ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 17, 2014

HOMA YA DENGUE: Mabasi 600 kupuliziwa dawa

Ni yale yaendayo mikoani Yatakayopuuza kukiona
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuhakikisha mabasi yote 600 yanayofanya safari zake mikoani yanapulizia dawa ya kuondoa mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa dengue.

Manispaa za Dar es Salaam zimetengewa Sh. milioni 218 kwa ajili ya kununua dawa na vifaa vya kupulizia mazalia ya mbu hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki alisema kuwa tayari serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ili usienee kwa wengine. Alisema mabasi yatakayokaidi agizo hilo yatafungiwa safari zake lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha ugonjwa huo hausambai katika mikoa mingine.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki alisema kuwa tayari serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ili usienee kwa wengine.

Alisema mabasi yote yanatakiwa kuhakikisha yanapulizia dawa ili yanapoanza safari zake ili yasiondoke na mbu hao katika mikoa mengine.

Alisema kuwa homa ya dengue ilianza rasmi Januari mwaka huu katika hospitali ya Mwananyamala Wilayani Kinondoni na hadi jana jumla ya watu 494 walipimwa na kugundulika na vimelea vya ugonjwa huo.

Sadiki alisema kwa Manispaa ya Kinondoni wapo wagonjwa 389, Ilala 73 na Temeke wapo 32 ambao wametoka katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

“Wagonjwa waliolazwa wapo 11 hadi sasa ambapo katika hospitali ya rufaa ya Temeke wapo wagonjwa sita, Amana wanne, Burhani mmoja na kwa upande wa vifo vipo vitatu akiwamo daktari bingwa wa masuala ya ugonjwa wa akili,” alisema Sadiki.

Alisema sababu iliyofanya Wilaya ya Kinondoni kuwa na idadi kubwa ya ugonjwa huo ni kuwapo kwa kituo cha Taasisi ya afya ya Ifakara kujitolea kupima watu mara kwa mara. Sadiki alisema kwa Manispaa mbili zilizobakia hazikuwa na vituo kwa ajili ya upimaji wa ugonjwa huo ikilinganishwa na Manispaa ya Kinondoni.

Aidha, alisema uongozi wa mkoa umechukua hatua mbalimbali katika kudhibiti ugonjwa huo ikiwamo kuelimisha jamii dalili za ugonjwa, njia za kujikinga na maambukizi pamoja na hatua za kuchukua pindi mtu atakapoona dalili za ugonjwa huo.

Pia alisema wametoa matangazo katika kata mbalimbali pamoja na vipindi vya kuelimisha jamii katika vyombo vya habari. Alisema tayari wametoa mafunzo kwa maafisa wa afya 219 waliopo katika manispaa zote za jijini ili wawe na uelewa dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwa ugonjwa huo ni mpya nchini.

Sadiki alisema zoezi la kuweka viuadudu kwenye maji yaliyotuama ili kuua mazalia ya mbu hasa kata zenye wagonjwa wengi wameendelea na hadi sasa jumla ya lita 90 za dawa zimenyunyuziwa kwenye madimbwi yaliyoko maeneo mbalimbali.

Aidha, alisema kuna barua zimeandikwa kwa wakuu wa shule na wamiliki wa shule binafsi zikiwataka kusafisha mazingira yao na kupulizia dawa za kuua mbu.

Hata hivyo, Sadiki amewataka wananchi kusafisha mazingira yao ili kuondoa mazalia ya mbu, kusafisha mitaro, utupaji taka ni marufuku, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa nguo zinazofunika sehemu za mwili na kufunika maji.

Pia aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni waondoke katika maeneo hayo kwani ni hatari zaidi kwa mazalia ya mbu. Dalili za ugonjwa huo ni homa kali, kuumwa kichwa, misuli na viungo, kichefuchefu na kutapika. Serikali imetenga Sh. milioni 500 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

Wakati huo huo, wagonjwa wa dengue waliolazwa katika hospitali ya Tumbi mkoani Pwani wamefikia wawili. Afisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gerald Chami alisema mgonjwa wa kwanza anayetokea Mbezi Dar es Salaam alikuwa na dalili za maradhi hayo ikiwamo kutoka damu puani na masikioni akiwa na homa kali.

Mgonjwa mwingine alipokelewa kutoka Kibaha kwa Matiasi akiwa na dalili hizo hizo na madaktari wanaendelea kumuhudumia. Aliongeza Chami. Alisema wagonjwa hao wametengewa chumba maalumu ambacho muda wote kinapigwa dawa ya kuzuia mbu pia kina vyandarua vya kuzuia mbu.

*Beatrice Shayo, Dar na Margaret Malisa, Pwani
CHANZO: NIPASHE

No comments: