ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 3, 2014

Kikwete aingilia kati vita ya urais CCM

Mbeya. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameingilia kati vita ya kuwania urais mwaka 2015 kwa kukemea kwa baadhi ya makada wa chama hicho kuanza kampeni mapema.
Kadhalika, ameziagiza Kamati za Maadili na Usalama za chama hicho kuwachukulia hatua stahiki viongozi na wanachama wake wanaomwaga fedha ili kupata uongozi.
Rais Kikwete alizungumzia masuala hayo kwa nyakati mbili tofauti; juzi wakati alipokutana na Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya na jana kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa chama hicho.
Kauli yake imekuja wakati kukiwa na vita ya maneno baina ya makada wa chama hicho, kutokana na kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye alitangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia marafiki na jamaa zake, Januari Mosi, mwaka huu huko Monduli mkoani Arusha.
Tamko hilo lilileta hisia kuwa ametangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015 kupitia CCM na kusababisha malumbano baina ya wazee, vijana, viongozi na makada wa chama hicho wakimtuhumu kuwa anakivuruga chama kwa kutangaza nia hiyo kabla ya muda wa kampeni kuanza.
Akizungumza wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya kwenye Ukumbi wa CCM, Mbeya, Rais Kikwete alisema kuanza kwa kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha.
“Hili ni moja ya mambo yanayosikitisha. Lakini suala zima tumelikabidhi kwa Mzee Mangula (Phillip - Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara), ambaye atalisimamia na kulishughulikia,” alisema.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi ambaye alimtaka kufafanua kama kampeni zimeanza ndani ya CCM au bado.
Kumwaga fedha
Akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya jana, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema kutoa fedha kunaharibu taswira ya chama hicho na kukiweka katika hatari ya kupoteza ushindi katika chaguzi zinazokuja.
“Agizo la CCM la miaka mingi iliyopita ni kwamba kila ngazi kuwa na shughuli za kuwaingizia mapato sambamba na kuwa na mfuko wa uchaguzi. Agizo hili bado halijatekelezwa na ndiyo linakiathiri chama,” alisema Rais Kikwete.
Alisema hali hiyo imekiathiri CCM: “Hivi sasa viongozi wanachukua fedha chafu kutoka kwa watu wenye sifa mbaya na nia chafu. Hata wanaotoa rushwa hupokewa kishujaa.”
Alisisitiza wanaotoa fedha chafu kwa ajili ya kuimarisha chama lazima wahojiwe akisema wema huo wameutoa wapi ilhali walikuwapo siku zote. Alisema taswira ya chama hicho ikiwa nzuri, kitaungwa mkono na ikiwa mbaya kitachukiwa na watu.
Aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kulipa uzito unaostahili suala la uadilifu na kwamba bila kufanya hivyo chama kinaweza kuwa imara na kutekeleza majukumu yake lakini kisiungwe mkono na wananchi.
“Tusipoungwa mkono na wananchi tunaweza kupoteza ushindi. Ndiyo maana chama kikaunda Kamati ya Usalama na Maadili kufanya kazi ya kuwabana watu wanaokiuka maadili, naomba kamati hizo zifanye kazi yake ipasavyo,” alisema.
Alisema kamati hizo zisipokuwa makini zitaathiri hadhi na kukubalika kwa CCM katika jamii.
“Vitendo hivi vibaya lazima tuvikatae na tuvipige vita kwa nguvu zetu zote. Tusiwaache watu wachache wanaotaka uongozi wa gharama yoyote waharibu sifa nzuri ya CCM.”
Alisema watu hao wakiachwa itajengeka dhana potofu kwamba uongozi ndani ya CCM ni wa kununua.
Mangula kuwahoji kina Lowassa
Akizungumzia mvutano unaohusishwa na mbio za urais, Mangula alisema jana kuwa Kamati ya Maadili ya CCM itawahoji wanachama wake kadhaa wakiwamo, Lowassa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja kwa kutoa matamko ambayo yanaonekana kukiuka kanuni na maadili ya chama hicho.
Mangula ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema si hao wawili pekee watakaoitwa kwenye kamati yake, bali wapo wengi.
Alisema kazi hiyo itafanyika kabla ya kikao kijacho cha Kamati Kuu ambacho hata hivyo, hakusema kitakutana lini.

Waliolumbana na Lowassa
Malumbano kuhusu ‘safari’ ya Lowassa yalianza kwa baadhi ya wenyeviti wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku `Msukuma’ kukana kauli ya Mwenyekiti wa CCM wa Singida, Mgana Msindai kuwa wenyeviti wote wa CCM wa mikoa walikuwa wanamuunga mkono Lowassa. Hata hivyo, Msindai alikanusha suala hilo.  
Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Malecela na Mkuu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Paul Makonda pia walimtuhumu Lowassa kwamba anakivuruga chama hicho kwa kuanza kampeni mapema za urais.
Hata hivyo, kauli zao zilipingwa vikali na makada wengine wa chama hicho akiwamo Mgeja, Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Dar es Salaam, John Guninita na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Morogoro.
Mwananchi

No comments: