ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT � TANZANIA)
�MABADILIKO NA UWAZI�
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumatatu, 03 Machi 2014, Dar es Salaam
1. Utangulizi
Ndugu wana habari,
Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano wetu, ambao ni wa kwanza tangu chama chetu kianzishwe. Tunatambua na kuheshimu kazi yenu kama mhimili wa nne wa dola, na leo tunaomba kuzungumza na watanzania kupitia kwenu.
Lengo kuu la mkutano huu ni kukitambulisha kwenu chama kipya cha siasa kinachoitwa Alliance for Change Tanzania (ACT Tanzania) na kuwaombeni kukitambulisha chama hiki kwa watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.
2. ACT Tanzania ni nini?
Ndugu Wanahabari,
ACT � Tanzania ni kifupi cha maneno: Alliance for Change and Transparency, yaaani Umoja wa Mabadiliko na Uwazi. Ni chama kipya cha siasa kilichoanzishwa kwa lengo mahsusi la kuwaleta pamoja watanzania wanaoamini kwamba nguvu ya pamoja inahitajika katika kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi hii, na kwamba uwazi na uadilifu ni tunu ambazo taifa hili linazihitaji sana kwa sasa na baadaye.
3. Itikadi na Misingi ya ACT Tanzania
ACT Tanzania ni chama kinachoaamini katika demokrasia jamii na chenye shabaha kuu ya kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi nchini Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kuwa mabadiliko yoyote katika jamii lazima yainufaishe jamii husika, na kwamba wananchi wenyewe ni lazima washiriki katika kuleta mabadiliko hayo kwa uwazi na uzalendo. Mwongozo wa sera za ACT-Tanzania ni maendeleo shirikishi na kuhakikisha uwepo wa uongozi adili katika ngazi zote.
ACT Tanzania inaongozwa na misingi mikuu mitano ifuatayo:
i) Uzalendo
ACT-Tanzania inaamini kwamba kila mwananchi ana wajibu wa msingi kabisa wa kutoa mchango wake katika jamii na Taifa kwa ajili ya kuhifadhi ustawi wa nchi kwa ajili ya kizazi cha leo na cha baadaye. Ili wananchi waweze kutoa mchango huu kwa dhati na kwa moyo, ni muhimu mazingira yawepo ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaipenda nchi yao. Kwa msingi huu, ACT-Tanzania itajenga mazingira mwafaka ya wananchi kuipenda nchi yao ili wajitoe kikamilifu katika kuijenga na kuilinda. ACT-Tanzania itajenga mazingira yatakayoongeza uzalendo wa wananchi kwa kuhakikisha uwepo wa uwazi, ulinzi na utumiaji bora wa rasilimali za taifa na uadilifu wa viongozi.
ii) Usawa
ACT-Tanzania inaamini katika usawa katika yyanja zote. Tunaamini kwamba mafanikio ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla yatatokana na bidii katika kazi. Kwahiyo, ACT Tanzania kitapigania kuwepo usawa wa fursa na mazingira mazuri kwa wote katika kuhakikisha kwamba kila mtu na kila kundi katika jamii linakuwa na fursa sawa ya kufanya kazi za kujiajiri au kuajiriwa, na kwamba kipato kitokanacho na kazi halali ndicho kitakuwa kipimo cha mchango wake katika jamii na taifa.
iii) Uadilifu
Uadilifu katika maisha binafsi na katika jamii utakuwa ndio msingi na mwongozo mkuu wa viongozi na wanachama wa ACT-Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kwamba uadilifu ndio msingi na nguzo kuu ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine katika jamii.
iv) Uwazi na uwajibikaji
ACT Tanzania inaamini katika uwazi kwenye mambo yote ya kijamii na kitaifa. Hivyo basi viongozi na wanachama wa ACT-Tanzania wana wajibu wa kupigania uwazi katika mambo yote wanayofanya kwa ajili ya umma. Sambamba na uwazi, ACT- Tanzania inaamini kwamba kila mwananchi na kiongozi mwenye dhamana katika umma ana wajibu katika jamii na Taifa kwa ujumla na ni jukumu lake kutekeleza wajibu huo bila kinyongo. Aidha, mwanachama na kiongozi atokanaye na ACT Tanzania anapaswa kuwajibika kwa maneno na matendo yake katika utumishi au nje ya utumishi wa chama au taasisi yeyote ya umma. ACT Tanzania inaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia maendeleo.. Hivyo basi wajibu mkuu wa mwanachama wa ACT Tanzania utakuwa ni: BIDII KATIKA KAZI.
v) Demokrasia ya Kweli
ACT-Tanzania inaamini demokrasia ndiyo msingi wa kujenga fikra pevu na kueneza uhuru wa mtu, jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, viongozi na wanachama wa ACT-Tanzania watapigania uwepo wa demokrasia ya kweli katika kila ngazi, ndani na nje ya chama. Kila jambo lenye maslahi mapana katika chama na katika umma litaamuliwa kwa njia ya kidemokrasia ya moja kwa moja au kupitia kwa wawakilishi waliochaguliwa.
4. Taarifa ya Kazi na mipango ya mbele
� ACT Tanzania imekwisha kukamilisha rasimu ya awali ya Katiba ambaye iliwezesha kupata usajili wa muda
� Zoezi la kuandikisha wanachama katika mikoa kwa ajili ya kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria limekwishakamilika. Tumewapata wanachama katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hata hivyo, tumechagua mikoa kumi ambayo tungependa msajili akahakiki kama sheria inavyotaka.
� Baada ya kukamilisha zoezi la kuandikisha wanachama, wiki hii kabla ya Ijumaa tutapeleka fomu na mahitaji mengine husika kwa Msajili wa vyama ili aweze kupanga ratiba ya zoezi la uhakiki.
� Mara baada ya msajili kutoa usajili wa kudumu kwa muda atakaopanga, tutafanya uchaguzi wa kwanza mkuu
� Kama itampendeza msajili akatupatia usajili wa kudumu mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi zote ndogo zitakazojitokeza, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
5. Shukrani
� Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru waratibu wote wa zoezi zima la uandikishaji wanachama waliojitolea kwenye mikoa na wilaya mbalimbali katika kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa wakati uliopangwa.
� Natoa wito kwa wanachama na wapenzi wa chama popote walipo waendelee kukichangia chama kwa nguvu zao, muda wao, taaluma zao na kwa kila hali kadri uwezo unavyomruhsu kila moja wetu.
� Nawashukuru sana wataalam na watafiti wetu mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutumia utaalam wao kutushauri katika maeneo mbalimbali ya utafiti, uongozi, sera, raslimali, usimamizi wa fedha, mawasiliano, sheria, sayansi ya siasa, na kadhalika.
6. Wito kwa wanachama na watanzania
Tunatoa wito kwa kila mwanachama, mfuasi na mpenzi wa ACT-Tanzania popote walipo nchini kuhakikisha kwamba:
� wanazingatia misingi ya chama iliyoanishwa hapo juu katika shughuli zao zote. Wakukumbuke kila mara kwamba lengo kuu la chama hiki ni kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi katika kila ngazi. Tungependa kila shughuli ya chama iwe shirikishi na wazi kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
� anafanya kazi kwa bidii katika kukijenga chama na kushiriki maendeleo katika jamii aliyomo,
akizingatia kwamba chama hiki kinaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Hivyo, kila mwanachama ahakikishe anatoa mchango wake katika kukijenga chama na kuleta maendeleo katika jamii husika aliyomo.
� Tunawakaribisha watanzania wote popote walipo na wanaoamini katika misingi tuliyoainisha hapo juu kujiunga na ACT Tanzania. Kila mtanzania anayejiunga na chama hiki akumbuke kuchukua wajibu wake katika kukijenga chama popote pale alipo. Na akumbuke wajibu mkuu kwa mujibu wa chama hiki kuwa ni: BIDII KATIKA KAZI.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki ACT-Tanzania, ahsanteni kwa kunisikiliza!
Kadawi Lucas Limbu,
Mwenyekiti wa Taifa
ACT Tanzania.
1 comment:
It's sad day kwa watanzania wanyonge, njia ya kuiondoa CCM madarakani sio kuanzisha chama kingine Bali ni kutafuta njia mbadala kwa upinzani kuunganisha nguvu pamoja. Huu ni uchu wa madaraka ambao unaonyesha wazi unyonge wa opposition nchini. I believe kwa mtindo huu CCM watatawala millele!
Post a Comment