ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 6, 2014

Uvuvi haramu sasa wachochea saratani

  Dawa za kuua wadudu kwenye mimea zatumika
  Ni aina ya thionex 35 EC, ikiingia mwilini haitoki
Wakazi wanaoishi katika vijiji vilivyopo wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wanakabiliwa na hatari ya kuugua saratani kutokana na kula samaki wanaovuliwa kwa kutumia dawa aina ya thionex 35 EC.

Dawa hiyo inayotumika kuua wadudu kwenye mimea, imegeuzwa matumizi yake na sasa  wavuvi wa eneo hilo wamebainika kuielekeza katika kuvulia samaki hasa kwenye mito midogo inayounganika kwenye bonde la mto Kilombero.

Wataalamu wa mifugo, wameeleza kuwa dawa hiyo ina sumu na kwamba ikiingia mwilini mwa binadamu haitoki.

Badala yake inajikusanya kwenye ini kwa kadri samaki wanaovuliwa kwa kutumia dawa hiyo wanavyoliwa na hatimaye ni kuugua saratani.

Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Kilombero, Dk. Kitambi Jullu, anasema dawa hiyo inapotumiwa tofauti na ilivyokusudiwa, ikiwamo kuvulia samaki, ndipo inapohatarisha afya ya binadamu.

Alisema inapotumika sumu hiyo kuulia samaki inasababisha madhara kwa binadamu kwani sumu hiyo huenda kujikusanya katika eneo moja lisilokuwa na usumbufu katika mwili wa binadamu.

 Dk. Jullu, alisema madhara ya sumu inayotokana na thionex 35 EC hayajitokezi haraka, badala yake inachukua muda mrefu na kadri mtu anapokula samaki waliovuliwa kwa kutumia dawa hiyo.


Alisema kiafya sumu hiyo siyo nzuri kwa kuwa madhara yake hayaonekani kwa haraka kama ilivyo kwa magonjwa mengine.

“Madhara yanaweza kujitokeza baada ya mwaka mmoja au miwili na kwa wengine hata miezi mitatu yanatokea, inategemea kinga ya mwili wa mtu ilivyo,” alisema Dk. Jullu
Dk Jullu, alisema samaki wa aina hiyo wanapotumiwa na mjamzito, wanaweza kumuathiri mtoto aliyepo tumboni na mwanamke mwenyewe.

Kwa mujibu wa Dk. Jullu, miongoni mwa athari kwa mjamzito anayekula samaki waliovuliwa kwa kutumia dawa hiyo ni mimba kuharibika.

Baadhi ya wavuvi, wakazi wa vijiji vya Mngeta pamoja na Chita panapotajwa kuwa maarufu kwa uvuvi wa kutumia dawa hiyo, wanasema matumizi hayo yanasababisha kupatikana kwa samaki wengi.

Mmoja wa wavuvi hao, Moses  Charles, anasema matumizi ya thionex 35 EC yanafanyika kwa kuihifadhi ndani ya kopo lenye matundu madogo, kisha (kopo hilo) kutegeshwa mahali wanapopatikana samaki.

Mchakato huo unatajwa kufanyika kwa muda usiozidi dakika 20 ambapo samaki wanalewa, kufa na kuelea juu ya maji ambapo wanavuliwa kwa urahisi.

Hata hivyo, kutokana na ukali wa sumu inayotoka kwenye dawa hiyo, samaki hao wanaoza muda mfupi baada ya kuvuliwa hivyo kulazimika kuchemshwa, kuokwa ama kuchomwa ili.

Pamoja na kusudio la kuwapata samaki hao, miongoni mwa wanaolewa wanachukuliwa na maji kwenda eneo jingine la mto hivyo kutovuliwa na wavuvi.

Hata hivyo, anasema yeye na wenzake wanatambua kwamba samaki hao wana madhara madogo ikiwa ni pamoja na kuharisha na kwamba wanategemea na kutumia dawa za miti shamba kujitibu.

Mvuvi mwingine, Boniface Mgeta, anasema ni rahisi kumtambua samaki aliyevuliwa kwa kutumia dawa hiyo. Anazitaja baadhi ya viashiria vya samaki wa aina hiyo kuwa kulegea, kubadilika rangi ya asili na kuoza muda mfupi baada ya kuvuliwa.

Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti kwa samaki aliyevuliwa kwa kutumia dawa hiyo kasha akakaushwa ama kuchomwa. Soko kubwa la samaki hao lipo kwenye vijiji vya jirani na maeneo ya Mkamba na Kilombero.

Mfanyabiashara wa samaki kwenye kijiji cha Mngeta, Samson Limbala, alisema kutokana na uzoefu wake katika biashara hiyo, amekuwa akiwatambua na kuepuka kununua samaki wanaovuliwa kwa kutumia dawa hiyo.

 Alisema, uvuvi huo unapaswa kushughulikiwa kwa vile unachangia, pamoja na mambo mengine, kutoweka kwa samaki kwenye mto huo.

Limbala alisema awali wakazi wa kijiji hicho walitegemea biashara ya samaki, lakini kutokana na aina hiyo ya uvuvi ulio haramu, imewalazimu kutafuta shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.

Naye muuza duka la dawa za mifugo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa dawa hiyo inauzwa Shilingi 15,000 kwa kipimo cha nusu lita.

Alisema, mauzo ya dawa hiyo yanalenga itumike kwa kuulia wadudu kwenye mimea, lakini watu wenye nia ovu wanaitumia kuvulia samaki.

Afisa Uvuvi wa Tarafa ya Mngeta, Elukaga Kandongere, alisema ufinyu wa bajeti unasababisha kutofanyika kwa doria zenye lengo la kuudhibiti uvuvi huo.

NIPASHE ilizungumza na mmoja aliyepata madhara baada ya kutumia samaki hao, Awadhi Ally, ambaye alieleza siku chache baada ya kula (samaki) aliharisha na kutapika.
 Alipogundua kuwa chanzo cha kadhia hiyo ni kula samaki aliyevuliwa kwa njia haramu, alitumia dawa ya miti shamba, akapona.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi msaidizi wa wilaya ya Kilombero, Masanja Joram, uvuvi huo umeibua changamoto nyingi huku ukisababisha kutoweka kwa baadhi ya samaki.

 Alisema hana takwimu ya uhakika kutokana na upungufu wa samaki hao kwani eneo la bonde Kilombero kijeografia ni ngumu kufikia katika maeneo ya kambi zote za uvuvi.

Joram alisema kwa kipindi cha mwaka 2012, walifungua kesi 15 dhidi ya wanaojihusisha na uvuvi haramu na kwa mwaka jana zilikuwa kesi tano.

Alivitaja  vijiji ambavyo vinajihusisha na uvuvi haramu kuwa ni kata ya Mlimba A, Chita, Mngeta, Chombe, Mofu, Idete, Rumemo, Ifakara, Kibaoni na Kiberege.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala, alisema kuna mikakati wanayoianzisha ikiwamo kuwashirikisha viongozi wa kata na vijiji, kwa kushirikiana na maafisa uvuvi katika kupambana na uvuvi haramu.

Alisema ugumu uliopo ni kwamba wanaojishughulisha na biashara hiyo wanafanya hivyo nyakati za usiku wa manane.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: