Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu
wa kivita,ICC imesema kuwa imepata ushahidi wa kutosha kumfungulia
mashitaka mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Demokrasia ya
Congo Bosco
Ntaganda.Ntaganda anashutumiwa kwa makosa ya Ubakaji, mauaji na hata kuwasajili watoto wadogo kama wapiganaji wakati wa vita vya mashariki mwa DRC.
Mahakama hiyo ilipokea ushahidi wa zaidi ya nyaraka elfu sitini na tisa kwa hivyo mwendesha mashtaka ameezelea imani kuwa anayo kesi ya kutosha kumfungisha Ntaganda.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Bwana Ntaganda alijisalimisha mwenyewe kwa ubalizo wa Marekani Mjini Kigali ambao ulimpokea na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC mjini The Hague.
Licha ya kuwa wanadai kupata ushahidi wa kutosha, Mahakama hiyo sasa itakabiliwa na kibarua kigumu kubainisha kuhusika moja kwa moja kwa bwana Ntaganda katika makosa wanayomshitaki nayo.
Mawakili wanasema kuwa mauaji ya Uvira, mashariki mwa DRC yalilenga makabila ya Lendu, Bira na Nande.
Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema kuwa hatua ya kumfungulia mashitaka Bosco Ntaganda ni hatua muhimu katika kuwalipizia haki waathiriwa wa mauaji ya DRC.
Wamesema pia kuwa huu ni ujumbe kwa wababe wa kivita kuwa hatimaye watakabiliwa na sheria kwa uhalifu dhidi ya binadamu.
BBC
No comments:
Post a Comment