Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) siku ya jumanne ambapo alitumia fursa hiyo kuainisha masuala mbalimbali yatakayopewa kipaumbele wakati wa Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki ijayo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani. Mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola ni moja ya suala litakalopewa kipaumbele cha pekee wakati wa mkutano huo utakaohudhuriwa na wa viongozi zaidi ya 140 wakuu wa nchi na serikali, viongozi wa asasi za kiraia, na wakuu wa mashirika mbalimbaliya Kimataifa.
Na Mwandishi Maalum,
New New York
Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 140 kutoka mataifa mbalimbali duniani
wamethibitisha kuhudhuria na
kushiriki majadiliano ya jumla wakati wa Mkutano wa 69
wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki hii
Akizungumza na
waandishi wa habari hapo siku ya
Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema, viongozi hao pamoja na kujadili
changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa, watautumia mkutano huu kujadiliana kwa kina
kuhusu mchango na ushiriki wa jumuiya ya
kimataifa katika kuukabili mlipuko wa
ugonjwa hatari wa Ebola.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete ni miongoni wa viongozi hao 140
na anaongoza ujumbe wa Tanzania katika
Mkutano huu.
Akizungumzia zaidi
kuhusu mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola na athari zake kwa uhai wa mwanadamu
na kwa maendeleo ya kiuchumi na
kijamii, Ban ki Moon amewaeleza waandishi hao, kuwa Jumuiya ya kimataifa
haiwezi kuendelea kuufumbia macho na kwamba kadiri inavyochelewa kuutafutia
ufumbuzi ndivyo hatari yake inavyozidi
kuongezeka.
“Tutatoa kipaumbele cha peke kuhusu ugonjwa wa Ebola ambao
umeleta athari kubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika ya Magharibi na maeneo
mengine. Siku mbili zijazo ( Alhamisi) Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa
Mataifa litakutana kwa dharura kuzungumzia mlipuko wa Ebola. Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Afya Duniani Margaret Chan na Mimi tutazungumza katika mkutano huo”
akasema Ban Ki Moon
Akaongeza kwa kusema wiki ijayo Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa litakuwa na mkutano wa kilele kuhusu mahitaji ya watu na nchi
zilizokabiliwa na ugonjwa wa Ebola.
Pamoja na
kujadili na kutafuta mkakati wa
pamoja wa kukabiliana na Ebola, Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema viongonzi hao wakuu wa nchi na serikali pia
wanatarajiwa kujadili na
kubadilishana mawazo kuhusu changamoto za mabadiliko ya tabia nchi
katika mkutano utakaofanyika septemba
23.
Mhe. Rais Jakaya
Kikwete ni kati ya Viongozi walioalikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuhudhuria na kuzungumza katika
mkutano huu muhimu kuhusu suala zima la
mabadiliko ya tabia nchi na athari zake.
Akielezea zaidi kuhusu mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi,
Ban Ki Moon anasema mkutano huo utakuwa
na malengo mawili, kwanza ni kukusanya utashi wa kisiasa ili kufikia makubaliano ya pamoja hapo
mwakani katika mkutano utakaofanyika huko Paris , Ufaransa. Na pili kuchukua
hatua madhubuti za kupunguza uzalishaji
wa gesi chafu.
Akiainisha zaidi kuhusu ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa
wakati wa Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema, majadiliano ya Baraza Kuu ( General Debate) yatakayoanza
septemba 24 yatatumika kukusanya nguvu za pamoja za kuushinda umaskini, na kupitisha ajenda za
malengo mapya ya maendeleo endelevu .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete atalihutubia Baraza Kuu
Septemba 25.
Masuala mengine ambayo pia
yanatarajiwa kutawala mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa
Ban Ki Moon, ni pamoja na
migogoro na machafuko yanayoendelea katika nchi za Syria, Iraq, Libya, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ukraine, Sudan ya
Kusini ukiwamo pia mgogoro kati ya Palestina na Israel.
No comments:
Post a Comment