BABU aliyefunga ndoa mwaka 2011 akiwa na umri wa miaka 94, Mathias Kisokota mkazi wa Kitongoji cha Isunta, Namanyere wilayani Nkasi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 97, amehamia na mkewe katika Mji wa Mpulungu mwambao wa Ziwa Tanganyika nchi jirani ya Zambia miezi sita iliyopita kwa lengo la kufanya tambiko la kumwezesha mkewe mwenye umri wa miaka 83 kupata mtoto wa uzeeni.
Mke
wa mzee huyo, Uria Mwamanzi ni mwenyeji wa nchi jirani ya Zambia
alizaliwa na kukulia katika Mji wa Mpulungu mwambao mwa Ziwa Tanganyika
ambapo kwa mujibu wa wajukuu zao ndiko babu yao alipokutana naye na kuwa
na mahusiano hadi walipofunga ndoa miaka mitatu iliyopita.
Wanandoa
hao ambao waliacha gumzo kubwa baada ya kufunga pingu za maisha katika
Kanisa Katoliki la Mtakatifu Anthony, alasiri ya Juni 18, 2011 mjini
Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi.
Akizungumza
na mwandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka katika Mji wa Namanyere
jana, Salvatory Adolf (19), mjukuu wa wazee hao kutoka kwa mtoto wao
kitindamimba mwenye umri wa miaka 40 sasa, alisema babu yake
amemsindikiza mkewe huyo ili kwenda kutambikia mizimu ya kwao.
“Bibi
hakuwa na raha mara kwa mara alikuwa akitamani kurudi nchini kwao
Zambia kuwasalimia nduguze pia akiwa huku alikuwa akiugua mara kwa mara
hivyo babu aliona bora amsindikize bibi akatambike kwa mizimu ya babu
zake nchini humo,” alisema.
Hata
hivyo, hakutaka kueleza kwa undani juu ya kiu ya babu yake ya kutaka
kupata mtoto, habari ambazo zinazungumzwa na watu wa karibu waliopo
ndani ya familia ya wanandoa hao.
Miongoni
mwao, Agnes ambaye ni mtoto wa mwisho wa Mzee Kisokota akizungumza na
mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka mjini Namanyere, Nkasi
alisema baba yake amekuwa na hamu hadi sasa ya kupata mtoto katika ndoa
yake changa. “Anasali sana akiomba kila siku apate mtoto katika ndoa yake.
"Bado
ana matumaini makubwa ….. nikianza kukusimulia tutakesha, tena anasema
siku akijaliwa mtoto katika ndoa yake hiyo atajawa na furaha kubwa na
kufanya sherehe ya aina yake… amemsindikiza bibi (mkewe) Zambia
kusalimia ndugu zake pia kutambika kwa kuwa baba ana hamu ya mtoto
atatumia fursa hii nae kutambikia kwa wakwe zake ili mkewe huyo ashike
mimba,“ alieleza Agnes.
Hali
hiyo inakuja licha ya ukweli kwamba, umri wa mke wa Mzee Kisokoto kuzaa
umeshapitiliza, lakini kwa pamoja wamedaiwa kuamini kwa Mungu hakuna
kisichowezekana hivyo anaweza kutenda miujiza kwa kuwapa baraka ya mtoto
wa ndoa yao ya uzeeni.
Mjukuu
huyo alipoulizwa juu ya ziara hiyo kuhusisha pia kusaka mtoto kutoka
kwa `mizimu’ ya ukoo wa mke wa babu yake, hakuwa na majibu ya moja kwa
moja.
“Bibi
alipoondoka alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mwili lakini tangu
atambike nchini Zambia inadaiwa amepona kabisa na sasa wanaishi raha
mustarehe na babu… ila watarudi huku kwetu baadae mwaka huu …”, alisema.
Katika
safari ya wazee hao, Adolf anasema bibi na babu yake walisindikizwa na
Claudio Mathias (21), kaka wa mjukuu huyo na kwamba kaka huyo
amesharejea nchini.
Wanandoa
hao kwa mujibu wa wajukuu zao kabla ya kufunga ndoa katika Kanisa
Katoliki Jimbo la Sumbawanga mjini Namanyere miaka mitatu iliyopita
walikuwa wakiishi ‘kinyumba’ kila mmoja wao akibahatika kuwa na watoto
katika mahusiano yake ya awali.
Kwa
pamoja wana wajukuu zaidi ya 30 na vitukuu zaidi ya 40 wengi wao
wakiishi nchi jirani ya Zambia. Mzee Kisokoto alifiwa na mke wa kwanza
zaidi ya miaka 39 iliyopita.
No comments:
Post a Comment