Kwa ufupi
- Akizungumza katika moja ya mfululizo wa vipindi vya miaka 50 ya Muungano vinavyorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa), Msekwa alisema woga wa hayati Abeid Amani Karume kupinduliwa na maadui, ulikuwa ni miongoni mwa sababu za kuharakisha Muungano huo.
Dar es Salaam. Wiki mbili kabla
ya
Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa ametoboa siri ya Muungano
huo akisema “mchakato wa kuundwa kwake ulifanywa kwa siri na haraka
sana,” kutokana na upepo wa kisiasa na usalama wa kipindi hicho.
Akizungumza
katika moja ya mfululizo wa vipindi vya miaka 50 ya Muungano
vinavyorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa),
Msekwa alisema woga wa hayati Abeid Amani Karume kupinduliwa na maadui,
ulikuwa ni miongoni mwa sababu za kuharakisha Muungano huo.
Msekwa
aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano unaasisiwa,
alisema pia yeye na wenzake walichelewa kujua kwamba Mwalimu Julius
Nyerere (Rais wa Kwanza wa Tanganyika) na Rais wa Kwanza wa Zanzibar,
Karume walikuwa na majadiliano ya kuunganisha nchi hizo.
“Kikubwa
cha kusema ni kwamba mazungumzo ya Muungano huo yalifanywa kwa siri....
kwa siri sana baina ya waasisi wa nchi hizo. Kwa nini yalifanywa kwa
siri? Siyo kwa sababu walikuwa wababe, la hasha, bali kwa mazingira ya
wakati ule, kulikuwa na maadui ambao wasingependa nchi hizi kuungana,”
alisema Msekwa na kuongeza:
“Kwa woga huohuo, ndipo Mwalimu
alipokubaliana na mwenzake wafanye mazungumzo ya siri mpaka waliposaini
yale makubaliano na kunijulisha.”
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa
Spika wa Bunge la Muungano, alisema baada ya makubaliano ya Muungano,
Nyerere alimwita na kumjulisha kuwa walishakubaliana (na Karume)
kuungana, hivyo walihitaji baraka za Bunge kuridhia Muungano huo.
“Mwalimu akaniambia, ‘wewe Katibu wa Bunge unaweza ukawaita wabunge wakaja kwa harakaharaka kuridhia makubaliano?’
“Nakumbuka
siku hiyo ilikuwa Jumanne na Mwalimu alipendekeza wabunge wafike Ijumaa
ya juma hilohilo, nao wabunge wakaja wakaridhia.”
Simulizi hii ya
Msekwa kuhusu Muungano imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la muundo wa
Muungano katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na mapendekezo
yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu badala ya
Serikali mbili za sasa.
Bunge kuridhia
Aliongeza
kuwa, baada ya Bunge la Tanganyika kuridhia Mwalimu Nyerere aliutaka
muswada huo “kwa haraka sana” ili aufanye kuwa sheria na alitaka
kupelekewa kwa mkono.
“Baada ya wabunge kuridhia pale Karimjee, nikauchukua muswada na kuupeleka Ikulu, sio mbali pale.
“Mwalimu
alifurahi sana, alishajua kuwa ulikuwa umesharidhiwa kwa sababu alikuwa
anafuatilia mkutano wa Bunge kupitia redio, ukumbuke zamani hakukuwa na
televisheni,” Msekwa anasimulia.
Sababu za kuharakisha
Msekwa
alisema kulikuwa na sababu kuu mbili za kuharakisha Muungano; moja ni
Mwalimu Nyerere kutaka nguvu ya Afrika itokane na miungano ya nchi,
wakati Karume alitaka kuimarisha usalama wa Zanzibar miezi miwili baada
ya kuuondoa utawala wa Sultani Januari 12, 1964.
Aliongeza kuwa
Nyerere alikuwa amejifunza kutokana na makosa ya awali ambapo maadui
waliharibu mpango wa kuziunganisha nchi za Afrika ya Mashariki na kuwa
shirikisho.
Hata hivyo, Msekwa aliongeza kuwa, Mwalimu alimwambia
Karume wangoje kwa muda, lakini kiongozi huyo wa Zanzibar hakuafikiana
na wazo hilo kutokana na masuala yake ya kiusalama.
Alisema hata
wakati Bunge la Tanganyika likiridhia muswada wa kuanzisha Muungano,
tayari wenzao wa Zanzibar walikuwa wamekwishauridhia.
Muundo wa Muungano
Msekwa
alisema suala la kubuni muundo wa Muungano ambalo linasumbua vichwa
wajumbe wa Bunge la Katiba sasa, halikuwa tatizo kubwa wakati huo, japo
Karume alimwomba Nyerere watengeneze Serikali moja.
“Karume
alimtaka Mwalimu waunde serikali moja; yeye awe Makamu wa Rais na
Nyerere awe Rais. Lakini Mwalimu hakutaka wazo hilo akihofia maadui
wangesema ameimeza Zanzibar na pia alizingatia udogo wa nchi hiyo pamoja
na hofu ya kuwa mkoloni mamboleo,” alisimulia Msekwa.
Msekwa
alisema mara tu baada ya Nyerere kusaini muswada wa Muungano kuwa
sheria, alianza kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano na aliwachukua
wajumbe 20 kutoka Zanzibar kuingia katika Bunge la Muungano.
Alisema
baada ya Muungano huo hakukuwa na chokochoko zozote na hata maadui
waliotaka kuipindua Serikali ya Zanzibar walikata tamaa.
“Hakukuwa
na kitu kinachoitwa kero za Muungano mpaka pale Aboud Jumbe alipoingia
madarakani baada ya kifo cha Karume 1972. Jumbe na wenzake walikuwa
wanahoji Tanganyika tuliyoungana nayo ipo wapi?” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya miaka kadhaa ya uongozi wake, Jumbe alianza harakati za kuandaa Katiba ya Serikali tatu kimyakimya.
“Jumbe
alimwomba Mwalimu apatiwe mwanasheria mzoefu ili awe Mwanasheria Mkuu
Zanzibar licha ya kuwa tayari alikuwapo mwanasheria mkuu.
Nyerere
alimpatia Jaji Damian Lubuva, ambaye alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa
upande wa Muungano, huku Joseph Warioba akiwa Mwanasheria Mkuu.
Alisema
baada ya miaka takriban sita, Jumbe alimrudisha Jaji Lubuva Tanzania
bara akidai ameshampata mwanasheria mwingine na hapo siri za kuunda
Katiba mpya zilianza kugundulika mwanzoni mwa mwaka 1984.
“Jumbe
alikuwa na mpango wa kumtafuta mwanasheria mkuu kutoka Ghana.
Mwanasheria huyo walimuozesha binti wa Kizanzibari kabisa na baadaye
walianza mchakato wao wa kutengeneza Katiba ya Serikali tatu kwa siri,”
alisema Msekwa.
Hata hivyo, usiri wa Jumbe ulivuja na kumfikia
Mwalimu, ndipo katika Mkutano Mkuu wa CCM, chama kilimwadhibu kwa
kumtaka ajiuzulu na rais huyo alifanya hivyo bila hiyana.
Hata
baada ya Jumbe kujiuzulu, Msekwa alisema bado madai ya Serikali tatu
yaliendelea kuibuka katika tume mbalimbali ikiwamo ile ya Jaji Francis
Nyalali, Kundi la Wabunge (G55) na hata sasa katika Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba.
Utashi wa kisiasa
Mwanasiasa
huyo mkongwe anasema hatima ya Muungano ipo mikononi mwa wajumbe wa
Bunge la Katiba ambao jana walianza kujadili mapendekezo ya kamati
kuhusu Ibara za Kwanza na Sita za Rasimu ya Katiba, zinazozungumzia
Muungano.
“Muungano wowote unahitaji utashi wa kisiasa. Kuna watu
wanasema kero za Muungano zitaondolewa na Serikali tatu na huku wengine,
kikiwamo CCM, wanasema watahakikisha wanatatua kero hizo kwa kutumia
Serikali mbili.
Hivyo, mimi naona iwapo uamuzi wa Bunge la Katiba
utaondoa kero za Muungano, sawa na wananchi wakiridhia uamuzi huo sawa,
hakuna tatizo kwa sababu hapo awali, uamuzi ulitoka kwa Serikali pekee,”
alisema Msekwa
Mwananchi.
1 comment:
Wadau na viongozi wa Tanzania. Hivi kweli tutaelendelea kurudishana nyuma hadi lini ina maana hawa viongozi hawasomi au kuelewa mambo yanayoendelea katika dunia. Mmeendelea kubakia na mawazo ya marehemu Mwl Julius kwel;i hii si aibu mawazo yanayotolewa kila leo hayana mwelekeo tunazungumzia mambo ya miaka 50 si kutokuelewa.
TUACHENI KUWALAGHAI WATANZANIA NDUGU.
Post a Comment