Mswagala alisema anajiuzulu kupinga kuwapo kwa waganga hao walioingia katika kijiji hicho wakijiita ‘lambalamba’ wanaofanyakazi ya kutambua na kuwatoa wanavijiji uchawi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mswagala alisema kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kuona viongozi wenzake wanashinikiza waganga hao wafanye kazi hiyo kijijini hapo wakati yeye hataki wawapo kwa vile wanachochea fujo na uvunjifu wa amani.
Mwenyekiti huyo alisema wananchi na baadhi ya viongozi ambao siyo waelewa wamekuwa wakishinikiza kufika waganga hao ambao wanapita kila nyumba kwa lengo la kutoa wachawi ambapo huo ni uchonganishi na uvunjifu wa amani kijijini hapo.
Alisema kuwa baada ya yeye kutoafikiana na ujio wa waganga hao, lakini baadhi ya viongozi na wananchi wakawa wanafurahia kuwapo kwao na kuwakaribisha kijijini, hakuona sababu ya kuendelea na uongozi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa baada ya malumbano hayo, aliamua kubwaga manyanga kwa kuwa hawezi kukiuka amri ya serikali iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ambaye amewapiga marufuku waganga hao.
Kwa upande wake, Mgalu akizungumzia suala hilo alisema amepiga marufuku waganga hao katika wilaya yake.
Alisema kuwa kuna viongozi wa siasa wanafiki wanawakaribisha waganga hao ili wapigiwe kura na wananchi na kwamba hatakubali kuona hali hiyo ikiendelea.
Mgalu alisema kuwa kiongozi yeyote akiwamo wa siasa, mwenyekiti wa kijiji na watendaji wa kata na vijiji ambao watabainika wamewakaribisha waganga hao watakamatwa na kupelekwa polisi na kuwaonya kuwa hataki kusikia anapigiwa simu ya kuomba radhi.
Aliwataka maafisa watendaji wote kuandika taarifa fupi kuonyesha wamejipanga vipi kukabiliana na waganga hao wa jadi ambao ni wavunjifu wa amani na kutaka zimfikie kabla ya tarehe 24 mwezi huu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment