Katika mada hii tunaendelea kuangalia ni kwa namna gani utakuwa mwenye umuhimu kwenye uhusiano wako. Ngoja niwachekeshe kidogo; kuna wakati niliwahi kukutana na msichana mmoja ofisini akihitaji ushauri.
Jambo lililokuwa linamsumbua ni kichekesho. Alikuwa akilalamikia kitendo cha mpenzi wake (rafiki tu) kukataa kupokea simu na kujibu meseji zake, wakati mwingine akifanya hivyo huwa kwa kuchelewa sana.
Alisema kwamba, kinachomshangaza zaidi (eti) hata anapomhitaji mwanaume wake huyo faragha humpiga chenga. Anaamini tendo la ngono kwa rafiki yake ni halali yake na akilikosa ni sawa amedharauliwa!
Nilimshangaa sana, lakini ilibidi nifanye kazi yangu ipasavyo. Nilitumia saa mbili kuzungumza naye. Alinieleza mengi, lakini kubwa ni kwamba, yule bwana alimshamchoka! Dalili zote zilionesha kwamba, hafikirii kuwa naye katika ndoa kama alivyokuwa akiwaza mwanzoni.
UMEJIFUNZA KITU?
Wepesi wa kutoa penzi na kujiachia na mwanaume ambaye hajakuoa huhatarisha nia ya ndoa. Ikumbukwe kwamba, si kila mwanaume anafaa kuwa mume na si kila mwanamke ni mke. Utajuaje uliyekutana naye kama ndiye au siye? Ni fumbo.
Wengine wanahamia kabisa kwa wanaume au wanakwenda kufua na kufanya usafi wa nyumba. Ni makosa makubwa. Unadhani ataharakisha ndoa ya nini wakati kila kitu anapata?
Yuko jamaa mmoja ambaye aliniambia kuwa, amejikuta amepoteza msisimko kwa mpenzi wake aliyedumu naye kwa miaka minne na anataka kumuacha ili aoane na mwingine.
Katika maelezo yake alisema: “Sikufichi kaka Shaluwa, nilimpenda sana mpenzi wangu lakini nahisi kama sikuwa sahihi kuwa naye. Kwanza ni mwepesi sana...hakunisumbua wakati namfuatilia, mbaya zaidi ameshatoa mimba zangu nne, wa nini mwanamke wa namna hiyo?”
Nilipomwuliza kuhusu mwanamke anayetaka kumuoa alisema: “Huyu nilikuwa naye kabla ya yule wa mwanzo. Wakati huo alikuwa sekondari, amemaliza UDSM mwaka jana - 2012 (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Ana msimamo hatari! Mpaka ninavyozungumza na wewe hajawahi kunipa penzi na mpaka sasa amenithibitishia kwamba bado ana usichana wake. Kwa nini nisimuoe mwanamke huyu mzuri, anayejitambua na kujitunza? Hawezi kunisumbua kwenye ndoa yangu kama yule mwingine.”
WANAWAKE MPO?
Kwa hiyo mmeona kumbe wanaume japo wanawalaghai muwape penzi haohao ni hodari wa kuwasema vibaya na kuwashusha thamani wakati wakiwaza kuhusu ndoa. Ni vizuri wanawake mkaamka na kujitambua na kufahamu thamani mliyonayo.
Acha kudanganyika, penzi si kigezo cha upendo wa dhati. Mbona mambo yako wazi tu! Kama anakupenda atume wazee nyumbani kwenu, taratibu muhimu zifanyike, uolewe kwa heshima na thamani yako ikiendelea kuwa juu. Mwanaume wa aina hiyo ni vigumu kukutesa.
KUWA MJANJA
Kusoma mada hii ni kitu kimoja lakini kuelewa na kubadilika ni kitu kingine. Badili utaratibu wa maisha yako huku ukizingatia kupandisha thamani ya utu wako.
Wiki ijayo nitakuambia athari za kuharakisha faragha kwenye uhusiano, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Lets Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment