Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira amesema mgogoro wake na Jaji Joseph Warioba uliotokana na kura za maoni ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, ndiyo uliomsukuma kujitoa chama tawala na kujiunga na NCCR-Mageuzi.
Hata hivyo, katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM) amesema hajutii uamuzi wake huo kwa kuwa anaamini historia imeandikwa.
Wasira aliingia kwenye mgogoro na Jaji Warioba wakati mwanasheria huyo akiwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais katika Serikali ya awamu ya pili na Wasira akiwa Waziri wa Kilimo.
Wasira alisema hakwenda NCCR-Mageuzi kwa lengo la kufanya ushushushu na baadaye kurudi CCM kama alivyofanya mwaka 2000, bali alikwenda huko baada ya haki yake kuminywa na viongozi wa CCM wa wakati huo.
Alieleza kuwa baada ya uchakachuaji huo katika kura za maoni, aliamua kwenda Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam kukata rufaa, lakini hata huko hakutendewa haki, kwani rufaa yake iliwekwa kiporo na ingesikilizwa baada ya uchaguzi mkuu.
Mgogoro ulivyoanza
“Nataka mwelewe kwamba mimi sikwenda upinzani kwa sababu nilikuwa napingana na sera za CCM. Kwanza 1985 nilikuwa mbunge na ndiyo maana Rais Ali Hassan Mwinyi aliniteua kuwa waziri wa kilimo,” alisema Wasira na kuongeza;
“Mwaka 1990 niliacha kugombea kwa kumwachia Jaji Warioba. Kwa sababu kama utakumbuka mwaka 1985 Warioba alikuwa ameteuliwa kuwa mbunge na waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais.”
Wasira alisema aliamua kumwachia Jaji Warioba kwa kumheshimu kwani aliamini ingekuwa kampeni ngumu kwamba waziri mkuu anachuana na waziri wa kilimo, ingawa hata hivyo, alisema iwapo angeamua kuchuana naye angemshinda.
“Lakini lile jimbo lilikuwa la kwangu kwa sababu mimi ni kiongozi kutokea chini kwenda juu na mwenzangu Warioba ni mwanasiasa wa kutokea juu kwenda chini,” alisema.
Wasira ambaye alionekana kuukumbuka vizuri mgogoro huo alisema, “Hiyo ndiyo tofauti iliyopo. Kwa hiyo kama mimi ningeamua kuchuana naye, angeshindwa mwaka huo wa 1990. Sasa faida yenyewe iko wapi?” alihoji Wasira.
“Mimi nikaamua kujitoa si kwa kumwogopa Warioba, hapana. Hii ilinipa sifa nzuri kwa sababu Mwalimu (Julius Nyerere) aliniambia umefanya jambo la heshima sana,” alisema.
Hata hivyo, Wasira alisema ilishangaza kuona Mwalimu Nyerere alimsifia kwa uamuzi wake huo, lakini Warioba mwenyewe aliyeachiwa jimbo hilo hajamsifia wala kumpongeza.
Alisema katika kipindi chote cha miaka mitano aliyomwachia Warioba jimbo hilo, wananchi hawakupata huduma nzuri hivyo wakamtaka yeye arudi mwaka 1995.
“Wapigakura wetu hawakupata huduma nzuri sana katika miaka hiyo mitano. Labda kwa kuwa alikuwa mtu mwenye shughuli nyingi sana kwa hiyo hakugusa msingi wa watu wa kawaida, kukawa na manung’uniko mengi,” alisema Wasira na kuongeza;
“Walinung’unika sana kwamba mimi nimewaacha nimekabidhi jimbo lao kwa mtu ambaye hayuko karibu na wao, basi kukawa na demand (hitaji) la mimi kurudi. Sasa mwaka 1995 mimi nikarudi kupitia CCM. Hiyo ndiyo nataka mjue.”
Alifafanua kuwa wakati huo kura ya maoni ilikuwa ikifanyika kata kwa kata ikiwahusisha mabalozi wa nyumba kumi na walipofanya kura hiyo katika kata kumi kati ya 12 yeye (Wasira) akawa ameshinda kata nane za jimbo hilo.
“Nikawa nimeshinda nane yeye ameshinda mbili, lakini zimebaki nyingine mbili. Kati ya mbili zilizobaki, moja ni ya nyumbani kwake kwa hiyo ili ashinde ilikuwa sasa lazima aweze kufanya mbinu,” alidai Wasira katika mahojiano hayo.
Wasira alisema mbinu iliyotumiwa na Jaji Warioba wakati huo ilikuwa ni kuwafanya wananchi karibu wote wa kata hiyo wapige kura upande wake badala ya mabalozi wa nyumba kumi kama Katiba ya CCM ilivyokuwa inaelekeza.
“Unaweza uka-imagine (kufikiria) kijiji chote sasa kinapiga kura, kila mtu akageuka kuwa balozi wa nyumba kumi. Kwa ajili ya ku-offset (kuondoa) tofauti kati ya ushindi wangu wa kata nane ili uweze kujibiwa na kata moja,” alisema Wasira.
Alisema hali hiyo ilimfanya ajitoe katika kinyang’anyiro hicho baada ya kutoridhishwa na namna uongozi wa CCM Wilaya ya Bunda ulivyoshindwa kuingilia kati suala hilo la wazi.
Ashtaki kwa makao makuu
Waziri Wasira alisema baada ya kuona suala hilo limeshindwa kupata mwafaka, yeye na wazee kadhaa wa jimbo hilo walifunga safari hadi makao makuu ya CCM jijini Dare es Salaam ili kumshtaki Jaji Warioba.
“Sasa manung’uniko tukayaleta makao makuu ya chama wakati ule Lawrence Gama (Marehemu) ndio alikuwa katibu mkuu. Tukaja kukata rufaa na wazee wa CCM kutoka Bunda wanasema uchaguzi si sawa,” alisema Wasira na kuongeza;
“Wale wazee sasa tulipokuja kwa mheshimiwa Gama akatuambia hilo tatizo lenu tutalishughulikia baada ya uchaguzi. Tukasema hii hakuna haki sasa, maana baada ya uchaguzi wakati uchaguzi ndiyo hoja, haukuendeshwa vizuri?”
“Tulitarajia katibu mkuu atasema anaingilia kati ili uchaguzi urudiwe, sasa badala ya kusema unarudiwa anasema kesi itasikilizwa baada ya uchaguzi, tukawa njiapanda mimi pamoja na wale wazee tuliokuja nao Dar es Salaam.”
Kuhamia NCCR-Mageuzi
Wasira alisema kutokana na kukasirishwa na namna marehemu Gama alivyoshughulikia suala hilo, wale wazee walimweleza kuwa jimbo hilo lingeangukia mikononi mwa upinzani kwa kuwa Jaji Warioba alikuwa hakubaliki kwa wananchi.
“Wakaniambia hata usiposimama wewe sasa, kwa sababu hutasimama kupitia CCM akisimama mtu mwingine wa vyama vya upinzani atachukua na ambaye anaweza kuwa dhaifu zaidi,” alisema Wasira na kuongeza kuwa;
“Kwa hiyo wale wazee wakaniambia utoke CCM uende chama kingine ili uchukue lile jimbo uendelee kuongoza. Lakini wao wakasema hawatoki CCM watanipigia kura wakiwa huko huko.”
“Sikwenda NCCR-Mageuzi kwa sababu nilikuwa napinga sera za CCM, hapana. Nilienda kunusuru jimbo kwa sababu nimeshindwa kupata jibu CCM,” alisema Wasira na kueleza kuwa huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuhamia NCCR-Mageuzi.
“Kwa hiyo nikaenda NCCR-Mageuzi, (hicho chama) bado kipo niliingia bila kujua madhumuni na mpaka leo bado sijasoma madhumuni hayo, lakini nikaenda. Unaingia chama siku hiyo hiyo unapewa na kadi na uteuzi hapo hapo,” alisema Wasira.
“Tukaenda tukagombea ubunge tukamshinda Warioba. Nikawa mbunge na bwana Warioba akakimbilia mahakamani. Warioba ni jaji, sasa kesi ya tumbili unampelekea nyani sina hakika sana kama nitashinda. Siwezi kusema zaidi ya hapo.”
Wasira alisema Mahakama Kuu ilisikiliza shauri hilo la kupinga matokeo ya uchaguzi na kuamua kutengua ubunge wake na kumzuia kugombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuridhika na madai ya ushindi wake kugubikwa na rushwa.
“Tumefanya kesi nimezuiwa kugombea tena, tumekaa, nikaenda kuuza samaki zangu pale Msasani (Dar es Salaam) kwenye kituo changu cha Cold Storage maana huwezi kusema kwa vile umetoka basi kazi yako ni kusubiri ufe, lazima utafute suluhisho,” alisema.
“Nilifanyafanya pale vibiashara na vyenyewe havilipi lakini haikupita muda mrefu sana nikaamua kurudi CCM,” alisema na kuongeza; kwa sababu mimi kwa kweli historia yangu ni ya ndani ya CCM tangu nina miaka 13, sasa utaenda wapi, lakini siyo kwamba historia haikuandikwa, historia imeandikwa na uzoefu nimepata.”
Kuhusu upinzani
Wasira alisema hivi karibuni alikutana na mtu mmoja ambaye hata hivyo hakutaka kumtaja, akimtaka ampe uzoefu wake kuhusu vyama vya upinzani nchini kwa kuwa yeye aliwahi kuwa huko.
“Nikamwambia mimi naviona kama ni vya watu binafsi. Kwa mwenye chama chake huwezi kusema lolote. Aliyekianzisha ndiye huyo huyo anaendelea nacho,” alisema na kuongeza;
“Ukijaribu kupambana naye unapata matatizo. Mrema (Augustino wa TLP) alipata matatizo sana NCCR-Mageuzi kwa sababu kile chama kilikuwa cha Marando (Mabere) na Mbatia (James).”
Wasira alisema chama hicho kilimkodisha Mrema mwaka 1994 kwa kuwa alionekana kama ana nguvu kidogo, lakini baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wakamtosa.
“Wakagombana na Marando. Marando tukamwambia si mtoke wote akasema hakuna, bora kifo. Hilo ndilo tatizo la vyama hivyo vipya, anayevianzisha ndiye anaendelea tu na demokrasia ni ndogo sana,” alisisitiza Wasira.
“Wala msijidanganye sana ukaona televisheni watu wanapiga makofi siyo rahisi. Hao waanzilishi wa hivyo vyama siyo rahisi kutoka na mifano ipo wala sitaki kutaja majina ya watu kwa sababu mnawajua na vyama mnavijua.”
“Siwezi kujuta kutoka CCM kwenda NCCR- Mageuzi kwa sababu nilikuwa natafuta haki na haki zina gharama. Unachojutia ni nini, si uamuzi niliufanya mimi na haki nilinyimwa mimi nikaitafuta kwa njia nyingine sasa kujuta unajutia nini?” alihoji.
Makosa ya uteuzi CCM
Mbunge huyo wa Bunda ambaye pia anatajwatajwa kuwania urais, alibainisha kuwa kushindwa kwa CCM katika baadhi ya majimbo baada ya vyama vingi nchini, kulichangiwa na uteuzi mbovu wa wagombea na mizengwe kwa wale walioongoza kura za maoni.
“CCM ni taasisi inayoongozwa na wanadamu wala siyo kwamba yenyewe huwa haifanyi makosa. Ni taasisi ya kibinadamu tu. Mahali pote CCM tulishindwa kwenye majimbo, tulishindwa kutokana na makosa yetu katika uteuzi,” alisema Wasira.
“Shibuda (John) ni mfano mmojawapo, lakini majimbo ya Iringa Mjini, Mbeya, Musoma Mjini, Arusha na Lindi, mahali popote unaposikia CCM imeshindwa lazima kuna makosa fulani imefanya halafu hao wapinzani wakapita.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment