ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 22, 2014

Biashara ya damu ya binadamu yaibuka

Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi

Uuzaji wa damu ya binadamu kwa nia ya kujipatia kipato umeshika kasi nchini na baadhi ya hospitali imethibitika kuwa biashara hiyo inawapatia kipato watu wanaofanya shughuli ndani ya hospitali hizo au jirani nazo.

Uchunguzi wa NIPASHE umethibitisha biashara hiyo kushika kasi karibu na Hospitali Teule ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha ambako madereva teksi na wa bodaboda wamekuwa wakinufaika na uuzaji wa damu zao kwa ujira wa kati ya Sh. 40,000 hadi 80,000 kwa lita moja.

Wanaolazimika kununua damu hiyo ni ndugu na jamaa wa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo na kuhitajika kuongezewa damu lakini kwa kukosa ndugu wa karibu, hulazimika kununua damu hiyo kutoka kwa madereva hao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka hospitali hiyo, wana upungufu mkubwa wa damu na utaratibu unaotumika ili mgonjwa aongezewe damu ni lazima awe na watu wa kumchagia.

Mwandishi wa NIPASHE alifika katika hospitali hiyo na kujifanya kuwa ana shida ya kuchangiwa damu kwa ajili ya ndugu yake aliyelazwa hospitalini hapo, na kwa mshangao mkubwa walijitokeza madereva kadhaa waliokuwa tayari kuchangia damu lakini kwa malipo.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi, ambayo imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wa ajali za barabarani zinazotokea katika barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro, umebaini kwamba mgonjwa hawezi kupata huduma ya damu bila kuuziwa.

Mgonjwa anayepelekwa katika hospitali hiyo anapokuwa na mahitaji ya damu baadhi ya madaktari huwaeleza ndugu za mgonjwa kwamba aende kuonana na madereva wa teksi na pikipiki (bodaboda) ambao wapo nje ya uzio wa hospitali hiyo.

Imebainika kuwa ndugu wa mgonjwa wanapokwenda kwa madereva hao hukubali kutolewa damu kwa makubaliano ya kulipwa kati ya Sh. 40,000 hadi 80,000 kwa chupa moja yenye ujazo wa lita moja.

Makubaliano ya bei yanategemeana na muonekano wa mteja mwenyewe na akionekana kuwa na kipato kikubwa anatozwa hadi Sh.100,000.

Katika kupata uhakika wa jinsi damu inavyouzwa, gazeti hili liliweka kambi kwa muda wa siku nne kuanzia Julai 15 na 19 mwaka huu katika hospitali hiyo na kufanya mazungumzo ya kuuziwa damu na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo, madereva wa teksi na bodaboda.

Siku ya kwanza mwandishi alifanya mazungumzo na mlinzi wa hospitali hiyo aliyekuwa amevaa kitambulisho cha kazi jina linahifadhiwa.

Mazungumzo kati ya mlinzi huyo ambaye alikuwa akizuia ndugu na jamaa za wagonjwa kutoingia wodini kabla ya muda uliopagwa na uongozi wa hospitali hiyo yalikuwa kama hivi;

Mwandishi: Samahani nina ndugu yangu yupo hapa wodini amelazwa, lakini nimeambiwa na madaktari kwamba atafanyiwa upasuaji kwa hiyo nimeambiwa niandae damu. Bahati mbaya sina ndugu huku, naweza kupata wapi watu wa kunisaidia kutoa damu.

Mlinzi: Kwanza unataka damu ya group gani.

Mwandishi: Group 'O'. Mlinzi; watu wenye group hiyo ni wachache sana, lakini nenda kwa wale madereva wa teksi na bodaboda wenzako wenye wagonjwa wanakwenda kuongea nao wanawalipa fedha wanakubali kutolewa damu.

Mwandishi: Kwani malipo yenyewe yanakuwa kiasi gani, maana hali yangu kifedha siyo nzuri pesa nyingi nimemaliza kutibia mgonjwa.
Mlinzi: Inategemea wengine wanaanzia Sh.30,000 na kuendelea kutegemeana na utakavyokubaliana nao, ila kumpata mwenye group O ni kazi pale kwa dereva wa bodaboda alikuwepo mtu mmoja tu mwenye damu ya group 'O'.

Wakati mwandishi wa habari hizi akiendelea kuzungumza na mlinzi, alipita mfanyakazi mwingine wa hospitali hiyo jina tunahifadhi ambaye alikubali damu yake kutoa kwa malipo ya Sh. 60,000.

Mfanyakazi huyo alisema yupo tayari kutoa damu kwa Sh. 60,000 na kumtaka mwandishi aende katika ofisi za kitengo cha damu salama kilichopo katika hospitali hiyo kuwajulisha kwamba yeye ni ndugu yake anataka kutoa damu ili wasimkatalie kwa kuwa wanamfahamu.

Baada ya mazungumzo mfanyakazi huyo alitoa namba yake ya simu kwa mwandishi na kumwelekeza zilipo ofisi za Kitengo cha Damu Salama na kwamba atakapomaliza kuongea nao ampigie simu ili kazi hiyo likafanyike.

"Unajua tangu kumeletwa kitengo cha damu salama, kumekuwa na masharti sana tofauti na mwanzo, utaambiwa uende na watu wanne wakapimwe wote na kutolewa damu na utalazimika kuwalipa, lakini ukienda kuongea nao tutaenda na mimi tu watakubali na utanilipa Sh. 60,000," alisema.

Baadaye mwandishi alitoka nje ya uzio wa hospitali hiyo kwa ajili ya kuzungumza na madereva wa bodaboda na teksi kwa nyakati tofauti ambao walikubali kutoa damu kwa makubaliano ya kulipwa Sh. 40,000 na wengine Sh.50,000.

Dereva wa bodaboda jina tunahifadhi aliyekuwa na pikipiki yenye namba za usajili T 8.. C.. alikubali kutoa damu kwa malipo ya Sh. 40,000 ingawa alianzia bei Sh. 80,000 na baada ya mwandishi kuomba apunguziwe alikubali kwa Sh. 40,000 na kupewa kianzio (advance) Sh. 5,000.

Katika mazungumzo, dereva huyo alisema wamekuwa wakitoa damu kwa bei ya Sh. 80,000 hadi 100,000 kwa chupa na kwamba awali walikuwa wanatoza Sh. 40,000, lakini kutokana na ujio wa wafugaji wa kabila la Wamang’ati kwa kuwa wao wanapenda kazi ifanyike haraka ndio waliopandisha malipo hadi kufikia Sh.100,000.

Hata hivyo, dereva huyo alisema kutokana na kufanya kazi ya kutoa damu ambayo inawaingizia kipato kikubwa ukilinganisha na kazi ya kuendesha bodaboda, ujio wa Kitengo cha Damu Salama katika hospitali hiyo umepunguza idadi ya wananchi waliokuwa wakiwafuata kuomba damu kwa ajili ya ndugu zao waliolazwa katika Hospitali ya Tumbi.

"Ukiwa tayari utanipigia simu katika namba hii,….. ila kiutaratibu lazima utowe advance (kianzio)," alisema na kutoa namba yake ya simu kwa mwandishi baada ya kupewa kianzio cha Sh. 5,000 kwa makubaliano kuwa siku itakayofuata atakwenda kutoa damu.

Dereva mwingine wa bodaboda, pia jina linahifadhiwa ambaye namba yake ya simu aliyompatia mwandishi ilikuwa imesajiliwa kwa jina la kike, naye alikubali kutolewa damu kwa malipo ya Sh. 40,000.

Dereva huyo ambaye alikuwa na pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili T 6.. C.. kama ilivyo kwa mwenzake alipewa kianzio cha Sh.5,000 ili siku itakayofuata awe tayari kutoa damu.

Dereva wa teksi yenye namba za usajili, T 7.. B.. jina pia linahifadhiwa ingawa katika namba yake ya simu ya mkononi aliyompatia mwanadishi ilikuwa imesajiliwa kwa jina tofauti, mwandishi alimkodisha kutoka hospitalini hapo kwenda Maili Moja kwa malipo ya Sh. 3,000.

Mazungumzo yalianza ndani ya gari ambapo mwandishi alimweleza dereva huyo kwamba ana mgonjwa amelazwa Hospitali ya Tumbi na anatakiwa damu hivyo anapata tabu ya kupata watu wa kuweza kumsaidia kutoa damu.

Dereva huyo alisema mara nyingi madereva wa teksi ndio walikuwa wanasaidia watu kutoa damu kwa ajili ya ndugu zao, lakini hivi sasa wanaopigwa mkwara hasa baada ya ujio wa Kitengo cha Damu Salama.

Alisema hivi sasa madereva wa bodaboda ndio wanaotoa damu kwa makubaliano ya malipo ya fedha kwa sababu walio wengi wanaoegesha pikipiki zao katika hospitali hiyo bado hawajafahamika sana kama ilivyo kwa madereva wa teksi.

"Ngoja nikupe namba yangu ya simu halafu utanipigia nikupatie namba za simu za madereva wa bodaboda wanaoweza kukusaidia kutoa damu, lakini kwa sisi dereva teksi tunafahamika sana, zamani ilikuwa kazi rahisi," alisema.

WAGONJWA WANENA
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Tumbi, wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, walisema upatikanaji wa damu katika hospitali hiyo umekuwa tabu sana kwani kama ndugu yako hana pesa mgonjwa wake hawezi kupata huduma ya damu.

Juma Abubakar mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kutokana na ajali ya gari aliyoipata eneo la Mlandizi, alisema kutokana na ajali hiyo alielezwa na madktari kwamba anatakiwa aongezwe damu kwa kuwa hakuwa na ndugu alipata wakati mgumu sana.

“Baada ya kupata ajali niliambiwa kuwa niwatafute ndugu zangu wasaidie kutoa damu za kuniongezea, lakini nilipowaambia kuwa ndugu zangu wapo mbali niliambiwa nitoe Sh. 20,000 ili watafutwe watu wa kunitolea damu,”alisema.

Mgonjwa mwingine Rose John alisema kuna agenda ya siri iliyojificha kati ya wafanyakazi wa hospitali hiyo na madereva wa teksi na bodaboda kwani mgonjwa asiyekuwa na ndugu wa kumtolea damu kama inahitaji anaambiwa aende kwa madereva hao.

“Kimsingi ni kama madereva wa bodaboda na teksi wanakula dili moja na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali ya Tumbi.

KITENGO CHA DAMU SALAMA
Mratibu wa kitengo cha damu salama Pwani, Jacqueline Mkuchu, alisema suala la madereva wa bodaboda na teksi kuuza dawa bado halijaifikia ofisi yake na kwamba kama itabainika hivyo zipo hatua za kisheria za kuwachukulia wahusika.

“Bodaboda na teksi karibu wengi tunawafahamu, huwa tunawafukuza wakiletwa na mtu na hasa na Wamang’ati na tukiwauliza maswali kweli huyu ni ndugu yako kweli akijibu kwa kubabaisha tunamfukuza,”alisema.

Mkuchu alisema kitengo cha damu salama Pwani kazi yake kubwa ni kukusanya na kusambaza damu kwenye hospital nane zilizopo katika mkoa wa Pwani kulingana na mahitaji ya damu kwa kila hospitali.

Alizitaja hospitali zinazopata damu kutoka katika kitengo hicho kuwa ni Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi, Mkuranga, Bagamoyo, Kisarawe, Rufiji, Mchupwi, Mafia na Bulele.

Alisema mahitaji ya damu kwa hospitali hizo ni takribani chupa 930 (blood unit) kwa mwezi, wakati kituo kina uwezo wa kukusanya wastani wa chupa 500 kwa mwezi.

“Mahitaji ya damu ni makubwa sana ukilinganisha na kiwango tunachokipata, mwezi Mei tulikusanya chupa 517 na Juni 667, hivyo mgonjwa akihitaji damu mara nyingi tunawaambia ndugu zake waje watoe damu,” alisema.

Mkuchu alisema tabia ya baadhi ya watu kuuza damu tulishatoa tahadhari kwa wananchi na kwamba hivi sasa kinachofanyika ni kuhamasisha wananchi kuendelea kuchangia damu.

UONGOZI WA HOSPITALI WATUPIANA MPIRA KUJIBU
Kutokana na kashfa hii, gazeti hili liliwatafuta viongozi wa Hospitali Teule ya Rufaa Pwani-Tumbi ambayo ipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha, lakini kwa takribani siku tatu wasemaji wakuu wa hospitali hiyo wamekuwa wakitupiana mpira kujibu suala hilo.

Wa kwanza kutafutwa ni Msemaji Mkuu wa Hospitali, Jeradi Chami, ambaye kwa siku mbili simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita tu bila kupokewa na siku ya tatu alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu kuhusu nini mwandishi wa habari hizi anataka alijibu kama ifuatavyo;

Asante kwa kukufahamu, nenda kamuone Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha atakupa maelezo yote kwa kadri utakavyohitaji, siko ofisini wiki ya 2/3 sasa.

Gazeti hili lilipokwenda katika ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Katibu Muhtasi alisema yupo likizo na kwamba anayepaswa kutoa majibu ya suala hilo ni Katibu wa Hospitali.

Katibu wa hospitali ambaye hakutaka kutaja jina lake alipofuatwa ofisini kwake, alikataa kuongea chochote kuhusu suala hilo na badala yake alisema anayepaswa kutoa ufafanunuzi wa suala hilo ni msemaji wa hospitali bwana Chami.

Kutokana na viongozi hao kutupiana mpira, gazeti hili liliwasiliana kwa mara nyingine na msemaji wa hospitali ambaye alijibu hivi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi.

“Mwenye mamlaka ya mwisho kuzungumza chochote ni Mkurugenzi Mkuu. Huo ni utaratibu unaotakiwa kufuatwa kama ulivyo.

Unachotakiwa kuwa na subira vile vile hiyo siyo dharura hata kama kaimu hayupo unaweza omba appointment kuna shida gani.”

Mimi siko ofisini, natoaje taarifa wakati sipo kazini hata kama jibu lipo obvious (wazi). Niko kitandani naumwa….please understand (tafadhali elewa).

Baadaye gazeti hili lilifanya mawasiliano na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Peter Dattani, ambaye alipopigiwa simu hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu na kuulizwa swali alijibu hivi:

“Mpigie PRO (Msemaji wa Hospitali) jina lake ni Chami.”

Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi alimjibu kuwa Chami ndiye aliyetoa ushauri kwamba nikuulize wewe (Mkurugenzi) na kumtumia meseji za Chami.

Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ajilibu sms kwamba: “Ok. Nipo nje ya mkoa.”
CHANZO: NIPASHE

No comments: