni wale ambao waliwasilisha Ikulu jina moja tu kutoka taasisi husika, kinyume cha sheria.

Alisema kila mmoja kati ya watu kutoka taasisi husika aliyewasilisha jina hilo, alijipendekeza mwenyewe Ikulu kuomba azingatiwe na Rais kwenye uteuzi huo.

“Nasikia wamejipendekeza 40. Hiyo sheria ya wapi?” alihoji Waziri Chikawe.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, makundi ya kijamii kutoka pande zote za Muungano, yanatakiwa yawasilishe Ikulu orodha ya majina ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa ajili ya uteuzi huo na siyo mtu mmoja.

Katika kuwasilisha huko, kila kundi linatakiwa kuzingatia umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu aliyependekezwa.


Lengo la Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013 kuyataka makundi ya kijamii kutoka pande zote za Muungano, yawasilishe Ikulu orodha ya majina ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa ajili ya uteuzi huo na siyo mtu mmoja ni kuzuia uwekano wa wajanja wachache kujiteua wenyewe na kumpa Rais wigo mpana wa kufanya uteuzi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Waziri Chikawe alisema hadi sasa wanaendelea kuchambua majina zaidi ya 5,000 yaliyowasilishwa kutoka makundi hayo kabla ya kuyakabidhi kwa Rais kwa ajili ya uteuzi na kwamba kazi hiyo inaendelea vizuri.

Alisema wanatarajia wajumbe watapatikana mapema kabla ya tarehe iliyotajwa na Rais Kikwete ya kuanza kwa Bunge hilo.

“Tunachokifanya, tunachambua. Kisha tutamkabidhi Mheshimiwa Rais. Akiwa tayari, atatangaza. Kabla ya tarehe hiyo ya Bunge (wajumbe) watakuwa wameshapatikana. Kabla ya hiyo tarehe 11 Februari,” alisema Waziri Chikawe.

Idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapungua moja ya tatu ya wajumbe wote.

Kwa mujibu wa Chikawe, mchanganuo wa wajumbe hao, upo kwenye sheria.

Alisema wajumbe 20 watatoka kwenye taasisi zisizokuwa za kiserikali na kwamba, nusu yao watakuwa wanawake na moja ya tatu kutoka Zanzibar.

Wengine ni wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Chikawe alisema kuna vyama vya siasa 21 vya siasa nchini, hivyo kila chama kitapeleka wajumbe wawili na kwamba, mgawanyo utakuwa huo huo.

Alisema kwa vyama hivyo ni lazima atoke Zanzibar na mwingine Tanzania Bara na lazima mmoja awe mwanamke na mwingine mwanaume.

Wajumbe wengine na idadi yao kwenye mabano ni Taasisi za Elimu ya Juu (20), makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowakilisha wavuvi (10) na vyama vya wakulima (20).

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na jumla ya wajumbe 635.

Kati ya wajumbe hao, wanaotoka katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini ni 201, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 358 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni 76.

Kwa mujibu wa Chikawe, kati ya wajumbe 201 kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, nusu watakuwa wanawake na nusu nyingine watakuwa wanaume.

Waziri Chikawe aliliambia Bunge katika Mkutano wake wa 13 kuwa kati ya wateuliwa 201, wanawake watakuwa 101 na wanaume 100.

Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70, linatarajiwa kuanza rasmi Februari, mwaka huu, kwa ajili ya kujadili na kuipitisha rasimu ya pili ya katiba iliyopendekezwa.

Rasimu ya pili ya katiba ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka jana.
Baada ya kukabidhiwa, itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.

Katika kipindi hicho, Rais ataitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa.


Baada ya rasimu ya pili kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, itaitishwa kura ya maoni, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake