ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 19, 2014

Hivi ndivyo Simba, Yanga zinavyoibiwa

  Wajanja wanufaika kwa mauzo ya jezi, klabu zenyewe njaa kali
Mteja akiangalia jezi kwa ajili ya kuinununua kwenye kituo cha mabasi cha Mbeya muda mfupi kabla ya mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara baina ya Tanzania Prisons na Simba Februari 9, 2014.

Wakati klabu kongwe za soka nchini Simba na Yanga zikihaha kupata fedha za kujiendesha hadi kufikia hatua ya kutembeza bakuli na kuwapigia magoti watu wanaoitwa wafadhili, wapo vigogo wenye uhusiano nazo wanaoneemeka kwa kuingiza mabilioni ya shilingi kwa uuzaji wa jezi na vifaa vingine vyenye nembo zake.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa miezi 11 tangu Septemba 2013 katika maeneo ya Mbeya, Tabora, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha, Tanga, Zanzibar na Dar es Salaam, umebaini wafanyabiashara wakubwa nchini, wakiwamo baadhi ya vigogo wa klabu hizo, huagiza nje ya nchi jezi na vifaa vingine vinavyotengenezwa vikiwa na nembo za Simba na Yanga kwa manufaa binafsi.

Wauzaji wa maduka ya jezi katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam wameiambia NIPASHE kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa nchini wakiwamo vigogo wa Simba na Yanga huwauzia kwa bei ya jumla jezi na vifaa vingine vya michezo vyenye nembo za klabu hizo.


"Sina uhakika kama viongozi wa Mbeya City, Ndanda FC na klabu nyingine ndogo ndogo za soka nchini wanashiriki kuingiza jezi za klabu zao kinyemela, lakini jezi za Simba na Yanga tumekuwa tukiletewa na wafanyabiashara ambao ninaamini kwa kiasi kikubwa wanajulikana kwa baadhi ya viongozi wa klabu hizi mbili," anasema mmoja wa wauzaji wa maduka hayo (jina linahifadhiwa).

MAPATO YA KLABU
Mapato ya kibiashara (commercial revenue) yanayohusisha mauzo ya jezi na vifaa vingine vyenye nembo ya klabu husika, mapato yatokanayo na haki za matangazo ya mechi (broadcasting revenue) na mapato ya milangoni (matchday revenue) ni njia kuu tatu zinazotumiwa na klabu za soka duniani kujiimarisha kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya rohlmann/pre-marketing.de iliyotolewa Januari 4, mwaka huu kuhusu hali ya uchumi wa klabu za soka duniani hadi Desemba 31 mwaka jana, klabu za Real Madrid, Barcelona na Manchester United zinakamata nafasi tatu za juu kwa kuingiza fedha nyingi kupitia mauzo ya jezi zenye nembo zake.

Wakati hali ya uchumi ni mbaya kwa timu za Tanzania, ripoti hiyo inabainisha kuwa klabu kubwa za soka barani Ulaya zimekuwa zikipata mabilioni ya shilingi kutokana na mikataba minono zinazoingia na kampuni zinazojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa vifaa vya michezo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Real Madrid inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), inaongoza duniani ikipata dola za Marekani milioni 49 (Sh. bilioni 78.4 za Tanzania) kila mwaka kutokana na mkataba wake na kampuni ya Adidas ulioanza 1998 na utafikia tamati 2020.

Real Madrid wanafuatwa na wapinzani wao wa jadi, klabu ya Barcelona, wanaolipwa dola za Marekani milioni 43 (Sh. bilioni 68.8) kwa mwaka katika ubia wao na kampuni ya Nike inayotengeneza jezi zao tangu 1998, mkataba utakaomalizika 2018.

Manchester United inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL), inaongoza Uingereza na inakamata nafasi ya tatu duniani kwa kuingiza dola za Marekani milioni 41 (Sh. bilioni 65.6) zinazotolewa kila mwaka na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike kutokana na ubia wao wa miaka 13 (2002-2015) wa utengenezaji na uuzaji wa jezi zao.

Manchester United wanafuatwa kwa karibu na wapinzani wao wa jadi, klabu ya Liverpool inayokamata nafasi ya nne duniani.

“Tangu 2012, Liverpool imekuwa ikipata dola za Marekani milioni 40 (Sh. bilioni 64) kwa mwaka kutoka kampuni ya Warrior inayotengeneza na kuuza jezi zao. Mkataba huo utamalizika mwakani (2015),” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

TP MAZEMBE
Katika kufuata nyayo za klabu nyingine kubwa duniani, klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefungua duka kubwa la kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya timu hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo, duka hilo lilifunguliwa mjini Lubumbashi, DRC Alhamisi Aprili 4, mwaka jana kwa ajili ya wapenzi wa klabu hiyo kununua bidhaa halisi za TP Mazembe.

Baadhi ya vifaa vinavyouzwa kwenye duka la klabu hiyo wanayocheza Watanzania Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ni jezi na kofia.

Klabu hiyo si kwamba inafanya vizuri kiuchumi tu, bali inang’ara pia uwanjani kwani Jumamosi Julai 26, mwaka huu mtandao wa footballdatabase.com ulitoa ripoti ya viwango vya ubora wa soka kwa klabu barani Afrika ikionesha TP Mazembe inakamata nafasi ya kwanza ikifuatwa na Al-Merreikh ya Sudan, Esperance de Tunis ya Tunisia na Raja Casablanca ya Morocco.

SIMBA, YANGA
Wakati timu za Ulaya na TP Mazembe zikitakata kwa mabilioni ya shilingi kutokana na mauzo ya jezi, klabu za Tanzania zimekuwa zikitegemea mapato ya mlangoni (gate collection) na kutembeza bakuli kuomba misaada ili ziendeshe shughuli zake huku mauzo ya jezi na vifaa vingine vyenye nembo ya klabu husika yakihujumiwa.

Kwa muda mrefu Simba na Yanga zimekuwa zikilalamika hujuma dhidi ya jezi na vifaa vingine vinavyotengenezwa na baadhi ya wafanyabiashara wakitumia nembo zao na kuviuza bila makubaliano yoyote.

Katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Mbeya Machi 10, mwaka huu, Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuna mtandao wa watu wanaotengeneza jezi na vifaa vingine vyenye nembo ya Simba bila klabu hiyo kunufaika na pesa inayopatikana kupitia mauzo ya vifaa hivyo.

Kamwaga alisema mtandao huo unahusisha wafanyabiashara wakubwa nchini ambao huagiza nje ya nchi jezi na vifaa vingine vyenye nembo ya klabu hiyo.

"Tumeanza mapambano dhidi yao, lakini vita hii ni ngumu kumalizwa na Simba peke yake, tunaomba serikali itusaidie kuzuia uingizaji wa jezi na vifaa vyenye nembo za klabu yetu na klabu nyingine zinazohujumiwa nchini," alisema Kamwaga.

Aidha, Septemba 5, 2013 Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini, Khamis Kilomoni ilitangaza kuanza rasmi kupigania haki za klabu kwa kuwakamata wafanyabiashara wanaonufaika na mauzo ya jezi na vifaa mbalimbali vyenye nembo ya klabu hiyo bila maafikiano maalum ya kibiashara baina yao na klabu.

Kilomoni alienda mbali zaidi kwa kusema wale wote watakaokiuka agizo hilo watakumbana na rungu la dola kwani klabu hiyo inashirikiana na Jeshi la Polisi na Tume ya Ushindani.

Wakati Kilomoni akitoa tamko hilo, alisema tayari bidhaa kadhaa zilikuwa zimekamatwa, ikiwa ni pamoja na jezi (fulana) 1,261, kaptula 31, ribbon 228, bendera 189 na vifaa tofauti vya urembo 1,248.

"Wajisalimishe. Waje tuzungumze na kuwatambua kisheria ili wao wapate na klabu ifaidike," alisema Kilomoni.

Lakini, licha ya kutolewa kwa tamko hilo, jezi, khanga, kalenda, picha, vitambaa vya kufutia jasho, stika za kwenye magari, bangili, vuvuzela, miavuli na hata skafu zenye nembo ya Simba zinaendelea kuuzwa nchini kiholela kila uchao.

Kamwaga alisema kuwa mwaka jana alijitokeza mfanyabiashara ambaye aliomba kutengeneza na kuuza jezi zenye nembo ya Simba akiahidi kuwapatia Sh. milioni 70 kila mwaka, lakini ubia huo ulishindikana kutokana na masharti magumu aliyowapa.

"Alitaka uongozi wa Simba ukamate jezi feki zote zinazouzwa mitaani na kuhakikisha hakuna jezi feki inayoingia nchini wakati akiuza jezi halali za klabu yetu. Ndiyo maana Bodi ya Wadhamini walianza mchakato wa kutekeleza sharti hilo lakini imeshindikana," alisema Kamwaga.

Na siyo Simba tu, wanaodhulumiwa huku wakijiona ni pamoja na watani wao wa jadi, Yanga na klabu nyingine zenye mvuto kwa washabiki nchini kama Mbeya City na timu iliyopanda ligi kuu msimu huu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara.

Watendaji wa Yanga wanasema wanashangaa kuona jezi na vifaa vingine vyenye nembo ya Yanga vikiuzwa katika maeneo mbalimbali nchini bila klabu hiyo kunufaika na biashara hiyo.

Baraka Kizuguto, kaimu ofisa habari wa Yanga, alisema klabu hiyo haina ubia na kampuni yoyote kutengeneza vifaa vya michezo kwa ajili ya mauzo.

"Tunasikitika kuona jezi na vifaa vingine vingi vyenye 'logo' (nembo) ya Yanga vinauzwa nchini bila sisi kuambulia chochote. Mpaka sasa hatuna makubaliano na kampuni yoyote kutengeneza na kuuza jezi zetu," anasema Kizuguto.

Hata hivyo, bidhaa feki zenye nembo za Yanga na watani wao wa jadi, Simba zimekuwa zikiuzwa kwenye kumbi za mkutano mkuu na viambaza vya majengo ya ofisi za makao makuu ya klabu hizo jijini Dar es Salaam.

Wakati mwingine, viongozi wa Simba na Yanga wamekuwa wakinunua jezi hizo feki kwa ajili ya kuwavalisha wachezaji wao wapya wakati wanawasajili au wanapowasili nchini.

MBEYA CITY YAPOTEZA MIL. 100/-
Uongozi wa Mbeya City nao umetangaza vita dhidi ya tabia hiyo kwa kuanzisha msako wa wafanyabiashara wanaouza jezi na bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo.

Msemaji wa klabu hiyo, Fred Jackson, aliiambia NIPASHE mjini Mbeya Mei 5, mwaka huu kuwa baada ya kuonekana ina mafanikio katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, jezi na skafu za Mbeya City zimekuwa zikiuzwa kwa wingi katika miji mbalimbali nchini bila klabu hiyo kunufaika.

Kutokana na hali hiyo, Jackson alisema klabu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, imeweka watu wake maalum wanaozunguka mitaani katika miji mbalimbali nchini kuwabaini watu wanaouza bidhaa zenye nembo yao bila makubaliano.

“Kuna wafanyabiashara wanauza jezi zenye nembo yetu ambayo ni alama ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Jambo hili ni hatari kwani wanaonufaika ni wao na si sisi ambao tunaihudumia timu kwa kila hali.

Kuanzia sasa mtu tutakayemkamata anauza bidhaa hizo pasipo idhini yetu, tutampeleka mahakamani ili akakumbane na sheria maana huo ni wizi wa wazi,” aliema Jackson.

Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda, alisema wamepoteza zaidi ya Sh. milioni 100 katika kipindi cha mwaka mmoja (Juni 2013 - Juni 2014) kutokana na maharamia wanaouza jezi za timu hiyo.

"Ni fedha nyingi tumepoteza tangu maharamia hawa waanze kuiba jezi zetu na kuziuza. Kwa tathmini ya haraka, katika kipindi cha mwaka mmoja Sh. milioni 100 tumeibiwa kutokana na mauzo ya jezi feki zenye nembo ya timu yetu," anasema.

Alisema hatua za makusudi zimeanza kuchukuliwa na uongozi wa timu pamoja na wamiliki wa klabu hiyo, Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kufanya msako wa kubaini wezi wanaouza jezi feki mitaani na wengine tayari wameshafikishwa mahakamani.

NDANDA FC
Uongozi wa Ndanda FC unasema baadhi ya wafanyabiashara wameanza kuihujumu klabu hiyo kwa kutengeneza vifaa vya michezo zikiwamo jezi zenye nembo ya klabu huku pesa zote zikiishia kwenye mifuko ya wafanyabiashara hao.

Katika mahojiano na gazeti hili jijini Dar es Salaam Mei 26, mwaka huu, Mkurugenzi wa klabu hiyo, Athuman Kambi alisema wamebaini kuuzwa kwa jezi na skafu feki za Ndanda FC katika maeneo mbalimbali nchini bila klabu hiyo kuambulia chochote kutokana na mauzo hayo.

Kambi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mtwara, alisema baada ya kufanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu na kufanikiwa kupanda ligi kuu, wafanyabiashara wameanza kutumia fursa hiyo kujipatia fedha kwa kutengeneza na kuuza vifaa vyenye nembo ya klabu hiyo inayovutia wapenzi wengi wa michezo, hasa Kusini mwa Tanzania.

"Tumebaini wafanyabiashara wameanza kujipatia fedha nyingi kwa kutengeneza na kuuza jezi za Ndanda FC kinyume cha sheria. Hivi karibuni tuliwakamata baadhi yao na kuwafikisha Kituo cha Polisi Msimbazi," alisema Kambi na kuongeza:

"Ndanda FC bado haijaanza kutengeneza jezi kwa ajili ya kuuza, uongozi upo katika hatua za mwisho kuingia mkataba na kampuni ambayo itashaghulikia suala hilo."

JEZI HUINGIZWAJE NCHINI?
Kutokana na uchunguzi walioufanya mwaka jana, maofisa wa Mbeya City wanasema wamebaini kuwa wafanyabiashara wanaojihusisha na hujuma hizo huagiza vifaa hivyo kutoka nchi za nje, hasa China.

"Jezi nyingi za Simba, Yanga na Mbeya City zipo kwenye maduka ya nguo Dar es Salaam, wafanyabiashara wakubwa nchini huziagiza China,” alisema Jackson.

“Katika mechi yetu dhidi ya Yanga jijini Dar es Salaam (Januari 28, mwaka huu) tulimkamata mama mmoja (anamtaja) akiwa na mzigo wa jezi 120 za Mbeya City. Zote zilikuwa feki kwa sababu zilikuwa na maandishi ya Kichina kifuani.

“Jezi zetu halali zinatengenezwa na kampuni ya 'Uhlsport' ya Ujerumani. Tulimchukulia hatua kwa kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

"Kilichotushtua zaidi, alikuwa akiuza bukta pamoja fulana ya Mbeya City kwa Sh. 12,000 tu wakati sisi tunauza na fulana peke yake kwa Sh. 15,000. Pia alikuwa na vifaa vingine vingi zikiwamo kofia, bendera na 'key holders' (vishika funguo) ambazo timu yetu bado haijaanza kutengeneza," alisema zaidi Jackson.

WAUZA JEZI WANENA
Katika maeneo ya Shinyanga, Zanzibar, Mbeya, Tanga, Tabora, Morogoro, Arusha, Bukoba, Dodoma na Dar es Salaam, mwandishi alizungumza na wauzaji wa jezi ambao wamekuwa wakizifuata timu za Simba, Yanga na Mbeya City kila zinakokwenda kucheza au kuweka kambi nchini.

Katika mahojiano na NIPASHE Machi 22, mwaka huu mjini Tabora, mmoja wa wauzaji wa jezi aliyejitambulisha kwa jina moja la Beka, alisema kuwa kwa miaka sita sasa amekuwa akiuza jezi za timu na wachezaji wanaofanya vizuri VPL.

“Jezi ambayo kwa sasa (Machi mwaka huu) inauliziwa sana na wateja wetu ni ile waliyovaa Yanga nchini Misri wakati wanakipiga dhidi ya Al Ahly, jezi hiyo bado haipatikani madukani,” anasema Beka na kubainisha:

"Jezi za Yanga zenye namba 25 au jina la Okwi (Emmanuel) ndiyo zinaongoza kwa mauzo kwa sasa zikifuatwa na jezi za Ngasa (Mrisho). Upande wa Simba, Tambwe (Amisi) na Messi (Ramadhani Singano) ndiyo wanauza sana.

"Jezi za Mbeya City zinauzika sana timu hiyo inapokwenda Dar es Salaam kucheza dhidi ya Yanga au Simba. Jezi zao halali zinapatikana kwa Sh. 15,000, lakini kuna kipindi tulikuwa tunaziuza hadi Sh. 25,000 kutokana na kutisha kwa timu hiyo ligi kuu.

“Jezi zao tunazozipata kwa njia ya panya wakati mwingine tunaziuza Sh. 10,000 kulingana na hali ya soko," alisema zaidi mkazi huyo wa Buguruni, Dar es Salaam.

WAUZAJI HUPATAJE JEZI?
Yasin Aziz, muuzaji wa rejareja wa jezi, aliliambia gazeti hili mjini Arusha Aprili 13, mwaka huu kuwa jezi za Simba, Yanga na Mbeya City huzinunua kwenye maduka ya nguo ya Kariakoo, Dar es Salaam kwa bei ya jumla ya Sh. 7,500 kwa kila jezi.

"Kuna kinachoshindikana hapa Bongo? Jezi tunazipata Kariakoo, gharama za kuchapa jina au namba ya mchezaji pale Kariakoo kwa kila jezi inaanzia Sh. 500 hadi 1,500," anasema Aziz, mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam.

WAFANYABIASHARA KARIAKOO
Baadhi ya wauzaji wa maduka ya jezi katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam wanasema jezi za Simba, Yanga, Mbeya City na klabu nyingine za soka nchini wanazipata kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao huziagiza nje ya nchi.

Mmoja wa wauzaji hao (jina linahifadhiwa) aliiambia NIPASHE jijini Dar es Salaam Julai 24, mwaka huu kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa nchini wakiwamo vigogo wa klabu za Simba na Yanga huwauzia kwa bei ya jumla jezi na vifaa vingine vya michezo vyenye nembo za klabu hizo.

Alibainisha kuwa yeye na wauzaji wenzake wa maduka ya jumla ya jezi katika soko hilo hununua jezi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kwa bei ya jumla ya Sh. 6,500 hadi Sh. 7,500 kwa kila jezi nzito na Sh. 4,500 hadi Sh. 6,000 kwa jezi nyepesi.



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: