ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 6, 2014

Sekta ya Nishati mwiba mchungu

Mafundi wa Shirika la umeme Tanesco wakihangaika kurekebisha nyaya za umeme ili wananchi waweze kupata huduma. Picha na Maktaba.

Dar es Salaam. Sekta ya nishati imebainika kuweka historia mbaya nchini katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 ikisababisha mitikisiko katika Serikali, kuyumbisha uchumi na kuwang’oa mawaziri zaidi ya watatu na watendaji mbalimbali wa Serikali, taasisi na mashirika yake.
Mbali na ukweli huo, kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), migogoro kuhusu miradi ya sekta hiyo imegharimu maisha ya watu, wakiwamo 12 waliouawa wakati wa vurugu za mkoani Mtwara, waliokuwa wakipinga gesi hiyo isisafirishwe kwenda jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Serikali ilidai waliouawa ni watu watatu.
Migogoro na tuhuma katika sekta hiyo ndiyo iliyosababisha kuondoka madarakani kwa mawaziri Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishari wa wakati huo akiwamo Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu mwaka 2008, kutokana na kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond Development Corporation.
Migogoro na tuhuma kwenye sekta hiyo, pia zilimwondoa madarakani William Ngeleja aliyerithi uwaziri wa Nishati na Madini kutoka kwa Nazir Karamagi.
Katika kipindi hicho cha miaka 20, kuanzia miaka ya tisini, kwa nyakati tofauti, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwamo Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na nchi washirika wamekuwa wakihangaikia kufanya mabadiliko katika sekta hiyo.
Hata hivyo, jitihada hizo zimekuwa zikirudishwa nyuma na migogoro mbalimbali iliyoitikisa sekta hiyo, mingi ikihusisha mikataba tata ya ufuaji wa umeme baina ya wazalishaji binafsi na Shirika la Umeme Tanzania  (Tanesco).
Katika kipindi cha ndani ya miaka 10 iliyopita, sekta hiyo nyeti imesababisha hasara ya mabilioni ya shilingi, huku ikitikisa nguzo muhimu za siasa, hasa katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Sekta hiyo ya nishati inajumuisha sekta ndogo za umeme, mafuta ya petroli, gesi pamoja na nishati mbadala ya upepo na mvuke.
Hata hivyo, umeme ndiyo umekuwa kiini kikuu cha matatizo kutokana na uwekezaji wake kuhusisha fedha nyingi zinazosemekana kuvutia mianya ya ufisadi na rushwa.
Baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu wanatuhumiwa kuliingiza taifa katika hasara kutokana na kutozingatia weledi na uzalendo, wakati wa kusaini mikataba na wazabuni wa miradi ya umeme.
Kamishna wa Nishati
Kamishna wa Nishati na Petroli wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hosea Mbise, alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa matatizo yaliyojitokeza katika sekta hiyo kwa miaka mingi, sasa hayatajirudia na kwamba watumishi watakaobainika kuiyumbisha wataadhibiwa mapema.
“Matatizo mengi yaliyoikumba sekta ya nishati yalikuwa ni ya kimfumo na kiutumishi, lakini sasa mabadiliko ya sera na sheria yaliyofanywa na Serikali yatazima migogoro iliyokuwepo na kuongeza ufanisi,” alisema Mbise.
Kiini cha tatizo
Mbise alisema matatizo mengi yaliikumba sekta ya nishati kutokana na kutojiandaa na mabadiliko, hivyo kusababisha msukumo wa mabadiliko hayo katika muda mfupi.
“Tanesco na Serikali kwa jumla hatukuwa tumejiandaa na mabadiliko yoyote ya mahitaji ya kinishati. Zaidi ya asilimia 80 ya umeme nchini ulikuwa ukizalishwa kwa maji na asilimia 20 iliyobaki ilizalishwa kwa mafuta,” alisema Mbise.
Alibainisha kuwa ukame wa miaka 1992, 1994, 1997 na 2003 hadi 2005 ulileta upungufu wa maji ya kuzalisha umeme, hali iliyoisababishia Serikali kutafuta njia mbadala za kukabiliana na tatizo hilo ikiwamo ufuaji wa umeme wa dharura.
“Uzalishaji wa umeme nchini ni ghali sana na wawekezaji wengi wanakwepa kuwekeza kutokana na hofu ya kutorudisha fedha zao za uwekezaji. Bei ya umeme ipo chini kiasi cha kutotoa mwelekeo wowote wa faida,” alisema Mbise hivi karibuni.
Aliongeza kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuendesha Tanesco kwa kuwa gharama ya uendeshaji ni kubwa kuliko mapato wanayopata.
“Mpaka sasa Tanesco wanatekeleza mikakati ya kuhakikisha wanajiendesha kwa faida, ili kupunguza mzigo kwa Serikali. Moja ya mikakati hiyo ilikuwa kuongeza bei ya umeme,” alisema Mbise.
Mapema Januari mwaka huu, Tanesco ilipandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 ambapo uniti moja ya umeme kwa wateja wanaotumia chini ya uniti 75 kwa mwezi, kutoka Sh60 hadi Sh100.
Kwa watumiaji wakubwa wa nyumbani, bei ya umeme ilipanda kutoka Sh221 kwa uniti hadi Sh306. Rungu hilo pia liliwakumba watumiaji wakubwa wanaopimwa kwa uniti 7,500 kwa mwezi ambapo bei ilipanda kwa Sh73 hadi kufikia Sh205.
Alipoulizwa ni mikakati gani imechukuliwa kudhibiti rushwa katika zabuni mbalimbali, Mbise alisema Serikali imekaza uzi katika usimamizi wa sheria za ugavi, pamoja na utendaji wa kila mtumishi.
Waliong’oka
Mwaka 2008, sekta hiyo ndiyo iliyowang’oa Waziri Mkuu, mawaziri watatu na katibu mkuu ikiwa ni sehemu ya kuwajibika baada ya kushindwa kusimamia taasisi zao kwa ufanisi.
Mawaziri hao wakiongozwa na Lowassa walichukua hatua hiyo kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza sakata hilo, iliyoongozwa na Waziri wa Uchukuzi wa sasa Dk. Harrison Mwakyembe, kubainisha kuwa Richmond ilikosa weledi na sifa za kupewa zabuni ya kuzalisha umeme nchini.
Mwananchi

No comments: