ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 16, 2014

RAIS KIKWETE AZINDUA SERA YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA MAADILI YA UCHUMI TANZANIA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akinyanyua juu kitabu baada ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na vijana baada ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) iliyoasisiwa na Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na msanii wa vichekesho ambaye pia ni mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja Mkandamizaji baada ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA) akiwa na mwasisi wake Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission International na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam Jumamosi, Februari 15, 2014

PICHA NA IKULU

Bofya soma zaidi kusoma hotuba ya Mhe. Jakaya Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UZINDUZI WA SERA YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA MAADILI NA UCHUMI TANZANIA (MVIMAUTA), KWENYE UKUMBI WA BCIC, MBEZI BEACH, TAREHE 15 FEBRUARI, 2014

Baba Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission  International  na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya;
Mheshimiwa Sadiq Meck Sadiq, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Askofu Michael Peter Imani, Mwangalizi wa Makanisa ya WAPO Mission International, Kanda ya Dar es Salaam na Pwani;
Maaskofu Waangalizi wa Wapo Mission;
Ndugu Waumini;
Wageni Waalikwa;
 Mabibi na Mabwana;
Shukrani kwa Mwaliko
Nakushukuru sana Baba Askofu Mkuu Sylverster Gamanywa na viongozi wenzako wa Wapo Mission International kwa kunialika na  kunishirikisha katika tukio hili la kihistoria la kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA).  Nakushukuru kwa Risala ambayo imeelezea kwa ufasaha malengo na madhumuni ya MVIMAUTA na jinsi mlivyojipanga kuyatekeleza na nini mnachotegemea Serikali ifanye kusaidia utekelezaji wake.  Napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa dhati kwa ubunifu wako na kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya wewe na Kanisa lako la kulea vijana wawe raia wema na wenye manufaa kwa familia zao, jamii na taifa kwa jumla. 
Hii ni mara ya pili kwangu kushuhudia matunda ya ubunifu wako na kazi njema inayofanywa na WAPO Mission International.  Mara ya kwanza ni mwaka 2010 mliponishirikisha katika uzinduzi wa Mpango wa Kizazi Kipya Tanzania.  Matokeo ya Mpango ule ni kuanzishwa kwa Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania ambao sera yake ndiyo hii tunayoizindua leo.  Nasema hongera sana Baba Askofu Mkuu na hongereni sana viongozi na waumini wa WAPO Mission International. 
Sera ya MVIMAUTA
Ndugu Baba Askofu Mkuu;
Napata faraja ya pekee kuona kuwa mpango huu sasa umewekewa mkakati madhubuti wa utekelezaji ili malengo yake yaweze kufikiwa.  Sote tumekusikia ukieleza kwa ufasaha maudhui ya sera na mikakati ya utekelezaji wake.  Ni ukweli ulio wazi kuwa ni Sera nzuri na hakuna mpenda maendeleo wa kweli anayeweza kubeza au kukataa kuwaunga mkono.  Jambo mnalokusudia kufanya ni jema kwa nchi yetu na la manufaa kwa vijana ambao ndiyo taifa la leo na kesho.  Mnalenga kusaidia kundi muhimu linategemewa sana na familia zao, jamii na nchi yetu kwa jumla.  Kundi ambalo bahati mbaya linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaadili na kimaisha.  Lakini changamoto ni fursa za aina yake pia kwani changamoto hupanua mawazo ya watu.  Changamoto huwafanya watu kuwa wabunifu katika kutafuta majawabu.  Baba Askofu na viongozi wenzako mmefanya kile kinachostahili kufanywa.  Hongereni sana. 
          Mmelitimiza vyema jukumu la wazazi, familia, jamii na viongozi wa dini kuwapatia watoto na vijana malezi mema ili waweze kuzikabili na kushinda changamoto za kimaadili.  Najua ni kazi ngumu hasa katika dunia ya leo ya utandawazi inayoongozwa na teknolojia za kisasa za habari na mawasiliano.  Hatuna budi kuifanya kazi hiyo, tena tufanye kwa umahiri na kushinda.  Tukishindwa tutakuwa tumepata hasara kubwa kwani tutakuwa na vijana wasiokuwa waadilifu jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo na ustawi wa familia, jamii na taifa.  Na sisi lazima tuwe wabunifu tutumie utandawazi huo huo na teknolojia hizo hizo kuwajenga vijana wetu wawe na maadili mema.  Natoa pongezi nyingi kwa WAPO Mission International kwa jitihada mzifanyazo kufanikisha jambo hili muhimu na la msingi sana.  Siyo kazi rahisi lakini ni jambo linalowezekana.  Penye nia pana njia.  Dumisheni msimamo wenu na endelezeni juhudi mzifanyazo mtafanikiwa.  Mungu ni mwema atawabariki na kuwashindia kwa kazi njema muifanyayo. 
Risala
Baba Askofu Mkuu Gamanywa;
Waheshimiwa Maaskofu na Ndugu Waumini;
Sote tumekusikia Baba Askofu ukieleza kwa ufasaha kwenye risala shabaha za Sera ya Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania na jinsi mnavyokusudia na mlivyojipanga kuzitekeleza.  Lazima nikiri kuwa nimetiwa moyo na mambo mazuri mliyokusudia kufanya.  Ikiwa mtandao mnaotaka kuunda utafanya kazi kama inavyokusudiwa, nina imani baadhi ya changamoto kubwa zinazowakabili vijana nchini zitakuwa zimepata muarobaini.  Mambo mengi yameelezwa vizuri na Baba Askofu Mkuu na mimi sina sababu ya kuyarudia.  Lakini naomba nigusie machache ambayo nadhani yanahitaji kusemewa kidogo.
Kwanza naomba niwapongeze kwa hatua mliyofikia ya kuanzisha mchakato wa kusajili Chuo Kikuu cha Uongozi wa Kimaadili na Taasisi ya Kukuza Vipaji.  Naomba mkamilishe mapema usajili wa taasisi hizi za aina yake ili vijana wetu waanze kunufaika nazo.  Kuhusu umilikishwaji wa ardhi, nawashauri mpeleke maombi yenu kwa mamlaka zinazohusika  bila ya shaka mtafanikiwa.  Nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kuwawezesha kujenga taasisi hizo.  Lakini ardhi hiyo ina wenyewe wanaoimiliki.  Ama ni  wananchi mmoja mmoja au familia zao au Serikali za Vijiji au Halmashauri za Wilaya na Miji.  Ni kweli Katiba inasema ardhi yote ya nchi hii ni mali ya Rais.  Lakini Rais ni mdhamini tu wa ardhi ya nchi yetu kwa niaba ya wananchi wote.  Inampa fursa ya kutwaa ardhi ya mtu ye yote kwa manufaa ya taifa.  Hapo tunazungumzia mambo ya kitaifa ya kunufaisha wengi.  Wenye ardhi hasa ni hao niliowataja hapo juu, hivyo  anaetaka ardhi hana budi kuwaona.  Mnachotakiwa ni kutambua ardhi mnayoitaka kisha mumjue mwenyewe nani muonane nae na kuzungumza nae.  Naamini mtaelewana na wala hakapakuwa na lazima ya Rais kusema neno.
Baba Askofu;
Nimefurahi kusikia kuwa kilimo ni miongoni mwa shughuli za vikundi vitakavyoundwa katika utekelezaji wa sera hii.  Mmefikiria jambo la maana sana.  Ni ukweli ulio wazi kamba kilimo kinatoa fursa kubwa za ajira kuliko sekta nyingine yo yote.  Kilimo hakivutii watu wengi hasa vijana kwa sababu ya matumizi madogo ya teknolojia za kisasa.  Kilimo ni kazi ya shuruba kwa sababu ya kutegemea jembe la mkono na plau ya kukokotwa na ng’ombe badala ya trekta.  Inakimbiza vijana wasomi.  Kilimo kina tija ndogo kwa sababu ya kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu na matumizi madogo ya pembejeo za kisasa kama vile mbegu bora, mbolea, dawa za kuua wadudu na za kukinga na kutibu magonjwa ya mimea.  Hali kadhalika kutokutumia maarifa ya kisasa katika utayarishaji wa mashamba, upandaji na mengineyo.  Juhudi tulizozianza mwaka 2006 chini ya ASDP zina lengo la kukitoa kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa.  Tuna program za kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima na tayari wengi wananufaika.  Tunao mpango wa kuingiza matrekta na kukopesha wakulima katika vikundi vyao.  Naamini vikundi hivi navyo vinaweza kunufaika.  Pia tunao mpango wa kuanzisha Benki ya Wakulima kutoa mikopo kwa wakulima waweze kupata zana na pembejeo za kilimo.  Vikundi hivi vitanufaika pia.  Ninawatia moyo likazanieni hili la vikundi vya kilimo kwani ni jambo lenye matumaini makubwa.  Sisi Serikalini tutaendelea kushirikiana nanyi kufanikisha malengo yenu.
Tutasaidia upande wa mafunzo kwa vijana wetu.  Maafisa ugani watawaelimisha masuala ya kilimo.  Kwa wale watakaojihusisha na viwanda ni vyema mkashirikiana kwa karibu na SIDO kwani wao wanao utaalamu wa kutosha katika shughuli za namna hiyo.  Kwa suala la mitaji siwezi kusema kwamba Serikali inaweza kuwa na fedha zote zitakazohitajika.  Lakini, jungu kuu halikosi ukoko. Tutasaidiana pale tutakapoweza. Hivi sasa upo Mfuko wa kusaidia wajasiriamali na hasa kupitia vikundi vya uzalishaji mali na huduma.  Bahati mbaya mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa Mfuko, hivyo wanaopata si wengi.  Katika hao wanaopata baadhi ya vikundi hivi vinaweza kuwa miongoni mwa hao. 
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na sekta binafsi, kuangalia namna ya kuchangia katika juhudi hizi za Serikali.  Siyo lazima watoe fedha, lakini wanaweza kufungua fursa za kuwasaidia vijana katika vikundi vyao kama hivi vilivyoanzishwa na WAPO Mission International.  Wanaweza kufanya kama wanavyofanya Shirika la Nyumba la Taifa na VETA.  Imani yangu ni kuwa hivi vikundi vikisaidiwa vitakua na kuwezesha vijana wengi zaidi kujitegemea badala ya kusubiri kuajiriwa Serikalini au kwenye makampuni binafsi. 
Mwisho
Kabla ya kumaliza narudia kuwapongeza kwa jambo hili jema mlifanyalo leo.  Lakini ni sifa yenu ya miaka mingi.  Napenda kuwaahidi kuwa Serikali itajitahidi kufanya yale inayotakiwa kufanya ili sera hii tunayoizindua leo ifikie malengo yake.  We will play our part.  Mwisho nawashukuru tena kwa kunialika, nawapongeza wale wote alioshiriki kuandaa na kufanikisha shughuli hii ya leo.  Wamefanya kazi nzuri iliyotukuka.  Nawapongeza waumini na hasa vijana kwa kufika kwa wingi.  Ninyi ndiyo walengwa.  Bila ya nyie hakuna MVIMAUTA.  Naomba sote tuendelee kumuunga mkono Baba Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa na kumtia moyo azidi kufanya mambo mengi mengine mazuri katika kuwatumikia ninyi waumini wa Kanisa lake na Watanzania kwa jumla.  Tunakupenda sana.  Tunatambua na kuthamini sana kazi njema uifanyayo.  Nawaomba muendelee pia kuliombea taifa letu, liendelee kuwa na amani na utulivu na tupate mafanikio zaidi. 
Baada ya kusema hayo,  sasa natamka kwamba Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania, imezinduliwa rasmi. 
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments: