Dar es Salaam. Serikali imetenga zaidi ya Sh700 milioni kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue ambayo imeendelea kushika kasi huku wengine wakipoteza maisha.
Tangu kuanza kwa ugonjwa huo Januari mwaka huu hadi kufikia juzi jumla ya wananchi 494 wa mkoani hapa walipimwa na kugundulika kuwa na vimelea vya homa hiyo, kati yao akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili nchini, Gilbert Buberwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu fungu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema mkoa ni hapa halmashauri imetenga jumla ya Sh218 milioni zinazotumika kwa sasa katika kupambana na ugonjwa huo.
“Fedha hizo zinatumika kwa sasa katika kutoa huduma mbalimbali za dharura kwa wananchi wa mkoa huu kutokana na homa hiyo wakati tukiendelea kutafuta vyanzo vingine ili kuongeza kasi ya mapambano haya,” alisema Sadiki.
Mkuu huyo alifafanua kuwa katika fedha hizo kila manispaa itatumia kiasi chake na Manispaa ya Temeke itatumia kiasi cha Sh24 milioni, Ilala Sh32 milioni na Kinondoni Sh150 milioni.
“Tayari manispaa hizo zimeanza kufanyia kazi fedha hizo kwa kuendesha shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo husika, ikiwamo elimu ya usafi ambayo ndiyo msingi wa kuepukana na ugonjwa huu,” alisema Sadiki na kuongeza pia watanunua vifaa vya kupimia wagonjwa (Test kits) vitakavyokuwa vinatumika katika hospitali za manispaa hizo.
Hata hivyo Sadiki alisema hatua hizo ni za mwanzo na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa dengue.
Akizungumzia Sh500 milioni zilizoahidiwa bungeni mapema wiki hii na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe, Sadiki alisema fedha hizo bado zinashughulikiwa na mfuko wa Hazina na pindi zitakapotoka basi zitaongeza nguvu katika mchakato wa kupambana na homa hiyo nchini.
Sadiki alisema mbali na hatua hiyo zoezi la kuweka viua vijidudu kwenye maji yaliyotuama ili kuwaangamiza viluilui wa mbu linaendelea, hadi sasa jumla ya kata 58 zinaendelea kuweka viuadudu na kuharibu mazalia ya mbu.
Mkuu huyo alisema kuwa zoezi la kunyunyiza dawa litafanywa nao kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwenye magari 600 yanayofanya safari zake kati ya Dar es salaam na mikoani.
“Bado tunaanda utaratibu huo ambao utaanza haraka iwezekanavyo kwa sababu kumekuwa na uvumi kuwa watu wanaotoka Dar es salaam ndiyo wanaosambaza ugonjwa huu na endapo tutabaini kuwa kuna gari linaloenda mikoni bila ya kunyunyizia dawa basi tutafungia gari hilo kufanya safari,” alisema Sadiki.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment