Dar na Marekani. Wakati kukiwa na uthibitisho kwamba Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali alifariki dunia na kuzikwa miaka sita iliyopita, kitendawili kilichobaki ni sababu za ugonjwa na baadaye kifo chake.
Wanafamilia wote waliozungumza na mwandishi wa gazeti hili tangu uchunguzi huu ulipoanza Julai 2012, hakuna aliyekuwa tayari kueleza sababu za kifo chake na wote waliohojiwa wanasema anayefahamu matokeo ya vipimo vya madaktari ni mkewe, Mama Anna Muganda.
Wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kuwa na taarifa za sababu za kifo cha Gavana huyo kilichotokewa Mei 16, 2008 nyumbani kwake Washington DC ni mtalaka wake, Malva Ballali na watoto wake; Octavio Ballali na Rahel Ballali.
Kwa muda mrefu gazeti hili lilijitahidi kutumia njia mbalimbali kumtafuta Mama Muganda, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa na taarifa kutoka kwa ndugu zake wa karibu zinasema hayuko tayari kwa namna yoyote kuzungumzia suala hilo.
Kwa jinsi hali ilivyo siyo tu kwamba imekuwa vigumu kwa Mama Muganda kuzungumzia suala hilo, ila hata upatikanaji wake kwa kukutana naye ana kwa ana au kupata mawasiliano yake yawe ya baruapepe au namba za simu yalishindikana.
Wakati mwandishi wa gazeti hili alipokwenda Marekani, aliambiwa kwamba mwanamama huyo aliyekuwa mshauri wa kwanza wa masuala ya uchumi enzi za uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, alikuwa nchini Tanzania kumuuguza dada yake ambaye baadaye alifariki dunia na kuzikwa Mugumu, Serengeti mkoani Mara.
Baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka Mara, kati ya Julai 8 na juzi, gazeti hili lilimtafuta kupitia kwa ndugu zake, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba na baadaye liliambiwa kwamba ameondoka Julai 16 usiku kuelekea Marekani. Habari zinasema Mama Muganda akiwa mshauri wa Mkapa, ndiye aliyemshauri kiongozi huyo kumchukua Ballali kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kuongoza BoT.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu serikalini alisema kama Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa ilipata mafanikio yoyote kiuchumi, basi mafanikio hayo hayawezi kutenganishwa na Ballali na mkewe Mama Muganda waliokuwa washauri na watekelezaji wa maboresho ya sekta hiyo.
“Kinachozungumzwa leo hii ni tuhuma tu dhidi ya Ballali kwa sababu pengine hayupo, lakini ukweli ni kwamba kukua kwa uchumi wakati wa uongozi wa Mkapa kunatokana na ushauri wa yule mama (Muganda) na utekelezaji na usimamizi wa sera za kiuchumi uliofanywa na BoT chini ya Gavana ambaye ni Ballali,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Kutokana na hali hiyo, Mama Muganda amekuwa kimya kutokanana kile kinachoelezwa na ndugu zake kwamba ni ukimya wa viongozi wa Serikali wakati wa ugonjwa wa mumewe na kunyamazia tuhuma alizopewa Ballali wakati akiumwa na baada ya kifo chake.
Mtalaka na watoto
Hali ya kutotaka kwa namna yoyote kuzungumzia chanzo cha kifo cha Ballali, pia imeonekana kwa Malva ambaye ni mke wa kwanza wa Gavana huyo na mtoto wake, Octavio.
Kwa nyakati tofauti wakati gazeti hili likitafuta mawasiliano nao, walisema hawakuwa na cha kusema kwa hiyo wasingependa simu, wala baruapepe zao zitolewe kwa mwandishi wa Mwananchi.
Katika harakati za kutaka kuzungumza na familia hiyo, gazeti hili lilimtumia ujumbe Malva ambaye ni mzaliwa wa Argentina kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini hadi jana hakuwa amejibu ujumbe huo, licha ya kuwa anwani yake ilionekana kufanya kazi.
Baadhi ya ndugu walioko Tanzania kwa upande wao walisema hawafahamu chanzo cha kifo chake na kwamba taarifa walizopewa zilihusu ugonjwa na baadaye kifo.
“Kwamba kilichomuua ni nini, kwakweli sijawahi kufahamu pengine mke wake anafahamu, mimi sijawahi kuambiwa na hata ndugu zetu wengine hawajui kilichomuua,” alisema Margaret Mpango ambaye ni dada mdogo wa Ballali.
Kauli yake inafanana na ile ya Paschal Ballali ambaye pia ni mdogo wa marehemu ambaye alisema: “Kwa kweli hatujawahi kuambiwa kwamba tatizo lilikuwa nini, tulipewa taarifa kwamba anaumwa na mara amezidiwa na baadaye taarifa za kifo.”
Wiki iliyopita Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu alisema wakati akienda Marekani Agosti 2007, Ballali alikuwa mgonjwa, lakini akasisitiza kwamba wanaoweza kueleza tatizo lake ni familia.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue katika mazungumzo yake na gazeti hili wiki jana alisema Ballali alikuwa mgonjwa, lakini naye akasema familia yake pekee ndiyo inayoweza kutoa taarifa kuhusu ugonjwa wake.
Inaendelea kesho...
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment