.Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi akichangia majadiliano kuhusu ajenda ya uthibiti wa silaha za nyukilia hapo siku ya jumanne. Akizungumza msimamo wa Tanzania kuhusu silaha hizo, Balozi Mwinyi amezitaka nchi zinazomiliki silaha hizo kuonyesha utashi wa kisiasa wa kuzipunguza na kuzidhibiti ili zisisambae kiholela lakini pia waihakikishie dunia usalama wake.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakifuatilia majadiliano kuhusu upunguzaji wa silaha za nyukilia ambapo wazungumzaji wengi pamoja na Tanzania walisisitiza haja na umuhimu wa kuwa na maeneo huru yasiyo na silaha za nyukilia kwa usalama wa dun dunia na wakatoa wito kwa Shirika linalohusika na masuala ya Nguvu za Nyukilia kuhakikisha kwamba kila nchi inakuwa na haki ya kupata elimu na teknolojia inayohusiana na nguvu za nyukilia bila ubaguzi au upendeleo.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeungana na mataifa mengine wapenda amani katika kuyachagiza mataifa yenye silaha za nyukilia kuonesha utashi na utayari wa kweli wa kutekeleza mkataba unaodhibiti usambaaji holela wa silaha hizo ( NPT).
Kauli ya kuyataka mataifa hayo yenye silaha za nyukilia kuutekeleza Mkataba huo imetolewa siku ya jumanne na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Ilikuwa ni wakati Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilipokuwa ikijadili ajenda inayohusu silaha za nyukilia na tisho lake kwa usalama na amani ya dunia.
Katika mchango wake, Katika kamati hiyo inayohusika na masuala ya upokonyaji wa silaha na Amani ya kimataifa,Tanzania licha ya kuyataka mataifa yenye silaha hizo kuchukua hatua za kuzipunguza na kuzidhibiti, imekwenda mbali zaidi kwa kuyataka pia kuihakikishia dunia usalama wake.
Akatoa wito kwa mataifa yenye silaha hizo kuzingatia masharti ya Mkataba wa NPT.
Balozi Mwinyi amesema Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine, pamoja na kuunga mkono juhudi za upunguzaji na udhibiti wa silaha za nyukilia, pia inaunga mkono umuhimu wa kuwapo kwa maeneo huru yasiyo na silaha za nyukilia kama sehemu ya kuihakikishia dunia usalama.
Hata hivyo akasema, inasikitisha kuwa licha ya nia hiyo njema ya kuwa na maeneo huru yasiyo na silaha za nyukilia bado kumekuwa na kusuasua katika majadiliano ya kuanzishwa wa eneo huru katika Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine Tanzania imelitaka Shirika linalohusika na masuala ya nguvu za nyukilia kuhakikisha kuwa elimu na teknolojia inayohusiana na masuala ya nyukilia inatolewa kwa mataifa yote pasipo ubaguzi.
Akasisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono matumizi sahihi na salama ya nishati ya nguvu za nyukilia na ni kwasababu hiyo inasisitiza kila taifa kuwa na haki ya kupata elimu na teknolojia inayohusiana na eneo hilo.
Majadiliano kuhusu ajenda hiyo ya silaha za nyukilia mara zote inapojadiliwa huwa na vuta nikuvute ya aina yake na malumbano ya hapa na pale , kutokana na ukweli kuwa zile nchi ambazo hazina silaha hizo zimekuwa zikisisitiza haja na umuhumu wa kutekeleza mkataba wa NPT huku mataifa yenye silaha hizo yakitetea uhalali wa umiliki wa silaha hizo au zikiainisha hatua ambazo zimeaza kuchukua katika kuzipunguza hatua ambazo Jumuiya ya Kimataifa inasema hazitoshi.
Wapo baadhi ya wazungumzaji ambao walieleza wazi wazi kutoridhishwa na baadhi ya nchi ambazo licha ya kuwa zinamiliki silaha hizo, lakini hadi sasa hazijakiri hadharani kuwa zinamiliki na hivyo kuwa sehemu ya kikwazo katika mchakato mzima wa kuzidhibiti.
Vile vile zipo nchi zinazomiliki silaha hizo ambazo zimeeleza bayana kwamba hazitaacha utengenezaji wake au hata majaribio mpaka pale mataifa makubwa nayo yatakapoonyesha utashi wa kweli wa nia ya kufanya hivyo
Hapana shaka kwamba kuendelea kuwapo kwa silaha hizo za nyukilia na kutokuwapo kwa uwazi au utashi wa kisiasa wa kuzipunguza, dunia bado itaendelea kukabiliwa na changamoto ya silaha hizo za maagamizi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake