Meya
wa Jimbo la Califonia Mstahiki Osby Davis akibadilishana mawazo na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kuzungumza naye akiuongoza Ujumbe wa
Viongozi, Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Jimbo hilo kuangalia maeneo
ya uwekezaji Nchini Tanzania.
Serikali
kwa kushirikiana na Taasisi, Mashirika na Jumuiya zinazojitegemea zina
wajibu wa kuwajengea uwezo wa Kitaaluma na Uwezeshaji wananchi wenye
kipato cha chini ili kupunguza mfumo tegemezi unaonekana kuathiri
Mataifa mengi hasa yale yanayojikwamua kiuchumi Duniani.
Kauli
hiyo imetolewa na Meya wa Jimbo la California Nchini Marekani Mstahiki
Osby Davis wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mstahiki
Meya huyo wa Jimbo la California Bwana Osby Davis alisema mpango huo
ukizingatiwa vyema na pande hizo husika unaweza kwa kiasi kikubwa
kusaidia kujenga jamii itakayojiamini katika kusimamia masuala
yanayowahusu kimaisha.
Alisema
katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za
kuimarisha uchumi wake pamoja na kupunguza ukali wa maisha kwa wananachi
wake Uongozi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na Taasisi za uwekezaji upo
nchini kuangalia maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kusaidiana na
Serikali katika uwekezaji.
Alisema
kwamba wapo wafanyabiashara, wawekezaji na hata Makampuni na Taasisi
zilizokwishaonyesha nia ya kutaka kutumia fursa iliyotolewa na Zanzibar
katika suala zima la uwekezaji Vitega uchumi mbali mbali.
Akitoa
shukrani zake kwa uamuzi wa Ujumbe huo wa Viongozi na Wawekezaji wa
Jimbo la California Nchini Marekani kutembelea Zanzibar Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Sekta ya Utalii Nchini bado
ina fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinaweza kusaidia pato la Taifa.
Balozi
Seif alisema juhudi kubwa tayari zimeshachukuliwa na Serikali Kuu
katika kuimarisha miundo mbinu ya Mawasiliano, Bara bara pamoja na
Huduma za Umeme na Maji safi ili kuwajengea mazingira rahisi wawekezaji
wa Sekta ya Utalii watakaoamua kuitumia fursa hiyo.
Ujumbe
huo wa Viongozi, Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jimbo la
California Nchini Marekani ambao ulianzia ziara Tanzania Bara ulikuwepo
Zanzibar tokea Tarehe 27 Mwezi uliopita.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alifanya ziara fupi ya kukagua ujenzi wa Hoteli Mpya ya Daraja la Saba {
Grand Hayert } inayojengwa katika eneo lililokuwa Starehe Club ndani ya
Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Ujenzi
wa Hoteli hilo inayomilikiwa na Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s
unafanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi kutoka Nchini Jamuhuri ya
Watu wa China ya CRJ.
Kampuni
hiyo ya ASB Holding’s katika ujenzi wake huo imechukuwa hatua za
matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Elimu, Sayansi na
Utamaduni { UNESCO } juu ya kuendeleza hifadhi ya Mji Mkongwe wa
Zanzibar ambao umo katika makubaliano ya Hifadhi ya Kimataifa.
Ujenzi
wa Ukuta Maalum wa mita tatu kama yalivyo majengo mengine ya Mji
Mkongwe yaliyo pembezoni mwa Bahari unazingatiwa kwenye Hoteli hiyo ili
kunusuru athari yoyote ya Maji, Mazingira au matukio ya Dhoruba
yanapotokea wakati wowote.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Issa Sarboko Makarani
alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba jengo
lililokuwa Mambo msiige ambalo limeambatana na ujenzi huo linafanyiwa
matengenezo makubwa kwa kutumia chokaa ili kulinda uasili wake.
Nd.
Sarboko alisema matumizi ya saruji katika majengo ya asili ndani ya Mji
Mkongwe yaliyojengwa kwa chokaa na udongo mbali ya kuharibu mfumo wake
wa kihistoria lakini pia unaondosha ubadhubuti wa majengo hayo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza uongozi wa Hoteli
hiyo kwa juhudi zake za kuwekeza kitega uchumi kitakachosaidia kunyanyua
sekta ya Utalii ambayo hivi sasa imepewa kipaumbele na Serikali.
Uongozi
wa Hoteli hiyo ulimuhakikishia Balozi Seif kwamba ujenzi wa mradi huo
unatarajiwa kukamilika rasmi mwezi Agosti mwaka huu na ulilazimika
kuchelewa kutokana na baadhi ya vifaa vingi vya ujenzi wake kuchelewa
kufika Nchini kwa wakati uliopangwa.
Jengo
la Hoteli hiyo ya Daraja la Saba litakalokuwa na ghorofa Tatu
unatarajiwa kutoa ajira za wafanyakazi wazalendo kati ya sitini na mia
moja wakati litakapoanza kutoa huduma zake
1 comment:
Hakuna kitu kama meya wa jimbo (mkoa) la California. Jimbo lina gavana (mkuu wa mkoa). Osby Davis ni meya wa jiji la Villejo, lililopo jimbo la California.
Post a Comment