ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 14, 2015

Jaji Mkuu: Majaji Escrow niachieni

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, ametaka suala linalohusu majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa na Aloysius Mujulizi, waliotajwa kupata mgawo katika fedha zilizochotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aachiwe kulishughulikia mwenyewe.

Jaji Othman Chande alitoa kauli hiyo kupitia Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Ignas Kitusi, aliyezungumza na NIPASHE, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana.

Kitusi alisema alielezwa hayo na Jaji Othman walipoongea naye hivi karibuni kufuatia NIPASHE kutaka kujua hatua, ambazo zimeshachukuliwa na Jaji Mkuu kuhusiana na tuhuma zinazowakabili majaji hao.

“Tuliongea na Jaji Mkuu, akasema suala hilo analifanya yeye. Hivyo, sisi wengine haturuhusiwi kuliongelea,” alisema Kitusi.


Awali, Naibu Katibu wa Jaji Mkuu, Kevin Mhina, alimweleza mwandishi ofisini kwake, wiki iliyopita kuwa aliwasilisha swali hilo la NIPASHE kwa Jaji Othman, lakini hakutoa jibu lolote.

“Nilim-brief (nilimweleza) Mheshimiwa Jaji Mkuu, lakini hakujibu kitu. Tafsiri yake, hayuko tayari kuzungumzia suala hilo,” alisema Mhina, ambaye baadaye alisisitiza kuwa Jaji Mkuu hana utaratibu wa kuzungumza na mwandishi wa habari mmoja mmoja.

Hata hivyo, alimshauri mwandishi kumuona ama Mtendaji Mkuu wa Mahakama au Msajili Mkuu akisema wawili hao ndiyo wasemaji wa Mahakama ya Tanzania.

Mwandishi aliwasiliana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga, lakini kupitia kwa katibu muhtasi wake, alimshauri mwandishi kurudi kwa Jaji Mkuui kwa maelezo kwamba, ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo.

Jaji Mujulizi na Jaji Ruhangisa walitajwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), bungeni, kuwamo miongoni mwa vigogo waliopewa mgawo katika fedha hizo na mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.

Kwa mujibu wa PAC, fedha zinazodaiwa kuchotwa kutoka akaunti hiyo, ni zaidi ya Sh. bilioni 300 wakati kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, ni Sh. bilioni 202.9.

Wengine waliotajwa kufaidika na mgawo wa fedha hizo, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6).

Tayari Prof. Tibaijuka ameshatimuliwa kazi na Rais Kikwete kwa kupokea fedha hizo kupitia akaunti yake binafsi iliyoko benki ya Mkombozi, badala ya akaunti za shule na kwamba ni kinyume cha maadili.

Wengine waliopata mgawo kutoka katika fedha hizo, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh. bilioni 1.6i); Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga Mjini (CCM), Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).

Pia wamo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh. miliobi 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), Jaji Profesa Ruhangisa (Sh. milioni 404.25) na Jaji Mujulizi (Sh. milioni 40.4) pamoja na Mkurugenzi mstaafu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).

Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8); Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.9); Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa (Sh. milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).

Hatua dhidi ya majaji hao ni utekelezaji wa moja ya maazimio nane ya Bunge lililokuwa likimtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi yao.

Akihutubia taifa kupitia wazee wa Dar es Salaam Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete, alisema amelipokea azimio dhidi ya majaji hao na kulijadili na washauri wake.

Hata hivyo, alisema itabidi wafuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo.

Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa utaratibu huo, inatakiwa suala kama hilo lianzie kwenye mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge.

Alisema Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua jaji yeyote pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo.

“Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa,” alisema Rais Kikwete.

Katika hatua nyingine,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema inasubiri wateja mbalimbali wakiwamo waliopata mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, kupeleka hesabu zao ili wapige hesabu na kujua kodi inayostahili kutozwa.

Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, iliyotaka kujua ni kodi kiasi gani imekusanywa kutokana na fedha za mgawo wa Escrow, alisema ili kupata kiasi cha kodi ni lazima wahusika wajaze fomu.

“Mtu yoyote anayepata kipato ni lazima alipe kodi, tumetoa muda wa siku 30, wajaze fomu za hesabu zao tunalinganisha na mapato yao na kisha tunafanya makadirio ya kodi…kodi ni lazima ilipwe kwa mtu yoyote anayepata kipato,” alisema na kuongeza:

“Sheria hairuhusu kuweka wazi taarifa za mteja, tunachoangalia ni kodi inayolipw akwa wote tunalinganisha alichojaza kwenye fomu, tunafanya uchunguzi na kujiridhisha juu ya kile alichoandika,” alisema.

Hata alivyotakiwa kuzungumzia fedha za mgawo wa akaunti ya Escrow, alisema kodi inatozwa kwenye fedha zote na siyo hizo pekee.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: