ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 27, 2014

YANGA NIPE TANO

Kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema: “Tulizidiwa na Yanga kila sehemu na wote mmeona hali ilivyokuwa, tunarudi Mbeya kujipanga na mechi ijayo dhidi ya Mbeya City.” Prisons inapambana kusalia kwenye Ligi Kuu Bara.

NIPE tano! Ndiyo salamu ya mashabiki wa Yanga jana Jumatano baada ya timu yao kuisulubu bila huruma Prisons ya Mbeya kwa mabao 5-0 ndani ya Uwanja wa Taifa. Lakini bado ina kazi pevu kutetea ubingwa wake kwani vinara wa Ligi Kuu Bara, Azam FC nao walimpiga Mgambo JKT mabao 2-0.
Mholanzi wa Yanga alionyesha jeuri ya aina yake baada ya kuwaanzishia benchi nyota watano waliozoweleka kucheza kikosi cha kwanza ambao ni David Luhende, Athuman Iddi, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza. Alimuanzisha Jerry Tegete kama straika wa kati akishirikiana na Emmanuel Okwi, lakini baada ya dakika 33 alimtoa na kumuingiza Hussein Javu aliyeonyesha uhai mkubwa.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 46 na kuzidiwa pointi nne na vinara wa ligi hiyo Azam ambao jana Jumatano waliifunga Mgambo JKT mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kufikisha pointi 50.

Kipigo hicho cha mabao 5-0, pia kimeifanya Prisons ya Mbeya kubaki nafasi ya 10 ikiwa na pointi 22 katika michezo 22 ilizocheza. Mgambo nayo imebaki nafasi ya 11 ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 22.
Hata hivyo Yanga ina mchezo mmoja mkononi kwani hadi sasa imecheza mechi 21 huku Azam ikiwa imecheza mechi 22. Kila timu inatakiwa kucheza mechi 26. Mabao ya Yanga yalifungwa na Emmanuel Okwi kwa shuti kali ikiwa ni pigo la mpira wa adhabu dakika ya 20. Okwi alipiga faulo hiyo kutoka nje ya eneo la hatari, faulo hiyo ilikuja baada ya Okwi kuchezewa madhambi na Jumanne Elfadhil.
Dakika ya 35 nusura Prisons ipate bao la penalti lakini Lugano Mwangama alipaisha pigo la penalti iliyotokana na Oscar Joshua kumchezea vibaya Frank Hau.
Mrisho Ngassa aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 38 akiunganisha krosi safi ya Hussein Javu aliyeingia kuchukua nafasi ya Tegete dakika ya 33. Mabao hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga walionekana kuwa makini zaidi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 67 mfungaji akiwa Hamis Kiiza akimalizia mpira uliopigwa na Simon Msuva. Kiiza aliingia kuchukua nafasi ya Okwi ambaye ni raia mwenzie wa Uganda.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliipatia Yanga bao la nne kwa njia ya penalti dakika ya 77 baada ya Javu kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Salum Kimenya.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihitimishwa na Kiiza aliyefunga bao la tano dakika ya 88 akimalizia krosi fupi ya Javu ambaye awali aliwachambua mabeki wa Prisons kutoka nje ya eneo la hatari hadi ndani.
Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alisema: “Nafurahi wachezaji wangu wamecheza katika kiwango kizuri na wananifurahisha kuona wanabadilika siku hadi siku. Tupo katika hali nzuri sasa.”
Kwa upande wake Kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema: “Tulizidiwa na Yanga kila sehemu na wote mmeona hali ilivyokuwa, tunarudi Mbeya kujipanga na mechi ijayo dhidi ya Mbeya City.” Prisons inapambana kusalia kwenye Ligi Kuu Bara.Pluijm amchenjia Tegete
Kocha wa Yanga, Pluijm aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Nililazimika kumtoa Tegete kwa kuwa hakucheza kwa kufuata maelekezo, hiyo ni kawaida yangu kama mchezaji anashindwa kufuata maelekezo namtoa bila kuangalia amecheza dakika ngapi.”
Baada ya kuingia dakika ya 33, Javu alionyesha uhai mkubwa na kufanikiwa kusababisha mabao matatu ya Yanga. Mara kadhaa Pluijm alifurahia uchezaji wa Javu ambaye hana namba kwenye kikosi cha kwanza.
Azam yatafuna mfupa uliomshinda Simba
Katika mchezo wa Mgambo na Azam, ambao Azam imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Mkwakwani Tanga, mabao ya washindi yalifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Brian Umony. Mgambo iliifunga Simba bao 1-0 mapema mwezi huu.
Katika mchezo wa jana kikosi cha Yanga kiliwakilishwa na: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Frank Domayo,Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu), Mrisho Ngassa/Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi/Hamis Kiiza.
Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Godfrey Mageta, Fred Chundu, Peter Michael, Frank Hau na Ibrahim Mamba.

No comments: