Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
pamoja na kiongozi wa waasi Riek Machar wanatarajiwa kukutana Jumanne
katika juhudi za kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umekumba nchi hiyo kwa
miezi sita.
Mkutano wao uliotarajiwa kufanyika leo mjini
Addis Ababa ulitibuka baada yaviongozi waliotarajiwa kwenye mazungumzo hayo kukosa kufika.
Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya wawili hao bila shaka yatakuwa hatua nzuri kwa mchakato huo wa amani.
Mkutano huo wenyewe utakuwa wa kwanza kwa viongozi hao kukutana tangu kutia saini makubaliano ya amani tarehe 9 mwezi Mei na wa pili tangu mwezi Januari.
Waziri wa mawasiliano Michael Makuei, alisema katika taarifa yake kuwa serikali ina matumaini kwamba awamu hii ya mazungumzo itafaulu na kwamba amani itapatikana.
Wakati huohuo, shirika la Amnesty International limewasihi wapatanishi kutoruhusu msamaha kwa washukiwa wa uhalifu kujumuishwa kwenye mkataba wa amani, na pia kuwaadhibu wale watakaopatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita.
Umoja wa Mataifa umetuhumu pande zote kwenye mzozo huo kwa kutenda uhalifu wa kivita na kutoa wito kwao kuheshimu mkataba wa amani.
Mashirika ya misaada pia yanaonya dhidi ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu na tisho la ukame ikiwa vita vitaendelea.
No comments:
Post a Comment