ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 17, 2014

Serikali yashikwa pabaya bungeni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15, bungeni mjini Dodoma juzi. Viti vya wabunge wa Kambi ya Upinzani vikiwa wazi baada ya wabunge hao kususa na kutoka nje kutokana na kukasirishwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Federick Werema aliyoitoa bungeni. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma/Dar es Salaam. Kashfa ya zaidi ya Sh200 bilioni za Akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua sura mpya baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kudai kuwapo kwa watu wanaonunua mashahidi.
Jaji Werema alitoa kauli hiyo nzito bungeni mjini Dodoma juzi, kauli ambayo imeibua maswali mengi kuliko majibu, kuhusu ni nani wanaotoa fedha kutafuta mashahidi na kwa masilahi ya nani hasa.
“Ninafahamu kwamba kuna watu wengi wanatumia fedha kwa ajili ya kutafuta mashahidi, lakini haituhusu, palipo na haki, haki itasimama na haki ya mtu haipotei,” alisema Werema katika kauli inayoonyesha kukata tamaa.
Werema alitoa wito kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuendelea na uchunguzi na waufanye haraka na kwa umakini.
“Uamuzi uliofanyika hapa ni kwamba uchunguzi uendelee na vyombo vilivyoteuliwa ni Takukuru na CAG na bado vinafanya uchunguzi… Nahimiza vyombo hivyo vifanye kazi hiyo haraka na kwa umakini,” alisema.
Hata hivyo, Werema alitahadharisha kuwa ni vyema ikafahamika, akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa malengo maalumu. Akaunti hiyo ilifunguliwa na Kampuni ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Werema alikiri zipo kodi ikiwamo ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo ilipaswa kulipwa na Tanesco na kodi ya Manufaa (capital gain) inapaswa kulipwa na Kampuni iliyoiuza IPTL kwa Pan African Power Ltd (PAP).
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa fedha katika akaunti ya Escrow na kuzipeleka.
Waziri Mkuu alisema: “Kwa tuhuma zenyewe zilivyo itabidi tuwahusishe Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao ili kupata ukweli kwa sababu wako pia viongozi wa Serikali wanaotuhumiwa katika suala hilo, hivyo ni vyema likachunguzwa kwa uzito wake ili wale watakaobainika wamekula rushwa washtakiwe.
Kadhalika Waziri Mkuu aliliomba Bunge limruhusu CAG kukamilisha kazi hiyo.
Lema
Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, jana alihoji Serikali inatoa wapi nguvu na sauti ya kukemea rushwa katika taasisi zake wakati baadhi ya viongozi wanadaiwa kuhusika na kashfa ya IPTL.
“Kama wanaopaswa kukemea na kuzuia rushwa ni wala rushwa, ni wazi moja kwa moja kuwa utamaduni wa kupokea rushwa katika taasisi zote za Serikali ni jambo la kawaida na linaloipendeza Serikali ya CCM,” alisema.
Lema alitoa shutuma hizo wakati akisoma hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
Lema alienda mbali zaidi na kudai: “Hakuna kiongozi hata mmoja mwenye mamlaka ya kiuadilifu kukemea jambo hili kwa kuwa familia zao zinaishi, zinasoma na kufurahia maisha kwa ajili ya ufisadi”.
Alidai kuwa viongozi wa Serikali ndiyo vinara wa migogoro na uuzwaji wa dawa za kulevya nchini.
Shutuma nyingine ambayo Lema aliitoa ni kuhusu uchochezi wa masuala ya udini na ukabila katika taifa na kusema kwamba yanasababishwa na uzembe unaofanywa na viongozi wa Serikali ya CCM.
Mbunge huyo alisema kuwa baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa ndiyo vinara wanaofanya biashara ya dawa za kulevya, lakini bado hawajakamatwa wala kutajwa hadharani kama ambavyo serikali imekuwa ikiahidi mara zote.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina sababu za kupoteza muda katika eneo hili, kwani ni ukweli usiopingika kuwa biashara hii inafanywa na viongozi wakuu wa Serikali, hivyo basi waamue wao wenyewe kama wangependa kuendelea kuwa sehemu ya mateso na mauaji ya vijana wetu katika jamii ya watu inaowaongoza,” alisema Lema.
Alihalalisha kauli yake kuwa, katika nyakati tofauti, Rais Jakaya Kikwete alishatangaza hadharani kwamba anawajua kwa majina vigogo wanaojihusisha na dawa za kulevya, lakini inashangaza akiwa Amiri Jeshi Mkuu ameshindwa kuwataja kwa majina watu hao.
“Rais wa nchi ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama anaogopa kuwataja wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa majina ambao alisema anawajua, je, tushawishike kuwa watu hao ambao hata Rais aliwagwaya ni Malaika au ni Mungu?” Alihoji Lema.
Alisema kumekuwa na uzembe mkubwa ambao unafanywa na polisi kwa maelekezo ya viongozi wa CCM waliopo madarakani kiasi cha kuwaachia watuhumiwa hadharani kwa visingizio vya ajabu.
Kiongozi huyo alitolea mfano wa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa Chadema wa Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo ambaye alichinjwa na wauaji walikamatwa lakini wakatorokea mikononi mwa polisi.
“Wauaji wale walikamatwa na Polisi lakini cha kushangaza waliweza kutoroka mbele ya Polisi kwenye chumba cha mahakama wakiwa na pingu pamoja na kumpora askari bunduki.”
Mdee
Katika mchango wake bungeni, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimlipua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa kile alichodai kukumbatia majalada ya rushwa kubwa kwa masilahi yake binafsi.
Mdee alisema DPP amekuwa akilalamikiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kwamba amekuwa kikwazo katika kushughulikia kesi kubwa za rushwa.
“Juzi tunaambiwa hapa suala la akaunti ya Escrow, Sh200 milioni mnapeleka Takukuru na kwa CAG… Sheria ya mwaka 2007 iko wazi kwamba hairuhusiwi kuwataja wala rushwa wakubwa na mafisadi kwa majina,” alisema.
“Akitaka kufungua shauri la rushwa kubwa kubwa (Dk Hosea) mpaka akaombe kibali kwa DPP… Analalamika DPP amekuwa akibania vibali vya kufungua kesi kwa masilahi yake binafsi,” aliongeza kusema Mdee.
Hosea azungumza
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea alisema kuwa mashtaka hayo 404 ni ya mwaka wa fedha unaoishia Juni.
Alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi ipasavyo ndio maana walifanikiwa kuwasilisha kesi hizo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Eliezer Feleshi kwa ajili ya hatua zaidi.
Alipoulizwa kuwa ni kitu gani huchelewesha kazi zake, Hosea alisema kuwa hakuna kinachowachelewesha kwa kuwa kuna mgawanyo wa madaraka baina ya taasisi yake na DPP.
“Takukuru tunachunguza makosa ya rushwa na DPP anaandaa mashtaka. Hivyo tunafanya kazi zetu kama inavyotakiwa,” alibainisha Hosea.
Kuhusu majalada 103 yaliyorudishwa Takukuru kwa uchunguzi zaidi, Hosea alisema wanaendelea kuyafanyia kazi na kusisitiza kwamba hawezi kusita kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote ambao hati zao za mashtaka zitakuwa zimekamilika.
Kwa nyakati tofauti kumekuwa na tuhuma kuwa baadhi ya kesi za rushwa hupigwa danadana makusudi kwa kuwa zinahusisha vigogo.
DPP asema anasingiziwa
Hata hivyo, DPP Feleshi alisema kuwa mambo ambayo huzungumzwa ni nadharia na kwamba wanaotuhumu kuwa taasisi yake inawabeba vigogo hushindwa kutoa vithibitisho.
“Hao watu wanaosema kuwa nawabeba vigogo wataje hizo kesi ni zipi? Na kila siku wamekuwa wakisema hayo mambo lakini ukiwaambia waseme huwa wanatokomea, hakuna aliyewahi kutaja,” alisisitiza Feleshi na kuongeza:
“Mimi siwezi kuchelewesha makusudi majalada ya watu kwa sababu ni vigogo, hiyo si kazi yangu. Ufanisi wangu ni kuhakikisha majalada yote yanayoifikia ofisi yangu yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.”
Imeandikwa na Daniel Mjema, Habel Chidawali, Dodoma, Nuzulack Dausen, Dar es Salaam
Mwananchi

No comments: