ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 4, 2014

CWT WAANZA KUITIKISA SERIKALI MADAI YA SH61 BIL


MKIBA_db9e0.jpg
Dar es Salaam. Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimetangaza mgogoro na Serikali kwa kile walichodai kutofanyiwa kazi madai yao mbalimbali yakiwamo malimbikizo ya mishahara na likizo ya walimu zaidi ya Sh61 bilioni.
Madai mengine ni Serikali kutofanya maandalizi mazuri ya mfumo wa kutathmini utendaji kwa kuwapandisha walimu madaraja.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania Gratian Mukoba alisema jana kuwa, katika madai hayo matatu, hakuna lililofanyiwa kazi hivyo wamechoka kupewa ahadi hewa na Serikali ndiyo maana wamefikia hatua hiyo.
Mukoba aliiambia Mwananchi kwa simu jana kuwa Baraza la Taifa la CWT lililokaa kuanzia Januari 27 hadi 29, mwaka huu liliazimia kwamba kero za walimu ziwe zimepatiwa ufumbuzi hadi mwishoni wa Februari vinginevyo chama kitangaze mgogoro na Serikari.
"Kwa kuwa hakuna dai hata moja lililofanyiwa kazi na Serikali, hivyo kutokana na kero za walimu kutopatiwa ufumbuzi kuanzia sasa, CWT kimetengaza mgogoro na Serikali," alisema Mukoba
Alisema Serikali iliiahidi CWT kuwa Februari mwaka huu ingewalipa madai ya walimu yanayohusiana na malimbikizo ya mshahara matokeo yake imebadili ahadi hiyo na italipa taratibu kwa sababu yanahitaji kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa kuingiza madeni ili yalipwe.
Alisema vikao mbalimbali vya majadiliano ya mishahara ambavyo vimeshafanyika kutokana na maagizo ya Mahakama Kuu ya Division ya Kazi ya mwaka 2012, hakuna chochote ambacho kimeshapatikana.
Mukoba alisema madai mengine kuwa Serikali haikufanya maandalizi mazuri ya mfumo wa kutathmini utendaji kazi, kwani iligawa fomu Septemba mwaka 2013 na imejikuta kazi ya kupandisha walimu madaraja imefanywa kwa mikoa 12 na siyo kwa wilaya zote.
"Serikali imejikuta ikishindwa kupandisha walimu madaraja kwa asilimia 100, na kwa bahati mbaya sana hadi kikao cha Februari 4 mwaka huu, ni mikoa 12 tu ambayo nayo siyo wilaya zote ndiyo walimu wamepandishwa madaraja na mikoa 13 iliyobaki tumeelezwa kuwa zoezi la kuwapandisha madaraja linaendelea," alisema Mukoba.

"Tungependa kuona mambo haya pia yanatekelezwa na Serikali kama ilivyoahidi kwa walimu," alisema
chanzo: Mwananchi

No comments: