ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 3, 2014

WAJUMBE TISA HAWAJARIPOTI BUNGENI

Wakati wajumbe tisa kati ya 629 wa Bunge Maalumu la Katiba, hawajaonekana bungeni tangu lilipoanza shughuli zake Februari 18, mwaka huu, Ikulu imesema kuwa Rais Jakaya Kikwete hawezi kuwachukulia hatua na badala yake wenye uwezo huo ni makundi wanayotoka.
Mkurugenzi Msaidizi wa Bunge (Habari), Deogratias Egidio alisema juzi kuwa, wajumbe watatu miongoni mwa wajumbe hao tisa, wanatoka Kundi la Baraza la Wawakilishi, wanne wa Jamhuri na wawili ni wateule wa Rais.
 “Ili mjumbe wa Bunge hilo atambulike kuwa amehudhuria vikao, lazima afanyiwe usajili, kufunguliwa jalada maalumu na baadaye kurejeshewa gharama za nauli na malipo ya posho zake. “Baraza la Wawakilishi lina wajumbe 77 na kati yao, watatu bado hawajaripoti. Kati ya wajumbe wanne wa kundi la Bunge la Jamhuri ambao hawajaripoti, wawili ni wagonjwa, mmoja ana udhuru wa kikazi na mwingine hatuna taarifa naye,” alisema Egidio.
 Wajumbe wa Bunge la Jamhuri ambao hawajaonekana tangu kuanza kwa Bunge hilo ni pamoja na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya ambaye Egidio alisema wana taarifa naye na mwingine  ni mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji ambaye Bunge halina taarifa zake.
  Alisema wajumbe 201 wa kuteuliwa waliofika katika Bunge hilo ni 199, na ambao hawajafika ni wawili; Omary Hussein na Zainab Bakari Dihenga.”
 Ikulu yazungumzia wabunge ‘watoro’
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema ingawa Ikulu haina taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Bunge Maalumu kuhusu mahudhurio hayo, lakini siyo jukumu la Rais kuwalazimisha wahusika wahudhurie Bunge.
 Alisema kwa sababu wajumbe hao waliteuliwa na Rais kutokana na kupendekezwa na makundi yao, ni vyema makundi hayo yawabane watu wao kuingia bungeni.
 “Hata hivyo, walioteuliwa na Rais Kikwete wamependekezwa na makundi ili wayawakilishe, ni wajibu wa makundi hayo kuhakikisha waliowapendekezwa na wakapitishwa majina yao, wanashiriki katika mikutano hiyo,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:  “Ni wajibu wa makundi yaliyowapendekeza kuwawakilisha kuhakikisha inawasimamia na kuwahamasiha kuhudhuria mikutano hiyo.”

No comments: