Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameingilia kati tatizo la mrundikano wa mizigo ulioanza kujitokeza katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuitisha kikao cha dharura cha watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Mrundikano huo wa mizigo inayotoka nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, umeanza kujitokeza tangu Januari Mosi, mwaka huu kufuatia TRA kuongeza matumizi katika mfumo wake mpya wa ufuatiliaji wa mizigo ujulikanao Cargo Management System (CMS).Katika kikao hicho kilichofanyika jana na kuhudhuriwa na watendaji wa TRA akiwamo Kaimu Kamishina Mkuu wa TRA, Rished Bade, taarifa zinaeleza kuwa imebainika kuwa mfumo huo mpya una matatizo ya kiufundi na TRA imekubali kuyamaliza kwa kufanya kazi pamoja na watendaji wa TPA.
Kutokana na mfumo huo kuhatarisha uchumi wa nchi, watendaji wa TRA na TPA wamekubaliana wiki ijayo watafanya uchunguzi kubaini kama matatizo yaliyojitokeza katika mfumo huo yamekwisha patiwa ufumbuzi na mamlaka husika.
Katika kikao hicho, ilibainika kuwa watendaji wa TPA walikuwa hawajafahamishwa vizuri namna ya kutumia mfumo huo, hali ambayo imekuwa ikisababisha tatizo linapojitokeza kushindwa kutatua kwa wakati.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mawakala wa mizigo katika bandari hiyo walisema wamekuwa wakipata wakati mgumu kutoka kwa wateja wao wanaotaka kutolewa mizigo yao ambao wanalazimika kukaa Dar es Salaam kwa zaidi ya siku 10 kusubiri taratibu za kupata mizigo yao zikamilike.
“Tangu matumizi ya mfumo huo, yameongezeka tunachukua hadi siku 10 kukamilisha taratibu za kutoa magari bandarini wakati siku za nyuma tulikuwa tunamaliza siku siku mbili tu, wateja wetu wanatulalamikia sana sababu wanaingia gharama kubwa kukaa Dar es Salaam,” alisema Mohamed Idd.
Mfumo huo ulianzishwa na TRA Agosti 14, mwaka jana ukiwa na lengo la kuweka rekodi za bidhaa zinazoingia nchini na unaziwezesha mamlaka hizo kufuatilia taarifa kwa ufanisi lakini bahati mbaya umekuwa ukizua malalamiko kwa mawakala wa mizigo kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa hivi sasa kuna mrundikano mkubwa wa mizigo yakiwamo magari na makontena katika Bandari ya Dar es Salaam, tatizo ambalo limeanza kujitokeza tangu Januari Mosi, mwaka huu baada ya TRA kuongeza kipengele cha Carry Out katika mfumo huo.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa mwanzoni TRA walipoanzisha mfumo huo ulitumika kwa kufanya ufuatiliaji wa mizigo inayohamishwa kwenda kwenye bandari kavu ili wateja wakachukulie huko.
Awali kabla ya TRA kuanzisha mfumo wao, kwa siku moja kuanzia saa 1:00 jioni hadi saa 12:00 asubuhi, TPA kwa kutumia mfumo wake wa Cargo System ilikuwa na uwezo wa kuhamisha magari 800 hadi 900, lakini TRA walipoanzisha mfumo wao mwaka jana yalihamishwa magari 170 tu.
Taarifa za ndani ambazo pia zimethibitishwa na baadhi ya maofisa wa TPA, zimeeleza kuwa baada ya tatizo hilo kuzidi na kutishia uchumi wa nchi, kulifanyika kikao cha watalaam wa teknolojia ya mawasiliano (ICT) ambapo baadhi ya mambo yaliboreshwa na kusaidia ongezeko la kuhamisha magari na kufikia 500 hadi 600 kwa siku hadi kufikia Desemba, mwaka jana.
Hata hivyo, kuanzia Januari Mosi, mwaka huu, TRA wameongeza matumizi ya mfumo wa CMS kwa kuanza kuutumia hata katika zoezi la wateja kuchukua mizigo yao ya kawaida baada ya kulipia kodi.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, alikiri TRA kuongeza matumizi katika mfumo wa CMS kwa kuongeza kipengele cha Carry Out ambacho kimesababisha mrundikano wa mizigo.

Watumishi bandari Dar wapelekwe Mombsa kujifunza maana ya customer services. Nafikiri inaweza kusaidia. Afrika nzima Tanzania tupo slow kwa kila kitu. Tukibaguliwa na majirani tunalalamika.
ReplyDelete