ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 5, 2014

BUNGE LA KATIBA:Pengo atoa msimamo

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ametoa msimamo wa Kanisa Katoliki nchini akisema halina msimamo rasmi kuhusu muundo wa serikali kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.

Kauli hii inafuatia habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku jana kuwa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) imetoa maoni ya Wakatoliki kutetea muundo wa serikali tatu.

Aidha, amewaasa waandishi wa habari kuwa makini juu ya masuala ya msingi wanayoyaandika, vinginevyo wanaweza wakalilaumu Kanisa kwa vitu ambavyo ni maoni ya watu binafsi.

Kardinali Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusiana na habari hiyo iliyobeba kichwa cha habari kisemacho ‘Wakatoliki watetea serikali tatu’.

Alisema si sahihi kuhusisha maoni ya tume hiyo kama msimamo wa Wakatoliki wote, kwa kuwa maoni ya tume hayawezi kufanywa kuwa maoni ya Kanisa.

“Nasisitiza hilo kwa sababu Kanisa linapotaka kutoa tamko au linapowajibika kutoa tamko ambalo lazima waumini wake wote walishike, ni wakati pale linaposhughulika au linapotamka juu ya imani au juu ya maadili,” alisema.

Kardinali Pengo alisema kwenye masuala ya imani na maadili, hapo ndipo Kanisa lina uwezo kikamilifu wa kutamka kitu, ambacho ni tamko la Kanisa.

“Kwa mfano, kumetokea pendekezo linasema Katiba yetu iseme hakuna Mungu, ni wazi hapo Kanisa linapaswa kusimama kidete na kusema hatuwezi kukubaliana na pendekezo hilo, kwa sababu liko kinyume na imani yetu,” alisema.

Alisema sehemu nyingine ambako Kanisa linaweza kutoa msimamo, ni pale inapotokea watu wakataka kutengeneza katiba inayoruhusu mambo kama ya utoaji mimba na ndoa za jinsia moja, ni dhahiri Kanisa litatoa tamko la kupinga hatua hiyo.

AFAFANUA WARAKA
Akitoa maoni kuhusu muundo wa serikali tatu kama ilivyonukuliwa kwenye gazeti, Kardinali Pengo alisema:

“Je, vipi kuhusiana na maoni mengine? Kama tume kweli ilikuwa inakwenda sambamba, inaweza kukashifu mapendekezo mengine? Kwa nini ichague juu ya serikali tatu tu, vipi wale wa serikali mbili au wale wa ile moja?”

Kardinali alipinga kuuhusisha waraka huo na Kanisa, kwa sababu hata ndani ya Kanisa, viongozi wake wana misimamo tofauti juu ya jambo hilo, hivyo waraka hauna haki ya kuharamisha ukatoliki wao, kwa sababu ya misimamo waliyonayo.

“Mimi kwa mfano, napendelea serikali mbili, msimamo ambao ni kinyume cha waraka wa tume, je, ninafukuzwa kutoka uongozi wa Kanisa kwa sababu hiyo?...Lakini kama kwa mfano, ningekuwa ninaunga mkono suala la utoaji mimba kinyume na msimamo wa Kanisa, ingekuwa haki kabisa kufukuzwa,” alisema.

KUHUSU TUME
Kardinali Pengo alisema ni haki kwa tume ya haki na amani kuwa na mapendekezo yake na ni sahihi kwa mwenyekiti wake ambaye kwa hivi sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paulo Ruzoka, kusaini tamko hilo.

“Lakini haki yake hiyo siyo kama Askofu, ni haki yake kama Mtanzania mwingine. Kama nilivyosema kwa mfano, mimi napendelea serikali mbili na ni Askofu, lakini haina maana kuwa anayetaka kuwa muumini wangu, afuate msimamo wangu,” alisema.

SABABU ZA KUTAKA SERIKALI MBILI
Alisema yeye anapendelea serikali mbili kwa sababu ana nia ya kuona Tanzania ikiwa moja na ikidumu katika umoja.

Alitofautiana na msimamo wa wanaosema kwamba serikali mbili zimeshindwa kutimiza matarajio, na akashangaa kuwa iwapo serikali mbili zimeshindwa kutimiza matarajio ya wananchi, serikali tatu zitaweza vipi kuyatimiza.

“Ndiyo yapo malalamiko toka pande zote, Bara wakisema Zanzibar imekuwa tegemezi mno, na mzigo wa kuendesha serikali mbili ni gharama na umetwikwa kwenye mabega ya Wabara, sasa mkileta serikali tatu mzigo utapungua?” Aliuliza.

Kardinali Pengo alisema kwa upande wa Zanzibar wanasema Bara wanatuzuia, wanatubana na inabidi tuwe na sauti kufanya urafiki na watu wengine tunaowataka ili watusaidie.

“Ulimwengu wa leo una matatizo mengi, yako matatizo ya Boko haram na mengine mengi, ikiwa tutatengana tunawezaje kuwaambia watu wa Zanzibar wasichague marafiki tunaohisi wanaweza kutuletea matatizo?” Aliuliza.

Alisema ukweli ni kwamba Wakatoliki wana maoni tofauti akiwamo yeye aliye muumini wa serikali mbili. Gazeti liliandika uwapo wa waraka lililodai umesambazwa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaoshiriki vikao vya Bunge hilo.

Gazeti hilo lilidai kuwa waraka huo pamoja na mambo mengine, unaunga mkono muundo wa serikali tatu, ingawa pia unaonya tabia ya baadhi ya wanasiasa kutaka kutawala mchakato wa Katiba mpya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: