ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 17, 2014

Mnyaa: Deni la taifa la trilioni 21/- haliwahusu Wazanzibari

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa amesema deni la Taifa la trilioni 21 ambalo kila Mtanzania amelibeba limekuwa likiathiri zaidi uchumi wa wananchi wa Zanzibar kutokana na faida ya upande wa Bara na kutaka serikali ieleze namna itakavyowafidia upande wa visiwani.

Mnyaa alisema hayo wakati akichangia katika kamati ya kupitia makadirio ya matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano iliyopitishwa juzi na Bunge hilo.

Alisema kuwa thamani ya Shilingi inaposhuka imekuwa ikiathiri uchumi wa Zanzibar kutokana na deni hilo wakati serikali ya Zanzibar haijihusishi na mikopo yoyote lakini wananchi wake wakilipa deni hilo kwa manufaa ya upande wa Bara.

Alisema ameshawahi kuuliza katika ofisi ya Wizara ya Fedha lakini alichojibiwa kuhusu suala hilo ni kuwa Zanzibar imekuwa ikikopa na zinalipwa na Jamhuri ya Muungano na kudai kuwa ni sawa Zanzibar imekuwa ikifanyiwa hisani na hawana haki.

Akizungumzia kuhusu fedha zinazopelekwa Zanzibar kutokana na kodi ambapo mwaka huu bilioni 44.05 na mwaka jana bilioni 44.784 zimekuwa hazitolewi ufafanuzi wa fedha hizo pamoja na matumizi yake.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, alisema Zanzibar imekuwa ikichukua mikopo kutokana na miradi mbalimbali pamoja na ile inayotekelezwa katika Jamhuri ya Muungano lakini inatambulika iliyokopa ni Jamhuri ya Muungano na ndiyo inayolipa.

Naye Waziri wa Muungano, Samia Hassan Suluhu, alisema kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya fedha wanaandaa semina maalum kwa wabunge wote ili kuelezea mapato na mgawanyo wake wote.
CHANZO: NIPASHE

No comments: