ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 26, 2014

MHE. BALOZI LIBERATA MULAMULA AMKARIBISHA BALOZI MPYA WA ZIMBABWE NCHINI MAREKANI UBALOZINI TANZANIA HOUSE


Mhe. Liberata Mulamula, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania nchini Marekani amemkaribisha Mhe. Ammon Mutembwa, Balozi mpya wa Jamhuri ya Zimbabwe Ubalozini Tanzania House, Washington DC, Marekani, Jumatano Novemba 26, 2014. Katika mazungumzo yake na Balozi Mutembwa, Mhe. Balozi Mulamula alimweleza Balozi huyo kwamba ajisikie kwamba yuko nyumbani. Mhe. Mulamula aliendelea kwa kusema kwamba Tanzania na Zimbabwe zina mahusiano ya kihistoria na kwa msingi huo ni vyema kutafsiri kwa vitendo mahusiano hayo kwa kujenga mashirikano zaidi baina yao. Mhe. Mulamula alifurahishwa na ziara hiyo ya Balozi Mutembwa Ubalozini na kuahidi kwamba kupitia kwa Jumuia ya Ushirikiano wa Nchini za Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania na Zimbabwe zina fursa ya kutosha kuziwakilisha nchi zao nchini Marekani kwa manufaa ya Serikali na wananchi wao.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Mutembwa alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kumkaribisha Ubalozini na kwamba kwa vile ndio kwanza ameripoti katika kituo chake kipya cha kazi atashukuru sana kupata mwongozo wake na ushauri kutoka kwake ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kiuwakilishi nchini Marekani kwa ufanisi. Balozi Mutembwa alisema pia kwamba moja ya jukumu lake kubwa  ni kuhakikisha vikwazo  ilivyoekewa nchi yake na Marekani vinaondolewa kupitia mazungumzo na kujenga maelewano mazuri baina ya  nchi yake na Marekani.


 Mhe. Liberata Mulamula, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Mexico(Kulia) akimkaribisha Mhe. Ammon Mutembwa,(Kushoto). Balozi  Mpya wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Marekani Ubalozini Tanzania House Washington DC,Marekani.

 Mhe.Balozi  Mulamula na Mhe. Balozi Mutembwa katika picha ya kumbukumbu baada ya kusaini kitabu cha wageni.

 Mhe. Balozi Liberata Mulamula(Katikati) akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Mhe.Balozi Ammon Mutembwa (Wa pili kushoto) huku Maofisa wao Bw. Suleiman Saleh (Wa kwanza kulia) na Bw. Whatmore Goora (Wa kwanza kushoto) wakifuatilia.


No comments: