ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 16, 2014

Mtoto wa Rais Banda afungwa jela

Kwa ufupi

Atiwa hatiani kwa makosa ya ufisadi na kujihusisha na rushwa wakati wa utawala wa baba yake

Lusaka. Mtoto wa Rais wa zamani wa Zambia, Andrew Banda amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa hatiani katika makosa ya kuhusika na rushwa.
Andrew (53), mtoto wa aliyekuwa Rais Rupiah Banda pia aliwahi kuwa mwanadiplomasia, alikamatwa mwaka 2012 akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa Kampuni ya Fratelli Locci ya Italia iliyopewa zabuni ya ujenzi wa barabara.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Joshua Banda alisema kwamba amezingatia maelezo yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka kwamba mtuhumiwa huyo ndiye mhusika mkuu katika kosa hilo la kudai na kupokea rushwa, lakini ni mara yake ya kwanza kutiwa nguvuni.
Alisema kutokana na hali hiyo, ameona ni vyema kuangalia namna ya kumpunguzia adhabu na hivyo kumhukumu kifungo cha miezi 24 jela, lakini pia akipewa haki yake ya msingi ya kukata rufaa.
Mahakama pia ilimtia hatiani kwa kushindwa kueleza kuhusu namna alivyozipata zaidi ya Dola 63,000 zilizokuwa kwenye akaunti yake, ambazo zinadhaniwa zilipatikana kwa njia zisizokuwa halali.
Banda, naibu balozi wa zamani wa nchi hiyo nchini India na aliyewahi kuwa katibu mkuu wa ubalozi wa Zambia nchini Italia ni mmoja miongoni mwa maofisa wengi kutoka katika utawala wa baba yake walioshtakiwa kwa kujihusisha na rushwa baada ya kampeni maalumu ya kupambana na rushwa inayoongozwa na Rais wa sasa, Michael Sata.

1 comment:

Anonymous said...

Je, hili laweza kutokea Bongo in our life time?