Wednesday, May 14, 2014

Trafiki kutana na nguvu ya umma Dar

Kamanda mpinga
Polisi wa usalama barabarani mwenye namba E 6290 amekutana na nguvu ya umma baada ya kutaka kukamata gari na kushusha abiria kinyume cha sheria.

Trafiki huyo aliyekuwa kwenye barabara ya Morogoro-Dar es Salaam, alikumbana na kibano hicho jana asubuhi na kulazimika kuwa mpole.

Mwandishi wa habari hizi alikuwa abiria wa basi hilo Coster namba T405 BVV linalosafiri kati ya Msata mkoani Pwani na Mbezi, Dar es Salaam na kushuhudia mkasa huo.

Polisi huyo alikamata basi hilo Kimara Baruti wakati likielekea Ubungo na kumwambia dereva ashushe abiria aende kituoni kwa kukiuka masharti ya leseni.


“Twende kituoni ukalipe faini au nikupeleke Sumatra kwani leseni inataka uishie Mbezi na si Ubungo,” alisema.

Abiria walimzomea na kumfokea kuwa kama anataka kitu kidogo hatapewa na hawatashuka kwani kushusha wasafiri ni kinyume cha sheria inayoelekeza wafikishwe mwisho wa safari.

“Acheni kusumbua, mmezoa kuomba.

Una kitambulisho au na wewe ni feki…acheni kula ndiyo maana njaa haziishi,” zilisikika sauti mbalimbali zikimfokea.

Abiria walikuwa wakali na kumshushua askari huyo wakimtaka akamate magari yote yanayotoka mkoa wa Pwani yanayoingia Ubungo kupitia barabara ya Morogoro kwani leseni zake huishia Mbezi.

Walimzonga na kumwambia mabasi yanaruhusiwa kufika Ubungo na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetoa idhini hadi miundombinu ya stendi mpya itakapokamilika.

Trafiki huyo aliingia ndani ya basi hilo na kuendelea kuwabana kondakta na dereva hata baada ya abiria kushuka Ubungo.

Ofisa Mfawidhi Sumatra, Conrad Shio, alisema mamlaka imeruhusu magari yenye leseni ya kusafirisha abiria hadi Mbezi iwafikishe Ubungo.

Alieleza kuwa mabasi yanayotoka maneo ya Msata, Kongowe, Mkata, Kongowe, Miono hadi Mbezi Mwisho yanafikisha abiria Ubungo hadi kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na nchi jirani kitakapokamilika eneo la Mbezi Luis.

Alisema kwa upande wa Bagamoyo yalitakiwa kuishia Tegeta Nyuku, lakini nayo yanafika hadi Mwenye hadi kituo kitakapojengwa.

Alisema trafiki na makamanda wa usalama barabarani wa mikoa wanafahamu na kushangaa kwanini askari huyo alikamata basi hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: