ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 30, 2014

Hiace yaua watu 12 Arusha


Watu 12 wamekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa baada ya basi dogo aina ya Toyota Hiace (pichani) maarufu kama kipanya walikokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana majira ya saa 10 katika eneo Makumira wilayani Arumeru.

Sabas, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya kipanya hicho aina ya Nissan T519 DBV kilichokuwa kikitokea jijini Arusha kwenda Usa River kuhama upande na kugongana uso kwa uso na lori hilo lenye namba za usajili T582 ACR lililokuwa likitoka Moshi mkoani Kilimanjaro kwenda Arusha Sabas alisema majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tengeru kwa matibabu.


Alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru kusubiri ndugu kuichukua kwa maziko.

Alisema baada ya ajali hiyo kutokea dereva wa lori hilo alikimbia na kwamba polisi wanaendelea kumtafuta.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya rufani ya Mount Meru, Dk. Josiah Mray, alithibitisha kwamba walipokea maiti za watu 12 waliokufa papo hapo katika eneo la ajali.Dk. Mray alisema kuwa walipokea majeruhi mmoja ambaye hali yake ni mbaya.

Hadi tunakwenda mitambo, Sabas hakutaja majina ya marehemu hao kwa kuwa zoezi la kuwatambua pamoja na majeruhi hao lilikuwa linaendelea na kuahidi kutoa taarifa baada ya kukamilika.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: