ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 25, 2014

Muhongo ahusishwa wizi nyaraka za Escrow bungeni

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ametajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mmoja kati ya vijana wawili wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuiba kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge ripoti ya ukaguzi wa hesabu za zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizochotwa kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).Wakati Waziri Muhongo akitajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mtuhumiwa huyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye jana ilikuwa ni siku yake ya kwanza kuongoza Bunge tangu lianze Novemba 4, mwaka huu, anadaiwa kutajwa kuwamo katika orodha ya vigogo waliovuna fedha hizo, huku yeye akipata mgawo wa Dola za Marekani milioni moja.

Aliyemtaja Waziri Muhongo kuwa na uhusiano wa karibu na kijana huyo, ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.


Mnyika alimtaja Waziri Muhongo, wakati akichangia mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, bungeni jana.

Muswada huo uliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni, Ijumaa wiki iliyopita.

”Mheshimiwa Spika, ni muhimu ofisi yako ifuatilie. Kwa sababu mtuhumiwa yule ana uhusiano wa karibu sana na Prof. Sospeter Muhongo, ambaye ni mmoja wa watuhumiwa kwenye kashfa tunazozijadili,” alisema Mnyika.

Aliongeza: “Sasa nasema haya mapema ili isifikie hatua tukatumiwa kisingizio cha mambo kuwa mahakamani kushindwa kuwataja kwa majina wahusika. Polisi wafanye uchunguzi, wachukue hatua.”

Mnyika alisema uharamia kwenye suala IPTL wa muda mrefu umezidi mipaka.

Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, polisi wanamshauri Spika wa Bunge kwa sababu wanataka haraka haraka wamkimbize mtuhumiwa huyo mahakamani ili baada ya hapo alieleze Bunge kuwa kishapelekwa mahakamani, hivyo hakuna sababu ya kutaja jina wala suala lake kujadiliwa.

Mnyika alisema tangu siku waliyowapa polisi taarifa, mpaka leo wamekuwa wakisitasita wakishindwa kutaja jina la mtuhumiwa, huku wakisingizia uchunguzi.
Hata hivyo, alisema upande wa serikali wanapokutana nao kwenye korido wamekuwa wakiwaambia kuwa mhusika anafahamika, ikiwa ni pamoja na watu wote ambao amekuwa akiwasiliana nao.

“Mheshimiwa Spika, ukiendelea kuyakinga mambo haya kwa kisingizio cha mambo kuwa polisi, halafu baadaye polisi wakaenda mahakamani, ukaja kuyakinga hapa kwa kisingizio cha kwamba mambo yako mahakamani, maana yake Mheshimiwa Spika na wewe utahesabika kwamba, hizo mbinu za hao maharamia waliopora ripoti ndani ya ofisi yako pengine na ofisi yako inahusika,” alisema Mnyika.

Alimshauri Spika Makinda kuwasiliana na vyombo vinavyohusika ili ofisi yake na kiti chake visitumiwe na watuhumiwa kuficha uharamia unaoendelea dhidi ya Bunge na uwajibikaji, ambao Bunge linapaswa kuusimamia kwa niaba ya wananchi.

Madai hayo ya Mnyika yalitolewa siku moja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, kukaririwa akisema kuwa katika mahojiano na polisi, kijana huyo alikiri kwamba, alipewa ripoti hiyo na Mbunge mmoja, ambaye alikataa kutaja jina lake ili kuepusha kuharibu upelelezi.

Vijana hao walikamatwa na polisi Jumamosi wiki iliyopita, mjini hapa, baada ya kukutwa wakiwa na ripoti hiyo yenye mhuri wa Katibu wa Bunge, ambayo wanadaiwa ‘kuichakachua’ kabla ya kuidurufu na kuisambaza mitaani kama njugu.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, pia alithibitisha kutoa taarifa polisi kuhusu vijana hao kumiliki nyaraka zenye muhuri wa ofisi yake isivyo halali.
Kamanda Misime alisema hadi juzi vijana hao walikuwa wanashikiliwa na polisi.

SPIKA ATAJWA KUVUNA ESCROW
Madai juu ya Spika Makinda kutajwa kuwamo katika orodha ya vigogo waliofaidi mgawo wa fedha hizo, yalitolewa bungeni jana na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, kupitia mwongozo aliouomba chini ya kanuni ya Bunge ya 68 (7).

Mnyaa alisema madai hayo ni katika mlolongo wa hali ya hewa kuchafuka mkoani Dodoma tangu mjadala kuhusu kashfa hiyo upambe moto bungeni.
Alisema hayo alipokuwa akijaribu kumshinikiza Spika Makinda aruhusu Bunge lisimamishe shughuli zake zote za jana lijadili suala la ripoti hiyo kuibwa, kudurufiwa na kusambazwa mitaani.

”Kwamba hivi sasa hali ya Dodoma kwa ujumla Mheshimiwa Spika imechafuka. Imechafuka. Kuna nyaraka zinasambazwa, wanatiliwa wabunge nyumbani mwao wanapoishi ambazo zina kuchafuliwa wabunge,” alisema Mnyaa.

Aliongeza: “Mheshimiwa Spika, katika kuchafuliwa, wameshachafuliwa wengine hawa wajumbe wa PAC (Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali). Na hivi sasa minong’ono hata wewe unatamkwa kwamba umechukua dola milioni moja na unatafutiwa documents (nyaraka) kusambazwa na wewe uchafuliwe.”

Kutokana na hali hiyo, aliomba suala hilo lijadiliwe na Bunge kama, ambavyo Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, alivyoomba kupitia hoja aliyoitoa bungeni jana.
Alisema mjadala kuhusu suala hilo ni mpana na kwamba, hauhusiani na kesi ya kukamatwa kwa vijana hao, ambayo iko polisi.

“Mjadala unahusiana na zile tulizosema haki na kinga za madaraka ya Bunge. Hili suala tunahitaji kujadili si kwa suala la kesi iliyoko polisi, tuna suala la kujadili haki na madaraka ya Bunge na namna gani Bunge lako liamue kutumia kiti chako,” alisema Mnyaa.

Aliongeza: “Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima tunaomba uruhusu mjadala huu japo kwa nusu saa ili tulishauri Bunge na kiti chako tuweze kuamua. Naomba kuwasilisha.”

SPIKA MAKINDA AJIBU
Baada ya Mnyaa kueleza hayo, alisimama Spika Makinda na kusema kama kweli naye amechukua dola milioni moja, basi wabunge watalionyesha hilo bungeni .

”Mtanionyesha, mtanionyesha,” alisema Spika Makinda na kusababisha kuzua zogo bungeni jana.

Awali, wabunge jana waliwasha moto bungeni, huku wakibishana, wakishinikiza kiti cha Spika kupeleka mapema ripoti hiyo ya CAG ili wapate muda mpana wa kuijadili.

Wabunge hao walichafua hali ya hewa kwa mara nyingine tena baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wakiunga mkono hoja ya Mbatia aliyetaka Bunge liahirishe shughuli zote zilizopangwa ili Spika awape wabunge muda wa kujadili hoja ya kusambazwa kwa ripoti hiyo ya CAG.

Mbatia aliomba mwongozo huo chini ya kifungu cha 51 cha kanuni za Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

“Mheshimiwa Spika naomba kutoa hoja ya kusitisha shughuli za kujadili suala linalohusu haki za Bunge lililotolewa katika kanuni ya 51 ya kanuni za Bunge toleo mwaka 2013,” alisema Mbatia.

Pamoja na mambo mengine, alisema inasadikiwa kuwa mtuhumiwa huyo anahusika katika kudurufu na kusambaza taarifa husika na mpaka sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi. Mbatia alisema inaonekana kuwa ripoti hiyo imeibiwa baada ya kupokelewa na Ofisi ya Spika, kwani katika ukurasa wa juu kabisa kuna muhuri unaosomeka ‘Ofisi ya Katibu wa Bunge’, imepokelewa Novemba 14, mwaka huu, sanduku la Posta 941 Dodoma.

Alisema kwa mujibu wa maelezo waliyopewa ni kuwa, inawezekana taarifa inayosambazwa imeibwa kabla ya kuwasilishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwani baada ya kuwasilishwa kwenye kamati hiyo kuna alama maalumu, ambayo iliwekwa kwenye nakala zote, ambayo haipo katika taarifa hiyo inayosambazwa.

“Mheshimiwa Spika, kitendo cha taarifa hiyo kusambazwa mitaani wakati kamati ya PAC ikiwa inaendelea na uchambuzi wake kinamaanisha kuwa kuna watu wamejipanga kuchafua uongozi wa Bunge hili, kushusha hadhi ya Bunge, kuzuia Bunge lisifanye kazi yake kikamilifu,” alisema Mbatia.

Aliongeza: “Kifungu cha 31(G) cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge sura 296 kinaainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote kusambaza nyaraka yoyote iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kabla ya wakati wake.”

Alisema kumekuwa na jitihada nyingi za wazi wazi na za kificho zinazoonekana kulenga kuzuia Bunge lishindwe kufanya kazi yake katika suala hilo.

Mbatia alisema wizi huo na usambazaji wa taarifa ya ukaguzi maalumu kabla haijawasilishwa bungeni, ni vitendo vinavyotakiwa kukemewa na kutolewa tamko kali la Bunge.
“Kwa kutumia kanuni ya 51 ya kanuni za Bunge ya toleo la Bunge la mwaka 2015, naomba kutoa hoja sasa Bunge lako lisitishe shughuli zake zilizopangwa kufanyika hivi sasa ili wabunge wapate fursa ya kulijadili suala hili kwa kina na kutoa maagizo yanayostahili kwa serikali. Mheshimiwa Spika kwa unyenyekevu mkubwa naomba kutoa hoja,” alisema Mbatia.

Hoja hiyo ya Mbatia, iliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye alisisitiza kutaka suala hilo lijadiliwe ili hali ya hewa iliyochafuka iondolewe.

Akijibu hoja hiyo baada ya wabunge kusimama kuiunga mkono, Makinda alisema hakubaliani nayo.“Hoja haikubaliki, hebu kaeni huko, huwa hakuna hoja ya aina hiyo. Kaeni, someni kifungu namba 51, naomba tusikilizane,” alisema Makinda.

Aliongeza: “kwanza kabisa mimi lazima nikiri kwamba namshukuru bwana Mbatia na wenzake kwa kazi waliyoifanya ya kuchunguza hiki wanachokisema, wamefanya kazi kubwa.” Alisema baada ya kufanya hivyo, aliyehusika amekamatwa na yuko ndani na kwamba, mpaka sasa Ofisi ya Bunge inashirikiana na polisi kutokumtoa huyo mtu mpaka aseme vitu alivyokuwa anavisambaza amevitoa wapi.

“Hiyo ndiyo kazi inayoendelea mpaka sasa hivi, wanafika mahali mpaka kutumia ofisi yao kubwa ya Dar es Saalam ili kutambulisha kwamba mashine zilizochapa zile ni za nani,” alisema Makinda.

Alisema kwa kutumia kifungu cha haki za wabunge na kinga namba 31, suala hilo linashughulikiwa na kwamba, mtuhumiwa huyo akithibitika alitenda ndiyo atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu au faini inayohusika.

Kutokana na hali hiyo, alisema suala hilo haliwezi kujadiliwa wakati mtuhumiwa huyo akiwa bado yuko ndani.

“Waheshimiwa wabunge, naomba tuelewane sisi ni wabunge, mnajadili kitu gani? Huyo mtu amewekwa ndani ‘ndiyo’ waheshimiwa wabunge sikilizeni hatuendeshi Bunge kwa kupiga kelele tuelewane, nasema hili swali tunaliacha kwanza, nawaambia mi nitapanga muda, tukipata taarifa ya polisi,” alisema Makinda, huku akizongwa na makelele ya wabunge.

Akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), Spika Makinda alisema ofisi yake inalishughulikia kwa umakini mkubwa suala hilo na mara tu uchunguzi wa kamati na ule wa polisi utakapokamilika ripoti hiyo itapelekwa bungeni na wabunge watapata fursa ya kujadili na kufikia maamuzi.

“Wabunge msiwe na wasiwasi hili suala liko wazi na linakwenda kwa utaratibu hivyo vuteni subira tutalileta humu ndani na litajadiliwa,” alisema Makinda.

Alisema ofisi yake imeshaweka utaratibu wa kuhakikisha ripoti ya CAG inawafikia wabunge mapema iwezekanavyo kabla ya kufikishwa kwa taarifa ya PAC bungeni.

Spika Makinda alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha wabunge kupata muda mzuri wa kuisoma ripoti hiyo na kuielewa vizuri kabla ya kuanza kuijadili Novemba 26, 27 na 28 itakapowasilishwa mbele ya Bunge.

Alisema ofisi yake imeiongezea nguvu PAC kwa wajumbe watatu, ambao ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), Mbunge Mwibara, Kangi Lugola (CCM) na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangwalla (CCM). Katika muongozo wake aliouomba chini ya kanuni ya 68 (7), Sendeka alitaka kujua ni kwanini Spika asimuelekeze Katibu wa Bunge kuhakikisha ripoti ya CAG inapatikana kwa wabunge jana badala ya kupatikana mitaani ili waisome pamoja na vielelezo vyake na kuitendea haki.

KAMANDA MISIME
Kamanda Misime alisema jana kuwa bado wanamshikilia mtu mmoja (hakutaja jina) anayehusishwa na usambazaji wa nyaraka hizo.

Alisema kwa sasa utambulisho wa mtu huyo unahifadhiwa, ili kulinda mazingira ya upelelezi wanaoufanya kuhusu tukio hilo, ambapo inadaiwa kuwa nyaraka hizo ziliibwa kwenye ofisi za viongozi wakuu wa Bunge.

“Kwa sasa tunachunguza mambo mengi nyeti, ikiwamo kubaini kama nyaraka hizi ni ripoti halisi za Takukuru na CAG, ikiwa muhuri uliyo kwenye nyaraka hizi ni wa Katibu wa Bunge na uhusiano uliyopo kati ya mmoja wa watuhumiwa wa Escrow na huyu jamaa,” alisema. Misime.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: