Dar es Salaam/Misenyi. Mjadala wa urais mwaka 2015 unaonekana kuanza kuitikisa nchi kutokana na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kujitokeza hadharani na kutangaza nia, huku wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na vyama vya siasa wakitaja sifa za mgombea.
Mmoja wa vigogo hao wa CCM ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye jana alijitokeza na kusema atajitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais iwapo wataendelea kujitokeza wasiokuwa na sifa.
Akizungumza kwenye Mahafali ya Chuo cha Uuguzi cha Masista wa Kanisa Katoliki Kanosa Mugana, Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera jana, Sitta alisema wengi wa waliotangaza nia hawafai na kwamba wanapiga porojo tu.
Sitta alisema wengine wamejitokeza kwa ‘gia’ ya ajira, lakini hawabainishi chanzo chake, kwani tatizo hilo limetokana na ufisadi kwa baadhi ya viongozi.
Aliwataka wananchi kuwapima wagombea kwa makini kwani wapo baadhi yao wanajinadi kuwa wao ni vijana kitu ambacho siyo kigezo cha kuwa rais.
“Ndugu zangu Watanzania, tusipowachuja watu kwa chujio la tabia zao, tutaangukia mtego wa kuwapima watu kama vile tunafanya mzaha, maana kuna wengine wameanza kusema nichagueni mimi ni kijana, hivi kwani urais ni mashindano ya ulimbwende, tunatafuta mzuri?” alihoji.
Awaponda waliotangaza nia
Alisema akiangalia orodha ya waliojitokeza haifai na kwamba, labda watu kama wawili wanaoweza kuungwa mkono lakini hakuwataja.
Waziri Sitta alitumia hadhara hiyo kuihadharisha jamii kuona suala la uchaguzi wa rais kama jambo la kawaida, kwani ikicheza nchi itazama.
”Niseme jingine, kwa kuwa nikitazama hiyo anga ya hawa wanaotafuta ukubwa, nawaona kama mmoja wawili ndiyo kidogo unaweza kuwaunga mkono. Hali hii ikiendelea namna hii, eeh itabidi na sisi wazee tujitose manake ikiwa watu wenyewe hawa ni walaghai, wengine ni waongo, wengine rekodi mbaya, wengine walishiriki kuhujumu nchi, ndiyo wanakwenda kimbelembele wanapigana vikumbo.
Wasomi, wanaharakati
Wakati Sitta akisema hayo, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamesema rais ajaye anatakiwa kuwa mzalendo, msomi, mwadilifu, mchapakazi, anayejua matatizo ya nchi na wananchi na akubali kuyatatua, asiwe mbaguzi, mwenye uamuzi mgumu, anayetanguliza masilahi ya taifa mbele na atakayepambana na rushwa na ufisadi kwa vitendo.
Kauli za wadau hao zimekuja kipindi ambacho watu wa kada mbalimbali, hasa kutoka ndani CCM wakiweka wazi nia zao za kugombea urais mwaka 2015, kufikia hatua ya chama hicho kuwapa adhabu makada wake sita, kutokana na kuanza kampeni mapema.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Makamba takribani siku nane zilizopita akiwa jijini London, Uingereza, alitangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2015, akisema huu ni wakati wa fikra mpya ambazo zinahitaji vijana na kwamba wazee wakae kando.
Hata hivyo, Makamba alipingwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema kuwa naibu waziri huyo anataka mambo makubwa, kwamba, “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka. Alhamisi iliyopita Sumaye akiwa mkoani Mwanza alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, akisema kuwa ana nia ya kugombea urais, lakini mpaka atakapoombwa kufanya hivyo.
Januari mosi mwaka huu, licha ya kutokuweka wazi Lowassa alitangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Hata hivyo, makada hao huenda wakakumbwa na rungu jingine baada ya siku tatu zilizopita chama hicho kutoa maagizo kwa Kamati yake ya Usalama na Maadili kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa vigogo hao waliotangaza nia kabla ya wakati.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema nchi ilipofikia inahitaji rais mwadilifu atakayekuwa tayari kuchukua uamuzi mgumu bila woga kwa viongozi wote ambao hawatakuwa waadilifu.
“Umri siyo hoja wala taabu, tunataka rais anayethubutu kutenda haki na mwenye kuzingatia maadili, kuwaunganisha Watanzania wote, lakini aweze kuchukua hatua kwa wasio waadilifu hata kama ni ndugu, jamaa au rafiki yake.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Tolly Mbwete alisema, rais ajaye anatakiwa awe mwelewa wa kiasi kikubwa hasa katika masuala ya uchumi na mwenye muono wa Tanzania mpya alipoikuta na anakotaka kuifikisha.
Wanaharakati
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema nchi ilivyo sasa suala la umri isiwe sababu, kwani mtu yeyote anaweza kuwa rais.
Alisema rais ni lazima awe mtu mwenye upeo mkubwa wa kupokea mabadiliko yatakayojitokeza na kuyafanyia kazi.
“Ujana haunipi shida, lakini ana uwezo? Kuna vijana wako makini kutuongoza, hivyo tusiwanyime nafasi kwa umri wao. Tuangalie ni jinsi gani atatatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi,” alisema Dk Bisimba.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya alisema, “Kiongozi tunayemtaka awe anaelewa na awe na msimamo thabiti wa kuendeleza nchi bila kujali kuwa ni mwanamke, kijana, mwanaume au mzee.” Aliongeza; “Tunahitaji kumpata kiongozi atakayepambana na rushwa, uzembe na kipindi hiki mtu wa aina hii ndiyo tunayemtaka.”
Vyama vya Siasa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), John Heche alisema umri, jinsia na rangi haijawahi kuwa sifa ya urais hiyo ni kampeni ya kibaguzi.
Alisema rais anayehitajika ni yule anayejua matatizo ya wananchi, atakayeitoa nchi iliyo katika matumaini yaliyofifia kwenda mbele zaidi.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alitaja sifa nne za rais ajaye na kufafanua kuwa umri ni kigezo cha kibaguzi.
“Rais lazima awe mzalendo, mwenye maadili, anayejua matatizo ya nchi yake na Watanzania na awe na majibu yake na asimamie misingi ya utawala bora iliyoanza kupotea na kuhakikisha kuwa anapambana na rushwa na ufisadi,” alisema.
Viongozi wa dini
Wakizungumza na gazeti hili Askofu Furaha Mwambusye wa Kanisa la Haven of Peace, Ammy Mwakitalu wa Kanisa la TAG-Tabata, David Samson (Jesus Power-Musoma) na Boniphati Makasi (EAGT-Bunju) na Askofu Mkuu wa Kanisa la Power Miracle, Joachim Peter walitaja sifa nne za anayefaa kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter alitaja sifa ya kwanza kuwa ni kiongozi mwenye kumcha Mungu, ambaye hatakuwa tayari kufanya jambo bila kumshirikisha Mungu.
“Taifa letu halihitaji viongozi wenye tuhuma za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Peter.
Alisema sifa ya tatu ni kuwa na kiongozi ambaye hayupo katika vita, ugomvi na mapambano na viongozi wenzake.
“Ugomvi wa aina hii unaweza kuzaa visasi ambavyo hudumaza amani na maridhiano ya viongozi,” alifafanua.
Alisema sifa ya nne, kiongozi atakayeweza kukabiliana na changamoto mpya zinazolikabili taifa, likiwemo suala la elimu, umaskini na ajira.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Midlraj Ibrahim na Ibrahim Yamola.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment