ANGALIA LIVE NEWS
Friday, November 14, 2014
UMOJA WA MATAIFA WATOA MWONGO DHIDI YA UWINDAJI HARAMU WA TEMBO AFRIKA
Na Mwandishi Maalu, New York
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Madawa ya Kulevya na Uhalifu mwingine ( UNODC) Novemba 13 imetangaza mwongozo ambao utachangia katika juhudi zinazoendelea za kukabiliana na mauaji holela ya tembo na biashara haramu ya pembe za ndovu hususani Afrika.
UNODC imetoa mwongozo huo kwa kile inachosema, ni kuongezeka kwa biashara hiyo ambayo sasa makundi ya kihalifu yanajihusisha kwa kasi, jambo linalotishia kutoweka kabisa kwa mnyama huyo.
Mwongozo huo, unahusu mbinu na taratibu za kitaalamu za kuchunguza sampuli na tathmini ya kimaabara katika kubaini vinasaba na hivyo kusaidia usambazaji wa teknolojia za kisasa za kuchunguza na kupambana na majangili dhidi ya tembo.
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa UNODC pamoja na Muungano wa Kimataifa wa kukabili uhalifu dhidi ya wanayama pori (ICCWC).
Inaelezwa zaidi kuwa kutokana na ongezeko la uwindaji wa haramu wa tembo, kuna ushahidi wa nguvu unaoonyesha ushiriki wa makundi ya wahalifu na katika baadhi ya maeneo makundi ya waasi ya wanamgambo wenye silaha ambao wanajinufaisha na biashara hiyo.
Kwa mujibu wa UNODC, mwongozo huo unatarajiwa kutumika kila mahali na kwamba ni mwongozo unaolenga kuwaongezea uwezo wa kiutendaji, waokoaji wa mwanzo, wachunguzi, waendesha mashtaka, mahakama na wataalamu wengine.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Bw. Yury Fedotov,amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, “ tunaamini matumizi ya mwongozo huu utachangia kwa wakati uchunguzi na hivyo kuongeza kasi ya kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa uhalifu huu na hatimaye kupunguza biashara haramu ya pembe za ndovu”.
Sambamba na hilo mwongozo huo utasaidia kuongeza matumizi ya ya teknolojia ya kuchunguza mauaji ( forensic) eneo ambalo wataalamu hao wanasema ni muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori, kutambua wapi wanyama hao walikouliwa au walikotoka na kusaidia utambuzi na hatimaye ukamataji wa wahalifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment