Hii ni kwa sababu wameingia kwenye penzi na watu ambao si sahihi. Kutokana na mazingira hayo, haiwezi kuwa kitu cha ajabu mume wa mtu kutokea kumpenda sana mke wa mtu au kinyume chake.
Pia huwezi kuonekana mwendawazimu kwa kumpenda mtu ambaye tayari ana mpenzi wake. Hii ni kwa sababu inawezekana una mapenzi ya kweli zaidi kwake kuliko huyo aliye naye. Hata hivyo, hakuna kitu kibaya kama kuanzisha uhusiano na mtu ambaye tayari ana mpenzi wake au ameshaingia kwenye ndoa. Utakuwa unatafuta matatizo kama utamtongoza mke wa mtu au utaonesha kumzimikia mume wa mtu na kujikuta ukishawishika kutaka kumpasulia ukweli.
Madhara yake ni makubwa kwani kuingilia uhusiano wa watu kunaweza kuyagharimu maisha yako. Wapo ambao wameuawa kwa kuwapenda wake za watu. Yawezekana si kwa u-kiwembe wao bali mapenzi ya kweli waliyonayo lakini ukweli unabaki kwamba, unayempenda tayari ana mtu wake, wewe huna jinsi tena. Itakubidi ubaki ukiumia moyoni huku wakati mwingine ukiomba hata waachane ili wewe uweze kuchukua nafasi. Hiyo inatokea sana huko mtaani.
Sasa basi, ni yapi ambayo unatakiwa kuyafanya pale ambapo umetokea kumpenda mtu ambaye tayari ana mtu wake? Kwanza kabisa, hakikisha unafanya kila uwezalo ajue kile kilichomo moyoni mwako. Tumia mbinu yoyote kumpata na kumpasulia ukweli. Utamueleza jinsi unavyompenda na namna anavyokukosesha amani lakini mwisho wa siku mweleze kwamba humaanishi aachane na huyo aliyenaye bali kokote atakakoenda ajue yupo mtu f’lani, sehemu f’lani anampenda.
Ukifanikiwa kufanya hivyo, angalau unaweza kubaki na amani. Kunaweza kuwa na ugumu kumpata kutokana na mazingira hasa ukichukulia kwamba kunatakiwa kuwe na usiri mkubwa sana kwenye kufikisha ujumbe huo. Pili, hakikisha unaonana naye mara kwa mara. Hiyo angalau itakupunguzia machungu hasa kama na yeye atakuwa na chembechembe za kukupenda.
Ukibahatika kuonana naye akiwa peke yake, msalimie kwa kumchangamkia huku ukionesha kufarijika kukutana na mtu ambaye ana nafasi kwenye moyo wako. Tatu, weka kumbukumbu kwa kumnunulia zawadi ndogo au kubwa ambayo itamfanya kila anapoiangalia akukumbuke. Isiwe zawadi ambayo inaweza kumletea matatizo kwenye uhusiano wake. Kwa mfano, kama ni mwanafunzi unaweza kumnunulia kalamu au leso, vitu ambavyo hata mpenzi wake hawezi kumshitukia. Kama ni mtu mnayefanya kazi au mnasoma pamoja, siku mojamoja mkikutana hotelini, mlipie bili ya chakula au kinywaji.
Fanya hivyo bila mtu mwingine kujua. Unajua kwa nini hii inatajwa kuwa moja ya njia inayoweza kukufanya ukawa na amani? Ni kwa sababu endapo ataipokea zawadi ama ofa yako, utabaki na furaha hata kama hajakukubalia wewe uwe mpenzi wake.
Kumbuka unafanya hayo yote si kwa ajili ya kumtega wala kumshawishi achepuke au amuache mpenzi aliyenaye awe na wewe, unafanya hayo kuonesha upendo wako kwake lakini pia kutafuta amani ya moyo. Tahadhari kubwa unayotakiwa kuichukua ni kuhakikisha humshawishi kufanya naye mapenzi wala kumuonesha upendo wako katika mazingira ambayo yeye asingependa. Kwa mfano, yawezekana kutokana na unavyomzimikia ukajikuta unatamani kumpigia simu na kuongea naye au kumtumia hata sms nzuri.
Usithubutu kabisa kufanya hivyo kwani unaweza kumfanya akuogope na asikuchangamkie akihisi utamharibua uhisiano wake. Pia epuka kuonesha upendo wako kwake akiwa na marafiki zake. Ukifanya hivyo inawezekana mmoja wa marafiki zake anajuana na mpenzi wa huyo unayempenda kisha akazifikisha taarifa ikawa tatizo. Mawasiliano yako na yeye ikiwezekana iwe mnapoonana tu akiwa hayuko na mpenzi wake.
Hii ni kwa sababu unaweza kumtumia sms kumbe simu anayo mpenzi wake au ukampigia simu akapokea mpenzi wake na kusababisha matatizo kwa mwenzako. Mwisho naomba niseme kwamba, unapotokea kumpenda mtu ambaye yuko kwenye uhusiano, hata kama na yeye anakupenda, chukulia kwamba huwezi kumpata tena.
Tafuta mwingine ambaye utamuonesha mapenzi yako na hakikisha unapambana na hisia zako za kumpenda mpenzi wa mwenzako kwani ukiziendekeza, zitakutesa sana. Nihitimishe kwa kukuambia wewe msomaji wangu kwamba, kumpenda mtu mwingine licha ya kwamba uko kwenye uhusiano wala si dhambi, ni hali ya kawaida ya kibinadamu inayowakumba wengi.
Kikubwa ni kuwa makini katika kila unachokifanya ili uendelee kuishi maisha ya furaha na amani lakini pia huwezi jua, yawezekana siku moja Mungu akatimiza aliyopanga na huyo unayempenda akaingia mikononi mwako. Kumbuka subira inahitajika katika kila jambo!
GPL
No comments:
Post a Comment