ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 15, 2014

Kitita cha Dola chakamatwa kikitoroshwa airport D`Salaam

  Ni Dola 230,554 sawa na milioni 380/-
  Vitisho vyaendeshwa kwa waliokamata
Watu wawili wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kutaka kutorosha nje ya nchi fedha za kigeni kiasi cha Dola za Marekani 230,554 (Sh. milioni 380) kwenda nje kinyume cha sheria huku ikidaiwa kuwapo kwa njama za kuficha tukio hilo lisijulikane kwa umma.

Watu hao (majina tunayo) walikamatwa Mei 9, mwaka huu saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Habari zinaeleza kuwa mmoja wa watuhumiwa hao alikuwa anasafiri kwa ndege ya Qatar kupitia Doha kwenda China, na alikutwa na kitita hicho kwenye ukaguzi wa pili kabla ya kuingia kwenye chumba cha kusubiri kupanda ndege.

Kwa mujibu kanuni za kudhibiti fedha chafu, mtu anaruhusiwa kusafiri na fedha zisizozidi Dola 10,000 tu na kama kiasi hicho kitazidi anatakiwa kuomba kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) utaratibu ambao inadaiwa kwamba watuhumiwa hao hawakuufuata.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege (RPC), Seleman Khamis, akizungumza na NIPASHE jana alithibitisha kukamatwa kwa watu hao wawili waliotaka kusafiri na kiasi cha fedha kinyume cha sheria.

Kamanda Khamsi ambaye hakuwa tayari kuwataja watuhumiwa hao kwa majina, alisema suala hilo kwa sasa linashughulikiwa na Kitengo cha Uhalifu wa Fedha (Financial Crime Unit).

Kamanda Khamis alipoulizwa fedha hizo zilizokamatwa ziko wapi, alisema majibu hayo yataweza kujibiwa na kitengo cha Financial Crime.

Hata hivyo, wakati RPC akitoa majibu hayo, taratibu za kisheria zinabainisha kuwa suala hilo linatakiwa kushughulikiwa na Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu (Tanzania Financial Intelligence Unit) na siyo Jeshi la Polisi.

Kitengo hicho kinaundwa na maofisa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, BoT na Jeshi la Polisi ambalo hata hivyo, lenyewe halipaswi kufanya kazi ya kupeleleza badala yake linatakiwa kufanya kazi ya kufungua kesi dhidi ya mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Fedha Chafu ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, mtu anayetaka kusafiri na zaidi ya dola 10,000, ni lazima apate kibali kutoka BoT lengo likiwa ni kudhibiti fedha, chafu, utakatishaji wa fedha na fedha za wizi.

Licha ya watuhumiwa wa makosa kama hayo kutoruhusiwa kupata dhamana, lakini inadaiwa kuwa baada ya kukamatwa waliachiwa na hakuna jitihada zozote zinazofanywa na Jeshi hilo kuhakikisha kwamba wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi na baadaye kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu JNIA na ndani ya Jeshi la Polisi, mmoja wa watuhumiwa hao alipohojiwa na maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) alieleza kuwa alipata fedha hizo kutoka kampuni moja ya jijini Dar es salaam (jina tunalihifadhi) ili zipelekwe kwa kigogo mmoja aliyoko China.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa alikwenda JNIA kumkabidhi mwenzake kitita hicho, kisha kuvinjari uwanjani hapo kusubiria mwenzake aondoke.

Habari zinasema baada ya aliyepewa mzigo huo kukwama kwenye ukaguzi wa pili, alieleza kuwa mzigo haukuwa wa kwake na mwenyewe alikuwa maeneo ya uwanjani hapo, ndipo alipoitwa na kukiri kuwa ni wa kwake ambao alipewa na mabosi wake kutoka duka moja kubwa na maarufu jijini Dar es Salaam.

Kutokana na tukio hilo, jalada namba JNI/IR/107/204 la upelelezi limefunguliwa katika kituo kidogo cha polisi cha JNIA.

Hata hivyo, mmoja wa watuhumiwa hao aliruhusiwa kuendelea na safari yake.

Katika hali ya kushangaza, tangu kutokea kwa tukio hilo, hakuna mtu ambaye amejitokeza wazi kueleza kuwa ni mmiliki kitita hicho, na baadhi ya wafanyakazi wa TAA walioshiriki kubaini suala hilo wakianza kupewa vitisho.

Habari zinasema kuwa simu hizo zinapigwa zikionyesha kuwa kuna vigogo wa serikali ambao wako nyuma ya mpango huo ambao unaonekana kama mbinu ya kutaka kutakatisha fedha chafu.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Sioni sababu ya kuyaficha majina ya watu waliokamtwa na fedha hizo pia na hayo ambae kigogo anaehusika na wizi huo wa mali ya watanzania kama bado tunaendelea kuficha maovu hatutokuwa na maendeleo