Simba imeamua kufanya mazungumzo ya kumsajili Kaseja kutokana na ripoti ya Kocha Mkuu, Mzambia Patrick Phiri, iliyoeleza kuwa inahitaji kupata kipa mzoefu ambaye ataisaidia timu kupata matokeo mazuri.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh, alisema tayari amepokea wito wa kuhudhuria kikao cha mazungumzo na viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba ili kuzungumzia usajili wa mchezaji huyo.
Abdulfatah alisema anaamini mazungumzo kati yake na Simba yatakwenda vizuri na kuhusu kiasi cha fedha ambacho kitahitajika ili kurejea kwenye klabu hiyo hana hofu kwa upande huo.
"Simba ni nyumbani, ninatarajia kukutana nao kesho (leo), kila kitu kitakwenda sawa, naamini hakutakuwa na tatizo lolote, hata mimi nitahakikisha kikao hicho kimalizike kwa heri," alisema Abdulfatah.
Meneja huyo aliongeza kwamba mbali na Simba, pia amepokea ofa nyingine kutoka klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi lakini si vema kuziweka hadharani.
YANGA HAINA CHAKE
Abdulfatah alisema licha ya Yanga kuendelea kumlipa mshahara wake lakini kisheria mchezaji huyo yuko huru.
Alisema mkataba wa Kaseja na Yanga ulivunjika rasmi kuanzia Novemba 8 mwaka huu kutokana na uongozi wa klabu hiyo kushindwa kumlipa fedha za usajili kama walivyokubaliana hapo awali.
"Yanga walipaswa kumlipa mchezaji wangu kiasi cha pili tangu Januari, lakini hadi leo hawajalipa chochote, pia hawajatekeleza makubaliano mengine yaliyoanishwa kwenye mkataba kama nyumba na bima," alisema Abdulfatah.
Uongozi wa Yanga ulikubaliana kumsajili Kaseja kwa dau la Sh. milioni 40, na ilimpa awamu ya kwanza Sh. milioni 20 mwaka jana na kiasi kingine kilichobakia ilipaswa kumalizia tangu Januari mwaka huu lakini hadi jana hakuna kilichotekelezwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, alisema milango iko wazi na wakati wowote endapo watamhitaji.Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu, alishindwa kuzungumzia madai ya Kaseja.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment